AINA TATU ZA MAJARIBU AMBAYO MTU ANAWEZA AKAPITIA
| Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU. | 
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Nakuomba soma somo lote maana ni ufunuo kwako ili usaidike.
Majaribu ni mambo yanayompata mtu ambayo hakuyataka.
Mambo hayo yana maana nyingi kulingana na chanzo chake.
Kama chanzo chake ni shetani basi unatakiwa ujue jinsi ya kuyashinda.
Kama ni jaribu la MUNGU basi hilo lina faida kwako.
Yakobo 1:12 ''  Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, BWANA aliyowaahidia wampendao.'' 
 Katika
 maisha yako kama Mteule wa MUNGU uliyeokolewa na Bwana YESU wakati 
mwingine unaweza kujikuta majaribuni lakini chunguza sana chanzo cha 
majaribu yako hayo maana majaribu mengi ni kazi za shetani ili umwache 
YESU na ukose uzima wa milele.
Mama
 mmoja alikuwa kiongozi kanisani na alimtumikia MUNGU kwa uaminifu sana 
kwa miaka mingi sana lakini baadae akakwazwa kidogo sana na kuacha 
kwenda kanisani. Kwa kokosa kwake Neno la MUNGU aliona kawaida tu na 
baadae hofu ya MUNGU ikaondoka ndani yake na kujikuta anaenda kwa mganga
 wa kienyeji. Alipooenda tu kwa mganga wa kienyeji akafia huko huko kwa 
mganga. Kanisa lililia sana maana hakumaliza vizuri maana alijitenga na 
Bwana YESU kisha akajiunga kwa shetani kwenye hirizi, ni hatari mno.
Ndugu unahitaji kuvumilia sana huku ukiendelea na wokovu na utakatifu.
Ngoja sasa tuangalie aina tatu za majaribu.
Natambua
 kabisa aina za majaribu sio hizi tu tatu bali ni zaidi. Na mimi pia 
nilishawahi kufundisha aina nne za majaribu lakini leo nahusika na aina 
hizi tatu za majaribu katika ufunuo wa leo ambao watu watasaidika na 
kuimalika kiroho. 
 Aina 3 za majaribu.
1. Majaribu ya kujisababishia mwenyewe.
Maana mojawapo ya neno ''Majaribu'' ni fikra zinazomshawishi mtu kutenda jambo ambalo ni machukizo kwa MUNGU. Maana nyingine Ya Neno jaribu ni ushawishi wa kipepo unaomfanya mwanadamu kutenda jambo baya au au ovu.
 Marko 14:38 '' Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.'' 
Bwana YESU alituonyesha njia mojawapo ya kutuzuia kuingia katika majaribu ni maombi ya kina na ya kudumu.
Mtu anaingiaje kwenye jaribu la kujisababishia?
-Kwa sababu ya tamaa mbaya mfano tamaa ya utajiri hivyo unajikuta kwenye jaribu ambalo kutoka inakuwa tatizo.
  1 Timotheo 6:9-10 ''  Lakini hao watakao kuwa na mali 
huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, 
zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.
Maana shina moja la mabaya 
ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo 
wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.
 ''
-Kwa sababu ya kutokumtii ROHO MTAKATIFU unajikuta kwenye jaribu.
- Kwa sababu ya dhambi uifanyayo kwa siri unajikuta unaingia kwenye jaribu zito na hakuna msaada wa MUNGU hadi utubu.
 Yakobo 1:14-16 '' Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.
Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.
Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.
 ''
-Kwa sababu ya kutokujitambua kama mteule wa KRISTO  na kutambua haki zako kwa MUNGU.
Unakuta binti anafanya uzinzi na kubeba mimba na masomo yanafutikia hapo, hilo ni jaribu la kujisababishia. 
-Kwa sababu ya kumwacha YESU na Wokovu.
-Kwa sababu ya kutokulitii Neno la MUNGU.
-Kwa sababu ya kutowasikiliza watumishi wa MUNGU.
 Mithali 12:15 ''  Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.''
Dawa ya majaribu haya ni kutubu toba ya kweli na kuanza kuishi maisha matakatifu huku ukijifunza sana Neno la MUNGU.
 ''Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na MUNGU; maana MUNGU hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.-Yakobo 1:13
 '' 
Unaweza kuyaepuka majaribu haya ya kujisababishia kwa;
A. Kutubu na kuacha dhambi.
B. Kulitii Neno la MUNGU na kulitumia kwa haki.
C. Kufanya maombi.
D. kulijaza Neno la MUNGU ndani yako.
E. Kuutumia muda wako mwingi kwa MUNGU na sio katika mambo yako.
2. Majaribu ya hila za shetani na mawakala zake.
Waebrania 10:32-33  ''Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu;
pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo.''
Baada
 ya kuokoka wakati mwingine kunaweza kukatokea majaribu kwa sababu ya 
nguvu za giza ambazo zinatambua kabisa kwamba wewe sasa umewakimbia kwa 
kuchagua kwenda uzima wa milele. Unahitaji tu kukaa vizuri na MUNGU 
maana MUNGU hatakuacha ujaribu zaidi.
 1kor 10 :13 ''Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila 
MUNGU ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini 
pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze 
kustahimili. ''
-Majaribu haya hutoka kwa watu wanaotumika kipepo dhidi yako.
-Hutoka
 kwa mawakala wa shetani ambao wanataka kukuangusha uli usihusike tena 
na Kanisa la MUNGU na usihusike na uzima wa milele.
 Luka 17:1-4 ''....  Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!
Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe.
Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.
 '' 
Majaribu haya ukiwa muombaji utayashinda kila leo.
-Anaweza
 mtu akakuendea kwa waganga, anaweza mtu akakusemea vibaya kwa wakubwa 
wako kazini n.k lakini ukiwa muombaji utashinda kirahisi mno mno.
 1wathesalonike 3:5 ‘’Kwa  hiyo 
mimi  nami  nilipo 
siwezi kuvumilia   tena  nalituma 
ili  niijue  imani 
yenu  asije  Yule 
mjaribu  akawajaribu  na 
tabu  yenu  ikawa haina 
faida ''      
Hakikisha tu unakuwa silaha kali ya kuangamiza kila kitu cha shetani kila siku na mawakala zake.
MUNGU atakushindia.
Ukiwa muombaji wanaotumika kipepo dhidi yako wanaweza hata kufa kwa sababu ya mapigo ya MUNGU kutokana na maombi yako.
Kwa
 majaribu haya unahitaji kupambana sana kimaombi na MUNGU atawaabisha 
maadui hayo na kuwaangamiza kabisa kama wakishupaza shingo. 
3. Jaribu kama kipimo cha MUNGU.
Zaburi 11:5 '’BWANA  humjaribu 
mweyehaki  Bali nafsi  yake 
humchukia  asiye  haki  
na  mwenye udhalimu’’ 
Jaribu la MUNGU ni kipimo tu cha MUNGU kama kweli unampenda.
Jaribu la MUNGU kwanza ni muhimu kujua kwamba linampata mtu ambaye yuko vizuri kiroho na amejaa ROHO MTAKATIFU.
Wewe mchanga sana kiroho na wewe mtenda dhambi maarufu wala usiwaze kwamba unajaribiwa na MUNGU.
Jaribu la MUNGU haliko katika mambo ya dhambi hata siku moja.
Jaribu la MUNGU lina faida kubwa sana kwa anayejaribiwa, ni mtaji mkubwa sana wa imani.
 Waebrania 13:1-2 ''Upendano wa ndugu na udumu.
Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.
 ''
Kuna watu majaribu yao yalikuwa kuwahudumiwa malaika wa  MUNGU walikuja na baraka zao.
Kitendo cha kuwakataa basi na baraka hupati.
Mfano wa Malaika pia unaweza kuwa wateule wa MUNGU na hao kitendo cha kuwafanyia Mema tu basi unabarikiwa.
 Jaribu la MUNGU linafunua moyo wako ili ijulikane kama kweli unampenda MUNGU kwa uharisia au kwa maneno tu.
Ngoja
 nikupe ushuhuda mmoja wa Askofu ambaye yuko kigoma akiwa na huduma 
kubwa sana sasa. Yule Askofu zamani akiwa kijana aliyeokoka  
anayemtumikia MUNGU kwa uaminifu alisikia sauti ya ROHO  wa MUNGU 
ibadani ikimwambia kwamba atoe sadaka viatu vipya alivyokuwa amevaa kwa 
mara ya kwanza siku hiyo ibadanai. Yule ndugu kwa sababu alikuwa anakaa 
karibu na kanisa alitoka ibadani na kwenda kuchukua viatu vingine 
alivyokuwa navyo nyumbani na kuleta Kanisani na kumpa mchungaji akisema 
kwamba Roho wa MUNGU amemwambia kutoa sadaka viatu. Ni wakati ibada 
inaendelea. Watu walishangaa sana lakini baadae kidogo tena yule ndugu 
sauti ikarudia ikisema kwamba atoe sadaka  maana hajatoa. Yule ndugu 
akatoka tena na kwenda nyumbani kuchukua pea nyingine ya viatu iliyokuwa
 imebaki na kuleta ibadani. Baadae akasikia sauti tena ikimwambia kwamba
 aliambiwa atoe viatu alivyokuwa amevaa na sio vya nyumbani. Akaambiwa 
kwamba aliambiwa atoe viatu vipya na sio vikuukuu. Yule ndugu akaanza 
kulia kwa sauti ibadani huku akivua viatu vile alivyoambiwa na kutoa 
madhabahuni huku akilia. Mchungaji hakusema Neno lakini kanisa zima 
walishangaa sana maana ibada ilikuwa inaendelea. Baadae ndipo akaeleza 
ukweli mbele ya Kanisa juu ya yaliyotokea.
Baada
 ya tukio hilo yule ndugu alibarikiwa kiajabu sana na hadi sasa ana 
huduma kubwa sana sana na ameinuliwa sana kihuduma na kimaisha.
Sio
 kwamba MUNGU alihitaji viatu bali MUNGU alijua kabisa kwamba moyo wa 
yule ndugu ulikuwa kwenye viatu vile vipya na hivyo akamjaribu huko huko
 ambako moyo wake uko. Yule ndugu alijikuta ametoa pea tatu za viatu 
badala ya moja tu iliyokuwa inahitajika lakini alipotii alibarikiwa 
sana.
Kumbuka Ibrahimu alijaribiwa na MUNGU kwa kuambiwa atoe sadaka ambayo ni mtoto wake wa pekee na aliyempata uzeeni.
 Mwanzo
22:1-2 ''Ikawa baada ya mambo hayo MUNGU alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 
Akasema, Umchukue mwanao, mwana
 wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, 
ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo 
nitakaokuambia.''
Jaribu la MUNGU huwa la kipekee sana na lina faida kuu kwa mtoaji baadae.
Unaweza ukapigia magumu kumbe ni jaribu la MUNGU kwako ili uimalike zaidi kiroho.
Unaweza
 ukawa kila ukiomba juu ya jambo fulani unaona kwenye ndoto kwamba 
utalipata. Lakini unapita muda kumbe unahitaji uvumilivu na tengeneza 
kwenye mambo mengine ndipo litakuja jambo hilo la baraka kwako.
Unaweza
 ukapatwa na majanga na matatizo makubwa na ukapata mtikisiko mkubwa 
sana kiuchumi na kimaisha lakini kumng'ang'a kwako YESU na utakatifu 
ukivuka hapo unapandishwa viwango.
Unaweza
 ukakosa uzao hata miaka mitano lakini hiyo haina maana kwamba MUNGU 
hatakupa, ukivumilia utapata uzao ulio bora na utabarikiwa.
 Mathayo 24:13 ''  Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.'' 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
 
Post A Comment:
0 comments: