Articles by "MAOMBI"
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MAOMBI. Onyesha machapisho yote
Wakristo wengi ni wepesi wa kwenda mbele za Mungu kupeleka Maombi, Dua na Sala zao kwa BWANA, ila si wepesi wa kupokea toka kwa Mungu.
Wanaamini Mungu anayakubali na kuyapokea maombi yao, sala na dua ila hawana UHAKIKA KAMA MUNGU AMEJIBU AU LA! Wengi wanaishia kubahatisha…Ni kama wanajaribu labda uenda BWANA YESU atawapa kile walichoomba.
Ila hili si tatizo la kizazi hiki cha WAAMINI, Lipo tangu zamani kabisa…leo ninayo mifano miwili…ebu jifunze pamoja nami;


1.ZEKARIA BABA YAKE YOHANA MBATIZAJI
Huyu alikuwa KUHANI (Mtumishi wa Madhabahuni) kama mimi, ambaye alikuwa na uhakika na NGUVU NA UWEZA wa Mungu katika kujibu na kushughulikia mahitaji na haja za watoto wake! Maana kila mara alikwenda PATAKATIFU PA PATAKATIFU kupeleka haja, mahitaji na maombi ya Watu wa Israel (Luka 1:5)
Kwa hiyo tangu ujana wake alikwisha dhibitisha ya kuwa Mungu yu hai na ni halisi na anajibu maombi…Hakuwa mgeni kuhusu tabia ya Mungu kujibu maombi.
Lakini cha ajabu, kuna wakati yeye mwenyewe aliwahi kuomba kwa Mungu ili ampe mtoto, maana mkewe alikuwa tasa (Luka 1:6) lakini Mungu alipoleta jibu kupitia kinywa cha malaika Gabrieli, Mzee Zekaria alianza KUUFUTA MUUJIZA WAKE…Hata ikambidi Malaika Gabriel amfunge mdomo [awe bubu kwa muda wote wa mimba ya Yohana Mbatizaji] ili asije akaufuta ule Muujiza (Soma Luka sura ya kwanza utagundua jambo hili, na utapata ufunuo huu)
Kama alivyofanya Zekaria, wengi wetu pia tuna tatizo la kuibatilisha miujiza yetu…Mungu anapotuma majibu ya maombi yetu, anatukuta tukiwa busy na KUTOAMINI kwingi mioyoni mwetu na MANENO YALIYO KINYUME NA KILE TULICHOOMBA NA KUUBATILISHA MUUJIZA HUSIKA…Kwa Zekaria alipata neema ya kufungwa kinywa ili muujiza ukae, wewe unaye Roho Mtakatifu na Neno la Mungu…Umalizapo kuomba, usiruhusu Maneno na mawazo yaliyo kinyume na Ulichokiri wakati wa maombi mbele za BWANA!
TUMBO LA MTU HUSHIBA MATUNDA YA MIDOMO YAKE (Mithali 18:20-21)
TUNZA MUUJIZA WAKO MARA BAADA YA MAOMBI USIRUHUSU MANENO YAKO YANAYOANGALIA KILE KILICHOKUZUNGUKA KUHARIBU MUUJIZA WAKO…Kumbuka, “Tunaenenda kwa Imani na si kwa kuona” (2Kor 5:7)!

MITUME; PETRO ALIPOFUNGWA
Ukisoma Matendo 12 yote, utaona tukio hili…
Kuna wakati Mfalme Herode alimuua Yakobo, na kisha akamweka Petro Gerezani.
Na Biblia inasema KANISA likamwomba Mungu kwa ajili yake (Matendo 12:5)
Kumbuka: Hawa walikuwa Mitume, ambao Mungu aliwatumia kutenda Ishara, maajabu na Miujiza Mikubwa. Na hapa walipatana ya kuwa watakesha usiku kucha wakimwomba Mungu ili amtoe Petro gerezani naye asiuwawe kama Yakobo.
Biblia inasema Mungu aliyasikia maombi yao, na usiku wa manane, Mungu alimtuma Malaika wake akaenda mle gerezani akamtoa Petro na kumpeleka hadi pale wale Mitume [kanisa] WALIPOKUWA WAKIENDELEA KUOMBA…
Kijakazi akasikia mlango ukigongwa, akaenda kusikiliza ni nani anayegonga…alipofika na kugundua kuwa ni Petro, alirudi bila kumfungulia mlango, akawanyamazisha wale WAOMBAJI na kuwaambia Petro yuko pale nje anagonga…KWA LUGHA NYINGINE ALIKUWA ANAWAAMBIA, “ACHENI KUOMBA, MAOMBI YAMEJIBIWAAAA, YESU AMETENDA…”
Cha kushangaza, badala ya wale ndugu kuungana na huyu kijakazi kumshukuru na kumtukuza Mungu kwa kujibu maombi yao, wao walimgeukia kwa pamoja na wakamwambia, “WEWE VIPI? UNA WAZIMU NINI? PETRO ANAGONGA? HAIWEZEKANI? ACHA TUOMBE HADI ASUBUHI, MUNGU ATATENDA…UMETUKATISHA MAOMBI YETU…UMEUKATA UWEPO WA MUNGU, TENA SIKU NYINGINE USIRUDIE…” (Hapa nimeweka msisitizo kama Mwalimu)
Kwa kweli inashangaza…inaonesha waliamua kuomba KAMA KUJARIBU HIVI…au WALITEGEMEA MUNGU ATAMTOA PETRO KWA NJIA WANAZOJUA WAO…WALIJARIBU KUFIKIRIA KWA JINSI YA KIBINADAMU (Kama wewe unavyajaribu kumpangia Mungu namna ya kukusaidia au kushughulikia mahitaji yako; acha utoto, USIMWEKEE MUNGU WANGU MIPAKA; HE IS OMNISCIENT, OMNI PRESENT and OMNIPOTENT…Mawazo yake na njia zake ziko juu sana, na hazichunguziki: Isaya 55:8-11)


MUHIMU:
Unapoingia mbele za Mungu kuomba, ukiwa na uhakika ya kuwa kile unachokiomba kiko sawa na Mapenzi ya Mungu (NENO LAKE) uwe na uhakika ya kuwa Mungu amekusikia sekunde hiyohiyo, na kama amekusikia, tayari unazo haja zote ulizomwomba (1Yohana 5:14-15)
Yesu alisema, “YEYOTE ATAKAYEUAMBIA MLIMA HUU NGOKA NA UJITOSE BAHARINI, WALA ASIONE SHAKA MOYONI MWAKE, BALI AAMINI YA KUWA YALE ALIYOSEMA YAMETUKIA [sio yatatukia bali yametukia] YATAKUWA YAKE” (Marko 11:23)
KUOMBA SI KAZI, KAZI NI KUPOKEA YALE UYAOMBAYO…ACHA KUOMBA, POKEA MAJIBU YA MAOMBI YAKO SASA!

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na kisha tuombe maombi ya ushindi.
Nakumbuka kuna siku nilikufundisha somo lisemalo MAOMBI YA KUMUOMBEA MTU ALIYEBEBA KUSUDI LA MUNGU KWA AJILI YAKO na kuna watu  walinipa shuhuda juu ya somo hilo la maombi, Lakini namshukuru ROHO MTAKATIFU maana amenipa somo lingine la maombi kwa ajili yako ndugu, somo hili ni tofauti na somo la kwanza, hili linasema MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUINULIE WATU ILI KUFANIKISHA KUSUDI LA MAFANIKIO. Kuna tofauti kati ya kuomba MUNGU akuinulie watu na kumuomba MUNGU awafanye kutimiza lengo wale walioinuliwa tayari kwa ajili yako. Nimeaanza hivyo ili usidhani ni somo moja, Sasa tunaendelea.
Jambo la kwanza kabisa nataka ujue katika somo hili ni kwamba usimtegemee mwanadamu wa aina yeyote kukuinua bali mtegemee MUNGU anayeweza kukuinulia watu ili ufanikiwe.
Kumbuka kuwatumainia wanadamu ni kosa mbele za MUNGU maana tendo la kuwategemea wanadamu huleta laana.
Yeremia 17:5 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.''

 Baada ya kukujenga katika hilo sasa naomba ujue kwamba MUNGU anao uwezo wa kukuinulia watu ili tu wewe ushinde au ufanikiwe.
Iko mifano mingi kwenye Biblia ya jinsi ambavyo MUNGU aliwainuliwa watu kundi lake ili washinde au wafanikiwe.
Acha tuone mifano hii.
1. MUNGU aliwainuliwa waisraeli Musa ili MUNGU awatoe Misri hao waisraeli kupitia huyo Musa.
Waisraeli kama ilivyo kwako leo walikuwa katika wakati mgumu sana lakini Baada ya maombi Biblia inasema hivi. 
Kutoka 2:23''Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa MUNGU kwa sababu ya ule utumwa.'
 Baada ya maombi yao kufika kwa MUNGU Biblia inaendelea kusema '' Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. - Kutoka 3:9-10 ''
 MUNGU aliwainulia Waisraeli Musa ili kuwatoa Misri.
Hata wewe kwa maombi yako ya kumwambia MUNGU akuinulie watu anaweza kukuinulia watu wa kukutetea katika ukoo wako unaokukataa, anaweza kukuinulia watu ili uajiriwe serikalini,hakikisha Ttu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai, anaweza kukuinuliwa watu ili kukuombea, anaweza kukuinuliwa watu ili wawapige maadui zako na wewe ushinde vita ya kiroho.
Inawezekana kuna jambo gumu sana kila ukijaribu unashindwa, leo mwambie MUNGU akuinulie watu wa kufanikisha jambo hilo.

2. Yoshua alipewa na MUNGU jukumu la kuwarithisha waisraeli maeneo.
Yoshua 1:16 '' Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. '
 Inawezekana kuna haki yako fulani unatakiwa uipate, umezungushwa sana na kuonewa kwa sababu walio katika maamuzi ya kukupatia haki yako sio watu wazuri, leo omba MUNGU akuinulie watu katika nafasi hiyo ili wewe ufanikiwe.
Inawezekana unashindana mahakamani  au kwenye mabalaza na mtu mwenye nguvu au tajiri, inawezekana ana ushawishi mkubwa kiasi kwamba hakuna anayekujali wewe wala kukusikiliza, leo muombe Bwana YESU akuinulie watu katika nafasi ya maamuzi ili ufanikiwe, hakikisha tu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Unaweza ukashangaa meneja au mkurugenzi au mkuu wako aliyekuwa anakuonea sana, baada ya maombi akapata uhamisho wa ghafla kumbe analipisha kusudi la MUNGU la kufanikiwa kwako, maana atakayechukua nafasi yake atakuthamini wewe na atakuwa mtu wa haki hivyo haki yako utaipata kirahisi sana.

3. Othnieli aliinuliwa na MUNGU kwa ajili ya kuwasaidia waisraeli dhidi ya maadui zao wenye nguvu.
Waamuzi 3:9-10 '' Kisha wana wa Israeli walipomlingana BWANA, BWANA akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. ROHO  ya BWANA ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye BWANA akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.''
 Biblia inasema walipomlingana MUNGU yaani walipotoa haja za mioyo yao kwa MUNGU yeye MUNGU aliwainulia Mtu na mtu huyo akawa chanzo cha ushindi wao dhidi ya maadui kwa miaka 40.
Unaweza ukamuomba MUNGU akuinulie watumishi wake ambao watakapokuombea majini waliokutesa watakuachia tangu dakika hiyo hadi uzeeni mwako, hakikisha tu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Inawezekana mtaani kwenu kumejaa ushirikina na uko hatarini kwa sababu wachawi wanakuwinda ili wakumalize, unaweza ukaomba MUNGU akuinuliwe watu na ukashangaa MUNGU akainua waombaji au MUNGU akamtuma mtumishi wake kufungua kanisa mtaani hapo na utashangaa wachawi wote wanatoroka mji maana nguvu ya MUNGU itawapiga na hawatakaa tena eneo hilo, kuna jinsi nyingi sana MUNGU anaweza akakuinulia watu ili wewe uwashinde madui zako. Unaweza ukashangaa sana yule aliyekuwa anakutisha na kukukosesha amani mara unamuona Polisi wamemkamata kwa makosa yake lakini hali hiyo ikawa na manufaa kwako maana hatakutisha tena, yaani hapo MUNGU anakuwa amekuinuliwa vyombo vya sheria ili tu wewe usiteseke tena, kuna njia nyingi mno.

MUNGU aliwainulia Daudi ili awe mfalme badala ya Sauli aliyewataabisha. Unajifunza nini?
Kuna watu wakikaaa tu kwenye ofisi fulani utasikia ajira zinatangazwa na wewe unapata kazi, hakikisha tu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kuna watu MUNGU anaweza kuwainua na wamebeba kusudi lake kabisa la kufanikiwa kwako.

Kwanini MUNGU akuinulie watu?

1. Ili watimize kusudi la MUNGU la wakati huo kwako.
Wafilipi 2:13 '' Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.''
Inawezekana kabisa umekosa mchumba lakini MUNGU anaweza kukuinulia mtu atakayeitimiza ahadi ya MUNGU kwako kwamba utafunga ndoa, mtu huyo atakupenda na kukuthamini hata kama wewe ngine wanakuona mbaya au wanakuona takataka, lakini aliyelibeba kusudi la MUNGU kwako atakuona unavaa sana  hata mpaka anaanza kujiuliza kwanini hakukufahamu mapema.
Inawezekana kusudi la MUNGU ni wewe ukue kiroho hivyo MUNGU anaweza kukuinulia mtumishi ili kukusaidia katika jambo hilo na hapo atakuwa analitimiza kusudi la MUNGU.
Mimi Mabula sitasahau mwaka 2012 ambapo MUNGU aliwainua watu wawili wakafunga siku 5 kila mmoja  ili kuniombea, mmoja alikuwa Mwanza na mwingine Dar es salaam, watu hawa wala hawakujuana na hata hawakujua niko katika hali gani lakini ROHO wa MUNGU aliwaonyesha hatari iliyokuwa inaniandama hivyo wakajikuta wanafunga na kuomba kwa siku 5 kuniombea mimi, hao walikuwa wanalitimiza kusudi la MUNGU. MUNGU ana njia nyingi sana za kuwafanya watu walitimize kusudi lake kwako. Sitasahau siku moja Mwanamke mmoja ambaye hatujawahi kuonana ila huwa ananifuatilia tu mtandaoni akijifunza masomo yangu, siku moja alinitumia Tsh 50,000 na nilisita kuitumia maana maana niliogopa lakini nilipokuja kumuuliza aliniambia jambo la ajabu sana, alisema kwamba aliambiwa rohoni na akakoseshwa amani hadi aliponitumia ndipo akawa na amani na MUNGU akasema na yeye kitu. Nilishangaa sana hata nikakosa majibu  ya kumweleza, ila wakati pesa hiyo inatumwa nilikuwa katika wakati mgumu sana sana lakini MUNGU akamwinua ili kunisaidia, hivyo ndivyo MUNGU anaweza kuinua watu kwa ajili yako. Hata siku nyingine tena kuna mtu alinitumia kiasi fulani cha pesa na nilipoongea naye kwenye simu niliishia tu kumwambia kwamba '' Hakika Wewe una ROHO wa MUNGU'' Maana ni kama MUNGU aliona nini kinaendelea kwangu hivyo akaniinuliwa watu kunisaidia.

2. Ili wakuletee jibu la MUNGU la maombi yako.
Isaya 38:14-15 '' Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.''
Tunafahamu habari hii vyema sana kwamba Hezekia alikuwa anaumwa sana na aliambiwa atakufa muda mfupi baadae. Yeye baada ya kuambiwa hivyo aliamua kugeukia ukutani na kuomba mbele za MUNGU na MUNGU akamuinulia Isaya Nabii kumletea majibu ya maombi yake kwamba atapona na kuongezewa miaka ya kuishi.
MUNGU anaweza akamwinua mtu kukuletea majibu ya maombi yako ambayo umeomba muda mrefu.
Sitasahau siku za karibuni nilikuwa nawaombea watu kwa simu, siku hiyo nilikuwa naombea watu zaidi ya 20. Wakati namuombea mtu wa kwanza nilisikia sauti ikisema ''Waambie wote utakaowaombea leo kwamba MUNGU anaenda kutenda jambo jipya la muujiza'' Kisha nikapewa andiko la Zaburi 35:8 ili kuwaombea dhidi ya maadui zao. Niliwaombea nikiwambia kwamba MUNGU anaenda kutenda jambo jipya baada ya maombi  nikalala na nilipoamka asubuhi nilikuta meseji za watu watatu katika lile kundi ambalo niliwaombea wakisema kwamba hakika MUNGU amefanya jambo jipya, kila mtu akanipa ushuhuda wake. Hapo ndipo nikaelewa kwanini MUNGU alisema atatenda jambo jipya. Ndugu unaweza kumuomba MUNGU akuinulie watu na akawainua wa kukuletea majibu yako kutoka kwa MUNGU na ukashinda vita ya kiroho uliyokuwa unapitia.

 3. Ili wewe umtukuze MUNGU kwa  kukujibu mahitaji yako kwa njia hiyo.
2 Wafalme 5:14-15  ''Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa MUNGU; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa MUNGU, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna MUNGU duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.''
 Inawezekana walikuwepo watumishi wa MUNGU wengi tu waliomuombea Naamani ili apone ukoma lakini hakupona, lakini siku moja MUNGU akamuinulia Elisha na Elisha akampa Naamani Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU uliopelekea Naamani kupona ukoma uliomtesa miaka mingi.
Naamani baada ya kumponywa alisema Neno hili  ''Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna MUNGU duniani mwote, ila katika Israeli ''
Naamani alimtukuza MUNGU aliye hai kwa sababu alitendewa ,uujiza wake baada ya kukutana na watu walioinuliwa na MUNGU kwa ajili yake.
Hata wewe inawezekana una mateso sugu sana, inawezekana unanyanyaswa sana, inawezekana unataka kufukuzwa hata katika nyumba uliyoijenga mwenyewe. Ndugu Unaweza kuomba maombi ya kumuomba MUNGU akuinuliwe watu wa kukusaidia na ukashangaa MUNGU anakuletea watu ambao wataguswa na matatizo yako na kukusaidia kiajabu sana.

4. Ili MUNGU aweke nguvu zake ndani yao kwa lengo la kukusaidia wewe.
Waamuzi 2:18 '' Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.'
MUNGU anaweza akaweka nguvu zake ndani ya watu fulani ili kuwasaidia watu wengine.
Inawezekana una maadui wengi mno kazini kwako, lakini MUNGU anaweza kukuinulia marafiki wenye nguvu sana kiasi kwamba maadui zako watajikuta wanakukimbia na kukuogopa.
MUNGU anaweza kukuinulia mtumishi Mwaminifu wa KRISTO ambaye atakuombea na utashinda kila kikwazo cha kipepo. 
MUNGU anaweza akakuinulia mtu wa kukusaidia na ndani ya Mtu huyo MUNGU akaweka nguvu za kumfanya mtu huyo kukusaidia na kukuletea ushindi.
Ndugu muombe MUNGU akuinuliwe watu.

 MUNGU Baba anaweza kukuinuliwa watu wa kukusaidia katika kila eneo la maisha yako au kila eneo la hatua zako za ushindi, ili wewe umtukuze MUNGU.
Mama mmoja mjane alikuwa anateswa na madeni ya mume wake marehemu na hadi watoto wake wanataka kuchukuliwa ili kufidia Madeni hayo. Siku moja mama yule akamwendea Elisha aliyekuwa ameinuliwa na MUNGU kwa ajili ya mama yule. Elisha alimuomba MUNGU na MUNGU akatenda muujiza na madeni yakaisha tangu siku hiyo kwa yule mama, Hiyo iko 2 Wafalme 4:1-7.
Hata wewe inawezekana uko katika tatizo la muda mrefu na gumu sana kwako lakini MUNGU anaweza akakuinulia mtu wa kuliondoa tatizo hilo kwa dakika 5 tu, ndugu leo omba MUNGU akuinulie watu ili kufanikisha kusudi la maendeleo.

 MUNGU aliwainulia Ayubu akina Elifazim Mtemani na marafiki zake wawili ili huyo Ayubu aliyeinuliwa kwa ajili yao awaombee msamaha kwa MUNGU ndipo watasamehewa. Hiyo iko Ayubu 42:7-8 '' ''
Hata wewe unaweza ukainuliwa watu wa kukuombea, kukupatia kazi, kuombea huduma yako au biashara yako n.k
 Samweli aliwaombea Israeli, Musa aliwaombea Israeli  ili wasiteketezwe, hata wewe wanaweza wakainuliwa watu kukuombea ili ufanikiwe.
 MUNGU alimwinulia Eliya mama mjane ili amlishe chakula.
1 Wafalme 17:8-9 ''Neno la BWANA likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.'
 Hata wewe MUNGU anaweza kukuinulia watu kukuhudumia katika wakati mgumu.
 MUNGU alimuinulia mama Mshunemu nabii Elisha ili Mtumishi huyo wa MUNGU aombe na mama yule apate uzao na akapata, hiyo iko 2 Wafalme   4:16-17.

 Hata wewe katika vifungo , katika jaribu, katika uonevu wa nguvu za giza, katika kuteswa na madhabahu za giza n.k MUNGU anaweza kukuinuliwa watu na kupelekea ushindi kwako, mtukuze tu MUNGU baada ya muujiza wako na hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.

Maombi ya leo.
1. Omba MUNGU akuinulie watu katika kila eneo la maisha yako.
2. Omba MUNGU watu hao wakae katika nafasi zao sawasawa na kusudi la MUNGU.
3. omba kwa MUNGU kwamba upate neema na kibali mbele ya watu hao.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni 
MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUINULIE WATU ILI KUFANIKISHA KUSUDI LA MAFANIKIO.   Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 


MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUINULIE WATU ILI KUFANIKISHA KUSUDI LA MAFANIKIO.



 Ninakushuru MUNGU Baba kwa kuwa wewe u mwema, na kwa maana fadhili zako ni za milele.
Niko hapa BWANA naomba usisamehe dhambi zangu zote na uovu wangu wote. Neno lako linasema Katika 1 Yohana 1:8-9kwamba ''Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.'' Eee MUNGU wangu katika jina la YESU KRISTO  naomba unisamehe tu BWANA, nisamehe kwa makosa yangu yaliyosababisha nikawa kinyume na kusudi lako, nisamehe BWANA kwa makosa ya wazazi wangu na mababu zangu yaliyosababisha mimi niwe katika agano la urithi la uovu, naomba unitakase na damu ya YESU KRISTO initenge mbali na hilo agano la urithi la kipepo. Nakuomba nipe nguvu za kushinda dhambi, makosa na uovu na kuanzia leo nitakuwa Mteule wako ninayeishi maisha safi ya Wokovu wako Bwana YESU mwokozi wangu.
Niko BWANA mahali hapa nikiomba juu ya watu utakaowatumia ili kufanikisha kusudi la maendeleo na mafanikio kwangu.
Eee MUNGU Baba nakuomba niinulie watu ambao watafanikisha kufanikiwav kwangu kiroho na kimwli.
Katika kutaka kazi nahitaji BWANA uniinulie watu wa kuniajiri na kunilipa mshahara mzuri.
Katika kupona kwangu nahitaji watu BWANA wa kutimiza kusudi lako la uponyaji kwangu.
Eee MUNGU Baba ahadi yako katika Neno lako Yeremia 33:6inasema kwamba utaniponya na kunipa afya njema, Eee Bwana YESU nakuomba uniponya na mahali ambapo panahitaji kuniinulia watu Eee BWANA nakuomba uniinulie watu ili nitoke katika vifungo vyote vya giza.
Eee MUNGU Baba ahadi yako katika Mwanzo 2:24 ni kwamba mimi nifunge ndoa takatifu mbele zako, Eee MUNGU wangu nakuomba niinulie uliyemkusudia ili awe mwenzi wangu wa ndoa, mwinue wakati huu ili kunitimiza kusudi lako la mimi kuwa katika ndoa takatifu niliyofunga Kanisani mbele za watumishi wako.
 Eee MUNGU Baba ahadi yako katika Neno lako Waebrania 1:14 ni kwamba Malaika zako watanihudumia kwa sababu mimi ni mteule wa KRISTO, Eee BWANA nakuomba niinulie malaika ambao watanihudumia na Malaika ambao watalinda na kuniokoa kama ahadi yako inavyosema katika Zaburi 91:11
Katika kazi Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu.
Katika safari na katika Biashara  Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu, niinulie wateja na watetezi wa ajira yangu.
Katika kesi mahakamani inayonikabili na katika wadeni wangu, Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu.
 Katika kila baraka yangu ambayo inazuiliwa kipepo, Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu uliowakusudia wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu.
Sasa katika jina la YESU KRISTO ninaomba kila aliyeinuliwa na MUNGU ili kunisaidia namuombea kwa MUNGU kwamba akae katika nafasi yake itakayoleta ushindi wangu.
Nawafukuza wote waliokalia nafasi kiuongozi za kunididimiza mimi na kunifanya nisifanikiwe katika kazi yangu.
Naamuru kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO Mwokozi kwamba viongozi wakuu wawatoe au kuwahamisha wale wote walioshikilia nafasi na kunionea au kunididimiza, na sasa namuru yule ambaye ni kusudi la MUNGU ili mimi nifanikiwe huyo ndiye akae katika nafasi yake iliyo na kusudi la MUNGU ili kunisaidia mimi.
Eee MUNGU Baba ninaomba kwa rehema zako na neema mimi nipate kibali na neema mbele ya wote uliowainua ili wanisaidie.
Neno lako linasema kwamba '' Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.-Mwanzo 39:21'' Eee MUNGU uliyekuwa pamoja na Yusufu, Ukampa Yusufu kibali mbele za wanadamu na pia ukamfadhili, nami naomba Eee YAHWEH MUNGU wa uzima uwe nami, unipe kibali na Neema mbele ya kila uliyemwinua kwa ajili yangu ili kufanikiwa, Eee MUNGU wangu, na iwe hivyo kwangu katika jina la YESU KRISTO.
Eee MUNGU Neno lako katika Esta 2:17 Linasema kwamba ulimpa Esta Neema mbele ya Mfalme na tena ukampa Esta kibali cha kipekee mbele ya macho ya mfalme, Eee MUNGU ninaomba unipe neema na kibali mbele za mwenzi wangu, mchumba wangu aliye kusudi lako, nipe neema na kibali mbele ya wazazi wangu na wafanya kazi wenzangu wote, nipe neema na kibali mbele ya ndugu zangu na wakuu wangu wa kazi na kila aliyeinuliwa na wewe kwa ajili ya kunifanikisha, nakuomba Eee BWANA nipe neema na kibali mbele zake na sasa kusudi lako litimie. Mimi naamini hakika imekuwa katika jina la YESU KRISTO.
Mimi naamini kabisa kwamba imekuwa sawasawa na nilivyoomba.
Katika jina la YESU KRISTO mwokozi aliye hai nimeomba na sasa ninashukuru.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
+255714252292.
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.



AINA ZA MAOMBI YA KUFUNGA
----------------------------------------------------
Ushuhuda:
‘Mtumishi nashukuru sana kwa somo hili la maombi ya kufunga. Nataka nitoe ushuhuda halisi wa mimi mwenyewe jinsi maombi ya kufunga yalivyokata kiu ya dhambi ya uasherati. Mimi nilikuwa nimeokoka na nilikuwa nikianguka sana kwenye dhambi ya uzinzi pamoja na kwamba nimeokoka. Nilivyokaa na kuzingatia sana nikajuta ndani yangu. Nikachukua dhamira ya dhati nikaanza kufunga na kuomba mara 2 kwa wiki. Mtumishi tamaa yote ya dhambi ikamezwa na nguvu ya maombi ya kufunga”

-----------------------------------------------------
Tumsifu Yesu Kristo mwana wa Mungu.
Mwana wa Mungu, jana nilitoa utangulizi wa somo la maombi ya kufunga. Muhimu kujua kwamba kusudi la msingi la maombi ya kufunga ni kuutafuta uso wa Mungu ktk mambo fulani fulani.

Na pia ni vizuri kujua kwamba kufunga na kuomba ni kazi ngumu. Tunapaswa kuiruhusu neema na hekima ya Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu vikuongoze kufunga na si matamanio yako binafsi. Tunaweza kufunga na kuomba iwapo tu tutakubali Roho Mtakatifu atufundishe na tuwe na utayari. Hakuna jambo mwanadamu atalifanya kwa uzuri wake pasipo neema ya Mungu na kujizoeza kwalo. Narudia neno hili kila leo kuna mazoezi ya kiroho ndugu zangu. Paulo amwambia Timotheo ‘jizoeze kupata utauwa’.

Tukitaka jambo lolote ktk kumtumikia Mungu tulifanye kwa uzuri wake lazima tujizoeze kulifanya. Kama ni kuhubiri injili, kufundisha, kuombea watu, kumtolea Bwana n.k. n.k. Ni lazima tujizoeze ndugu yangu haya mambo. Ni lazima tujizoeze kuishi maisha ya utakatifu Ni lazima tujizoeze kufunga na kuomba.
Tunapofunga na kuomba tunayatafuta mapenzi ya Mungu katika jambo Fulani. Bwana Yesu alitufundisha kuomba na akasema tuombapo tuombe ya kwamba “Mapenzi ya Mungu yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni” #Mathayo 6:10. Kwa hyo kusudi la kufunga na kuomba ni kuyatimiza mapenzi ya Mungu hapa duniani kama huko mbinguni! Kuyatimiza mapenzi katika hayo tunayoutafuta uso wa Mungu.


Kufunga na kuomba hakumfanyi Mungu ayabadilishe mapenzi yake. Hatufungi kuwaonyesha wanadamu ya kwamba sisi ni wa kiroho sana. Kwamba labda twamjua Mungu sana. Hapana. Tunayatafuta mapenzi ya Mungu maishani mwetu. Haijalishi umeokoka miaka mingi ilopita au hivi karibuni.

Tukumbuke maneno ambayo Mungu aliyasema ktk 2Nyak 7:14 “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao”

Kwa kufunga na kuomba tunamruhusu Roho Mtakatifu azihuishe nafsi zetu na kutufanya tuweze kusikia sauti ya Mungu na kumtii katika maisha yetu.

Kwa ujumla Tunafunga ili:

• Kuna watu wanafunga kwa sababu za kimwili kabisa. Kwamba miili yao imefika wakati inawapa shida. Matamanio ya mwili yameshindwa kuwasiliana vizuri na roho. Kuna nyakati tamaa za mwili zinakuwa kubwa na hivyo kwa kufunga na kuomba waweza kuutiisha mwili huu. Kwa vijana hasa, vyakula na vinywaji tunavyokula vinaleta shida wakati mwingine ndani ya mwili. Kwa kufunga unautiisha mwili na kuzinyamazisha tamaa hizo. Wengine wanafunga kwa ajili ya kuyatiisha mawazo. Bwana Yesu akasema mawazo ndiyo yamtiayo mtu unajisi. Kabla mtu hajafanya uasi Fulani huanza kujichafua katika mawazo yake. Ndani ya mawazo yake ataua, atamtukana mtu, atazini, ataiba yani atafanya kila lililo baya kabla hajalifanya katika ulimwengu wa kimwili. Rafiki yangu mmoja akasema ikiwa mwanadamu anaweza kupangilia mipango mbali mbali miovu hadi akaitimiza kwa nn asiweze kufanya hivyo hivyo kwa ajili ya Mungu? Kwa hyo wakati mwingine mtu anafunga kuyatiisha mawazo machafu ndani yake. Mawazo machafu hututia unajisi! Ndo maana mtume Paulo akasema “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu” 2Kor 7:1

• Lakini kiroho tunafunga ili kuweka mahusiano yetu na Mungu vizuri rohoni. Ezra 8:21-23

“Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote. Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani; kwa maana tulikuwa tumesema na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao. Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali”.


AINA YA MIFUNGO:

1. Mfungo kamili
Katika mfungo huu hakuna kula kabisa chakula kigumu bali waweza kunywa maji au kimiminika chochote cha kukusupport.
Siku ngapi waweza kufunga mfungo wa aina hii unategemea na neema na malengo yako katika mfungo huo. Wengine huenda siku moja, mbili, tatu, wiki, n.k n.k

2. Mfungo nusu

Mfungo nusu huanzia saa 12 asbh hadi saa 9 mchana au kuanzia jua linapoibuka hadi linapozama. Mfungo ambao madhehebu mengine wamewazoeza waumini wao kuufanya. Wengine wameweza kuufanya kila ijumaa. Madhehebu ambayo yamewazoesha watu wao kufunga angalau kila wiki mara moja wameweza kuwa na mafanikio makubwa sana katika kuzifungua nira na vifungo mbali mbali​

3. Mfungo wa Daniel
Daniel alifunga mifungo miwili ya aina yake;

• Katika Sura ya I Daniel alifunga alikula mboga mboga tu (Yaweza kuwa alikula mboga mboga na juisi Fulani Fulani)

• Katika sura ya 10 Daniel alifunga kwa siku 21 kwa kutokula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwake”​

Ngoja nikomee hapa kwa leo hadi wakati mwingine na Mungu akubariki sana na kama umependezwa na ujumbe huu hebu share na mwingine ili naye abarikiwe.

Nakushukuru sana wewe ambaye umekuwa ukibarikiwa na neno la Mungu ambalo tumekuwa tukijifunza pamoja kwenye huduma hii na umeona ni vema kuungana nasi kuwafikishia pia wengine injili (hasa walioko vijijini) kwa njia ya vipeperushi. Nawashukuru wote mnaoendelea kujitoa kwa ajili ya hili. Lengo letu ni kutengeneza vipeperushi angalau 5,000 kwa mwezi. Kipeperushi 1 ni tshs 250 tu. Kama unabarikiwa na neno ambalo tumekuwa tukishirikishana naamini utapenda pia watu walioko mazingira yasiyokuwa na Internet wafikiwe na injili hii kwa njia ya vipeperushi.

Ungana nasi kwenye huduma hii kwa kadri ya kufanikiwa kwako na Mungu akubariki. ‘Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema” #2KOR. 9:6-8. Hebu fanya kazi nasi kwa njia hii kwa kupenda. Ukichangia hata vipeperushi 2 (tshs 500 tu) kwa wiki au kwa mwezi waweza kuwafikishia injili watu zaidi ya 10. Utakuwa umeshiriki utume mkuu pamoja nasi. Basi changia kwa kadri ya kufanikiwa kwako.


YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU, KWA MUNGU YOTE YANAWEZEKANA

Kwa maombi | ushauri au unataka kumpokea Yesu akusamehe dhambi na abadilishe maisha yako basi ongea nami kwa tumia namba hii +255 712 204 937 |Kama unataka uwe unapokea mafundisho kila siku kwa Whatsapp +255 758 443 873 usiache kunipa majina yako|Unaweza pia kuwasiliana na mtenda kazi mwenzangu Mwinjilisti Emmanuel Jeremiah kwa simu namba +255 753 123 222 | Tuandikie pia kupitia
info@nenolauzima.org|  


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Kwa furaha kubwa nakukaribisha tujifunze faida za maombi ya kufunga.
Marko 9:23 ‘’ YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.‘’
-Kwanini Mengine yanashindwa kuwezekana? 
Ni kwa sababu hatufungi na hata tukifunga basi tunafunga bila kuomba na hata tukiomba tunaomba kidogo sana.
Baada ya mimi kuokoka nilikaa siku kadhaa bila hata kuwaza kama huwa kuna kufunga. Lakini siku moja kwa neema ya ajabu nikasikia sauti ikisema ‘’ Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha MUNGU.’’  Na baada tu kusikia sauti hiyo nikapata msukumo wa ajabu wa kufunga. Niliazimia kufunga siku 3 hata hivyo sikuzimaliza. Lakini baadae nilizoea na wakati mwingine nilikuwa naweza kufunga siku 3 bila kula chochote na kazi mbalimbali nafanya lakini hawezi kujua mtu yeyote. Maombi ya kufunga ni muhimu sana kwa kila Mkristo. Kuna watumishi hufunga siku hata zaidi ya 7 bila kula chochote wakiomba kwa BWANA.
2  Petro 1:10 ‘’ Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe. ‘’
Kunahitajika juhudi na nguvu ili tusijikwae. juhudi hizo na nguvu hizo wakati mwingine zinahitaji kufunga na kuomba.
 
Luka 2:37 ‘’ Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. ‘’
-Maombi ni maisha kwa mkristo.
-Maombi ni mkono mrefu wa kupokea kutoka kwa MUNGU.
-Kwa sababu maombi ni maisha tambua jambo hili kwamba maombi ya kufunga  ni sehemu ya maombi ambayo maombi hayo ni maisha.
-Mama huyu kweli andiko hapo juu alikuwa na miaka 84 lakini alikuwa akifunga na kumwomba MUNGU. Kumbe kufunga ni muhimu sana kwako, kama watu wa miaka 84 wanafunga unadhani kuna udhuru utatoa wewe mwenye miaka chini ya 40. Kila mtu anatakiwa kuomba na wakati mwingi kuomba maombi ya kufunga.
FAIDA SABA ZA MAOMBI YA KUFUNGA.
        1.     Maombi ya kufunga yanaweza kukufanya uongezeke kiimani.
Mathayo 17:21 ‘’ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]   ‘’
-Kwa sababu kuna mambo ambayo yatawezekana tu baada ya kufunga, naamini imani yako itaongezeka kupitia matokeo ya kufunga kwako.
Mfano. Ulikuwa ukihitaji kupata kazi kwa muda mrefu sana. Uliomba maombi ya kawaida na bado hukufanikiwa kupata kazi, baada ya kuamua kufunga siku 5 ukajikuta unapata kazi na pia ukawa unapigiwa simu kwamba unahitajika katika kazi 3 tofauti. MUNGU amekujibu ombi lako la kupata kazi na nahakika imani yako itaongezeka sana. Ndio maana nasema hivi maombi ya kufunga yanaweza kusababisha imani yako ikue, hiyo ndio sifa ya kufunga na kuomba kisha kupokee kutoka kwa BWANA.
        2.     Macho yako ya ndani yatakuwa yanaona vizuri.
Zaburi 119:18 ‘’ Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. ‘’
-Mambo mengine ya kiroho kuyajua  ni lazima ufumbuliwe macho ndipo utaona na kujua.
-Kuna vitu vingi sana ambavyo sikuwahi kuvijua wala kuviona lakini baada ya maombi ya kufunga niliona na kushangaa sana.
-Biblia inaposema kwamba ''Unifumbue macho yangu nitazame'' maana yake mwanzo hakuweza kutazama  na kuelewa hata kama macho anayo ila macho ya ndani yalikuwa yamezibwa ndio maana hakuona, na katika hilo tunarudi pale pale kwamba ''Mengine yatawezekana tu baada ya kufunga na kuomba''
-Maombi ya kufunga yatafungua macho yako ya ndani na na utaona hata maadui walio sirini ambao wamekutesa kwa muda mrefu. 
.       3.   Mwili wako utakuwa umetiishwa.
Wakolosai 3:5 ‘’ Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;‘’
-Ndugu yangu, kuutiisha mwili wakati mwingine hauhitaji tu kujaribu kuishi maisha matakatifu bali ni kuishi maisha matakatifu huku ukiomba na maombi ya kufunga ndio yaliyo na nguvu zaidi za kukusaidia katika hilo.
-Unapofunga na kuomba hata kama hukuombea kutiisha mwili wako lakini lazima tu mwili wako utiishwe kutokana na maombi uliyoomba hata kama hukuombea jambo hilo. 
-Maombi ya kufunga ni tiba kuu ya vitu vinavokutesa ambavyo viko katika mwili wako.
-Kama unateswa na mwili wako kwa kuwaka tamaa ya ngono, basi funga na kuomba na mwili wako uttiishwa.
-Kama mawazo mabaya yanakutesa basi funga na kuomba yataondoka.
-Kitu chochote ambacho kinakuendesha bila hata wewe binafsi kutaka, lakini unajikuta tu ukikitii kitu hicho ambacho ni machukizo, basi funga na kuomba utashinda.

 1 Thesalonike 5:17  ''ombeni bila kukoma;''
-Njia mojawapo ya kuutiisha mwili wako hata usinaswe na dhambi wala tamaa mbaya ni kwa njia ya kufunga.
-Kama umekuwa unateswa na mawazo machafu yanayokunajisi basi ukifunga na ukaomba kweli katika kufunga kwako hakika mawazo hayo machafu yataondoka.
-Kufunga ni muhimu sana kwa wewe ambaye dhambi za zamani zinataka kukuteka tena. Funga na omba hakika utabaki mshindi daima.
 Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''
     4.   Kupokea maana ni ahadi ya MUNGU kujibu maombi yako.
Yeremia  29:13 ‘’Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.''  Tena Biblia inasema  ''Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;-Mathayo 7:7''   na kwa sababu MUNGU analiangalia neno lake alitimize basi hata aliposema tuombe ni hakika atajibu maana yeye hajipingi na Neno lake, labda tu sisi tuombe vibaya na tupungukiwe na imani katika maombi yetu.

1 Yohana 5:14-15 ''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.'' 

-Maombi ya kufunga ni mkono mrefu wa kupokea kutoka kwa MUNGU.
 Waebrania 4:16 ''Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. ''
      5.  Utamruhusu ROHO MTAKATIFU kukutumia.
1 Kor 12:11 ‘’ lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ‘’
-ROHO MTAKATIFU humgawia kila mtu huduma kama atakavyo yeye ROHO lakini wakati mwingine huduma unayo lakini haiendelei kwa sababu huombi ndio maana BWANA YESU akasema '' Mengine yatawezekana kwa wewe kufunga na kuomba''
 -Maombi ya kufunga ni muhimu sana na inakuwa rahisi zaidi ROHO MTAKATIFU kukutumia maana hata wewe unakuwa rohoni.
-ROHO pia anaweza kukutumia kwa maombi.
 
Warumi 8:26-27 ''Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya ROHO ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU''.
      6.   Utatumika kwa MUNGU vizuri
Matendo 13:2-3 ‘’Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.’’
-Maombi ya kufunga yalifungulia njia ya watumishi hawa kuitwa na kupewa jukumu na MUNGU.
-Hata wewe unaweza kuwa katika kufunga na MUNGU akasema na wewe jambo fulani ambalo unatakiwa ulitende, unaweza kujiuliza kwanini ROHO hakusema wakati hawakufunga na kuomba?
Maombi ya kufunga ni muhimu sana.
 
     7.    Utakuwa na nguvu za MUNGU.
Mathayo 11:12 ‘’Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.‘’
-Ndugu, watu wenye nguvu tu ndio wanaouteka ufalme wa MUNGU. nguvu zinazozungumzwa hapa sio nguvu za miili ila ni nguvu za rohoni ambazo hupatikana kwa kujifunza neno la kulijua, kuishi maisha matakatifu, kumtumikia BWANA YESU na kuomba sana. na maombi ya kufunga ndio maombi ambayo yatakufanya uwe na nguvu zaidi za rohoni hata shetani asikurudishe nyuma.
 
''Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, BWANA asingesikia. Hakika MUNGU amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu-Zaburi 66:18-19''

-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu


KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.

''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.''

Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula


source: https://maishaushindi.blogspot.com