Articles by "SHUHUDA"
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo SHUHUDA. Onyesha machapisho yote


Billy Graham enzi za uhai wake.
Muinjilisti wa kimataifa kutoka nchini Marekani, Billy Graham  amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 99 nyumbani kwake, North Carolina.
Akitoa taarifa ya kuondoka kwa Baba yake, Mtoto wa Marehemu Billy Graham aitwaye Franklin Graham alisema hivi;
''
My father Billy Graham was once asked, “Where is Heaven?” He replied, “Heaven is where Jesus is and I am going to Him soon!” This morning, at the age of 99, he departed this world into eternal life in Heaven, prepared by the Lord Jesus Christ—the Savior of the world—whom he proclaimed for nearly 80 years. He will be missed by our family, his colleagues, faithful ministry partners, and, yes, many around the world. But what joy he has to be welcomed by God the Father, and be reunited with my mother in the presence of Jesus who speaks peace to eternal souls.
What about you? When you depart this world do you know with certainty where you will spend eternity? You can know this today. Jesus said, “For God so loved the world, that He gave His only begotten Son, that whosoever believeth in Him should not perish, but have everlasting life” (John 3:16). The One who comforts weary souls has given us this promise, “Let not your heart be troubled; you believe in God, believe also in Me … I go to prepare a place for you … I will come again and receive you to Myself; that where I am, there you may be also” (John 14:1-3).
'' 
Mwinjilisti huyo mtoto wa mkulima amefariki majira ya saa mbili asubuhi, sawa na majira ya saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki, nyumbani kwake, Montreat – Jumatano tarehe 21 Februari 2018.
Takwimu za huduma yake, zinaeleza kwamba Billy Graham ndiye Mhubiri pekee aliyewahi kuhubiria watu wengi zaidi tangu historia kuumbwa, akiwa amefikia zaidi ya watu milioni 210 kwenye nchi 185 duniani, aidha kwa njia ya runinga ama ana kwa ana.
 
Billy Graham akiwa na mkewe Ruth(aliyekaa na mtoto wao wa mwisho aitwaye Ned).  Juu kutoka kulia waliosimama ni ni watoto wao wengine ambao ni  Franklin, Anne, Gigi na  Ruth Bell . Picha hii ilipigwa mwaka 1962.


Graham, raia wa Marekani, alieanzia kuhubiri jijini London Uingereza mnamo mwaka 1954, alikusanya maelfu ya watu kila mahali alipofanya mikutano ya hadhara ya injili.
Afrika Mashariki, Graham aliwahi kuhubiri Tanzania, miaka 55 iliyopita, wakati nchi iliitwa Tanganyika, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Afrika miaka ya 1960. Takriban "watu 40,000 walihudhuria mkutano huo wa siku moja, tarehe Feb 28. 1960", kwa mujibu wa mtandao wa shirika lake.
Kwa zaidi ya miaka 60 inakadiriwa kuwa amehubiri kwa jumla ya watu milioni 210.
Alikuwa Mkristo akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kumsikiliza mhubiri mmoja na kuanza huduma ya mahubiri mwaka 1939.

Graham alifahamika sana duniani kutokana na Uinjilisti alioufanya na mahubiri aliyotoa katika nchi mbalimbali duniani kuanzia miaka ya 1950.
Alianza huduma ya kuhubiri baada ya kutawazwa akiwa na miaka 21, mwaka 1939.
Familia yake imesema alifariki dunia akiwa nyumbani kwake katika jimbo la Carolina Kaskazini.
Graham anaelezwa kuhubiri kwa zaidi ya miaka 60, na kubadilisha mitizamo ya Mamia ya Mamilioni ya watu waliokubali ujumbe wake.
Mbali na mahubiri akiwa katika viwanja mbalimbali vya michezo na ukumbi, alitumia pia runinga na redio kuhubiri.
Amesuifiwa kama Mhubiri mwenye ushawishi mkubwa katika karne ya 20.
Wakati wote wa uhai wake, alikuwa na urafiki wa karibu na marais wote wa Marekani tangu  rais Truman hadi Barrack Obama.
Rais Donald Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, Graham alikuwa mtu wa kipekee na Wakiristo na watu wa dini nyingine, watamkosa sana.
 
Billy Graham ambaye ndiye mtoto mkubwa kuzaliwa akiwa na Baba yake mzazi na mama yake mzazi pamoja na ndugu zake wa damu katika Picha ya pamoja  mwaka  1962

Mnamo mwaka 1950, aliunda Umoja wa Wahubiri wa Billy Graham katika juhudi za kusambaza neno la MUNGU kupitia kile kilichokuja kuwa maarufu hivi leo kama “crusades”, mahubiri ya mfululizo ambayo hufanyika katika viwanja mbalimbali.
Graham aliendesha mahubiri haya katika mabara yote isipokuwa Antarctica, akihubiri yeye mwenyewe kupitia matangazo ya satellite. Alihubiri katika mataifa ya Soviet kabla ya kuanguka kwa ukomunisti.
Na katika msimu wa baridi mwaka 1994, Billy Graham alitoa mahubiri huko China na Korea Kaskazini, ambako alikutana na viongozi wa kisiasa na kidini katika nchi hizo.
Kutokana na safari zake alizofanya katika mataifa mbali mbali ulimwenguni, mhubiri huyu mashuhuri wa Marekani alithibitisha  kuwa Ukristo sio tu dini ya nchi za Magharibi.
alisema katika moja ya mahubiri yake kwamba  
“Ukristo ni wenye nguvu Afrika na Amerika ya kati na Asia kuliko ilivyo nchi za Ulaya, kwa hatua kubwa. Huko Ulaya , bado unaitwa Ukristo, lakini hauna ukakamavu na nguvu kubwa. Na nilikuwa Rome na kufanya mazungumzo na Papa juu ya suala hili na nafikiri mtakubaliana na hilo – kwamba maisha halisi ya Ukristo hivi sasa yako kule tunakokuita ulimwengu wa tatu,” alisema .
Graham, ambaye kabla hajaanza kazi ya MUNGU alifanya kazi kama afisa wa mauzo, aliendelea na kuwa mmoja wa wahubiri wenye ushawishi mkubwa miongoni mwa watu wa dini zote huku akiwashauri marais na viongozi wengine wengi duniani juu ya imani ya Kikristo.
Mwaka 1949, alipata umaarufu wakati alihubiri kwa wiki nane kwenye hema kubwa huko Los Angeles.
Wakati wa harakati za mashirika ya kupigania haki za binadamu, Graham aliibuka kuwa mkasoaji mkubwa wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Mara kadhaa muinjilisti huyo aliyemrithisha huduma mwanaye aitwaye Franklin Graham, amekuwa akinukuliwa akisema, “Nyumbani kwangu ni mbinguni, hapa nilipo ni mpita njia tu.”

Ni muhubiri aliyeepuka kashfa mbalimbali zilizowazonga wahubiri wengi waliotumia runinga kusambaza injili.
Mkutano wake wa mwisho wa hadhara ulikuwa mwaka 2005 jijini New York Marekani akiwa na umri wa miaka 86.
Rais Donald Trump amemuelezea Graham kama "mwanaume wa kipekee".
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Trump amesema "Mhubiri maarufu wa Injili Billy Graham. Hakuna aliyekuwa kama yeye! Atakumbukwa na Wakristo na watu wa dini zote. Mwanamume wa kipekee kabisa."
Shujaa amemaliza kazi yake duniani, na sasa ni uzima wa milele katika KRISTO YESU.
MUNGU alimtoa na sasa amemtwaa hivyo daima jina la BWANA lihimidiwe.
 
Billy Graham na mkewe  Ruth Graham  katika mkutano wa injili  New York for mwaka 1957.

Siku za karibuni nitakuletea mambo kadhaa usiyoyajua kutoka katika kazi ya MUNGU aliyoifanya shujaa  huyu hata upate kitu chema cha kujifunza.
Ubarikiwe.

Askofu Emmanuel Lazaro, Askofu mkuu wa kwanza wa Kanisa la T A  G
BWANA YESU ALINITOKEA

Nilizaliwa katika kijiji cha Modio, wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro Tanzania. Nilisoma elimu ya msingi katika shule ya msama, na baadaye nilienda Mombasa kwa mafunzo ya miaka miwili. Baba yangu anaitwa kunandumi na mama yangu anaitwa Firayandiani . Wazazi wangu walipenda sana mambo ya dini inagawaje wakati huo neno la wokovu lilikuwa halijahubiriwa kwa hiyo hawakujua wokovu.
Katika siku za utoto wangu, neno la uponyaji kwa jina la Yesu halikuhubiriwa kabisa, wala hatukusikia kuwa Yesu anaweza kumponya mtu mgonjwa kwa jina lake. Nilipokuwa na umri kama wa miaka saba niliugua, hali yangu ilizidi kuwa mbaya ikabidi nilazwe kwenye zahanati ya kanisa la Kilutheri Masama. Hata hivyo hali yangu iliendelea kuwa mbaya na Daktari akataka nirudishwe nyumbani. Mwili wangu ulidhoofika sana, na kutoa harufu mbaya. Chumba nilimokuwa nikilala kilinuka harufu hiyo, na kwa ajili ya udhaifu pia sikuweza kula kabisa.
Nilipokuwa nikiongea , niliisikia sauti yangu nyuma ya kichwa changu. Siku moja asubui, kama saa nne niliskia baridi sana mwilini mwangu: nikamwomba mama anitoe nje ili nipate joto la jua. nikiwa nje mama aliniangalia kaanza kulia nilipomwona mama analia nilimuuliza "Unalia nini?" Akaniambia "Nalia kwa sababu nimefanya kila niwezalo ili upone lakini huponi" kwa ghafla nikatokewa na maneno haya yafuatayo "SITAKUFA YESU NI UWEZA" nikamwambia mama.
Wakati maneno hayo yalipokuwa yakinitoka, yalibadilika kuwa moyo ndani ya kinywa changu, ikawa kama kunga donge la moto kinywani. Nikiwa nashangaa yanayonitokea ule moto ulishuka tumboni nikaanza kusikia joto kali katika mwili wote. Nilitokwa na jasho mwili wote na hapo hapo nikajikuta mimi ni mzima kabisa. Nikiwa sielewi ni nini kimetokea nilijiskia hamu ya kula, nikamwomba mama anipe chakula. mama hakuamini kuwa naweza kula, akaniuliza , "wewe waweza kula?" Nikamjibu "ndiyo". Akanitengenezea chakula nikala na tangu wakati ule sikuwa mgonjwa tena "JINA LA BWANA LITUKUZWE"
Ingawa jambo hilo lilitokea mbele ya mama yangu sikuweza kumweleza ile hali iliyonitokea , bali ilinikaa moyoni mwangu bila kumweleza ile hali iliyonitokea , bali ilinikaa moyoni mwangu bila kumweleza mtu , Tangu zamani Mungu amekuwa akidhihirisha mambo yake yajayo na ndiyo awafunguaye vinywa wanadamu kwa wakati ulioamriwa ili wayanene. wakati nilipokuwa kwenye masomo yangu huko Mombasa niliugua tena. Hali yangu ikawa mbaya sana hata nikashindwa kula , Nilibebwa nikapelekwa katika hospitali ya madaraka Mombasa, na mjomba wagu Wilson Kimaro.
Nilipofika hospitalini nilikaa nikimngojea Daktari aje, Wakati nipo nje ya hospitali Mwili wangu ulionyesha hali ambayo nilihisi kama ninakufa. Mawazo yangu yakafikwa na hali ya kumwomba Mungu ingawaje sikuwa mtu mwenye hali ya kuomba wala sikuwamtu wa kutaka mambo ya Mungu kwa wakati huo. Ninakumbuka wakati huo, hofu ya kifo ilinitisha ndipo nilimwambia Mungu maneno haya "KAMA UKINIPONYA NITAKUTUMIKIA" sielewi nilipata wapi fikra hizo. Mara baada ya kusema hivyo , nilizimia nilipochukuliwa kupelewa ndani ya hospitali kulazwa sikuwa na fahamu kabisa. Kufuatana na taarifa nilizozipata baada ya fahamu zangu kunirudia daktari alisema hakuna uwezekano wa matibabu, kwa kuwa nisingeweza kupona.
Nilizimia tena kwa siku tatu na daktari alikuwa anaangalia mapigo ya moyo tu. Hii ikiwa na maana alikuwa akipima kuona kama nipo hai au nimekwisha kufa. Wakati wote nilipikuwa nimezimia, niliona malaika wa Bwana akija na kunipakata , akinionyesha maua mazuri ya ajabu. Malaika huyo alikuwa akinitokea hasa wakati ambao natokewa na hali ya kutoweka kabisa (Yaani kufa). Aliendelea kunitokea hivyo mpaka niporudiwa na fahamu zangu nikajikuta nimepona.
Niliwauliza wale wangonjwa waliolazwa chumba kile pamoja nami "Yuko wapi yule mtu anayeniletea maua?" wote walishangaa kuskia nimerudiwa na fahamu zangu, wakanieleza kuwa daktari alikuwa anaongea saa yangu ya kukata roho, na kwamba sikupewa dawa yoyote wala sindano tangu nilipolazwa hapo. Wala hakuna mtu yeyote aliyekuja kuniletea maua. "MUNGU NA ATUKUZWE KWA REHEMA ZAKE KWA WANADAMU"
Hata hivyo baada ya kupona sikuwa na mawazo tena kwamba nilimwahidi Mungu kuwa kama angeniponya ningemtumikia . Niliendelea kuwa mwovu kama kawaida.

NATOKEWA NA SHETANI NA KUOKOLEWA NA YESU
Katika siku za ujana wangu, mimi sikuamini shetani ni kitu cha kweli, wala katika kanisa langu hakukuwepo na fundisho lolote kuhusu shetani , na pia, tulipokuwa shuleni hatukupata elimu yoyote au tamko lolote lisemalo kuwa shetani yupo. Katika kijiji nilichozaliwa kulikuwa na dini mbili tu, Dini ya kiislamu na dini ya Kikristo (Dhehebu la Kilutheri). Mimi nilikuwa mkristo ingawa sikupenda mambo ya dini sana kama wazazi wangu walivyopenda. Tena nilipuuzia sana elimu juu ya mashetani. Waislamu katika Kijiji chetu waliamini sana nguvu za mashetani na uchawi lakini mimi sikuyasadiki hayo kabisa wala sikuyaogopa.
Ilikuwa siku moja saa nne usiku, nikiwa kitandani nikivuta sigara, kwa ghafla alitokea mtu mfano wa mwarabu, akiwa na taa kubwa iliyowaka chumbani kote. Macho yake yalikuwa kama nyoka, aliponiangalia niliona hali ya uadui machoni pake. Hungehitaji kufahamu kama ni mtu mbaya au mwema, kwani macho yake yalidhihirisha wazi kuwa ni adui, tena muuaji. Alisimama na taa yake kunikabili. Nilianza kujiokoa naye kwa kutupa mikono na miguu ili asinisogelee. Mara baada ya jitihada zote hizo ambazo hazikumuogopesha, niliona ametokea mtu mwingine upande wangu, na yule mtu aliyeshika taa alipomwona yule mtu aliyekuwa nami aliogopa kama vile mbwa aliyekemewa na bwana wake, Aligeuka akakimbia na kutoweka kabisa. Yule mtu alikuwa upande wangu alipoona yule adui amekimbia, naye aliondoka na kutoweka. Mambo hayo sikuyaona kwenye ndoto bali niliyaona kwa macho yangu kwani sikuwa nimelala. Pamoja na mambo hayo yote mimi sikumfahamu Kristo kama Bwana na mwokozi wangu na sikuwahi kusikia mtu akihubiri neno la Wokovu.
NAUGUA TENA.
Wakati niliokuwa na umri wa miaka ishirini na mbili, nilishikwa na hali ya mfadhaiko wa kufa, Niliwaona madaktari lakini hawakuona kama kuna ugonjwa wowote ndani yangu , ila walinambia niache mawazo. Hali ile ilizidi ndani yangu ikanifanya niwe mlevi sana, Niliamua kulewa ili kujisahaulisha hali iliyokuwa ndani yangu, lakini hata hivyo hali hiyo haikunitoka.
Baada ya kuona sipati msaada kwa hayo yote, ndipo nilimwomba baba yangu aniazime Biblia. Nilijaribu kusoma Biblia lakini sikupata msaada wowote, mwisho nilisema kama Mungu yupo basi nitaweka kichwa changu juu ya Biblia kila nilalapo na kama Biblia ni neno lake basi atanisaidia. Nililalia biblia kwa muda wa miezi mitatu. Kila siku jioni, kabla sijapanda kitandani nilale nilimwomba Mungu aniruhusu niweke kichwa changu juu ya Biblia nikasema "Ee Mungu nisamehe kama kuna kitu nimekosea au kama nimenunua pombe au sikumlipa muuzaji pesa zake naahidi nitamrudishia kesho, lakini niruhusu tu niweke kichwa changu juu ya Biblia."
Siku moja nilipokuwa kitandani ili nilale kama kawaida nikaweka kichwa changu juu ya Biblia mara chumba changu kikatokewa na nuru kali sana iliyong'aa kuliko uwezo wa jua, ndani ya nuru ile akatokea mtu akasema nami na kuniambia amekuja kunijulisha kuwa nitakufa!. Nikamwuliza, "Kwa nini nife?" Akaniambia ni kwa sababu mimi ni mwenye dhambi. Nikamwambia mimi si mwenye dhambi kwa sababu nilibatizwa tangu nikiwa mtoto mdogo. Akanijibu kwamba ningelikuwa nimebatizwa nisingelikuwa natenda mambo mabaya. Nikamwuliza "mambo gani?" Ndipo aliponyoosha mikono yake akanionyesha matendo yangu yote mabaya niliyokuwa nimeyatenda tangu utoto wangu.
Akanambia "Je , Matendo haya ni yako?" Nikamwambia "Ndiyo" Kila tendo alilonionyesha lilikuwa kweli na nililikumbuka nilivyotenda. Nikamwambia, "Ninakubali mimi ni mwenye dhambi." kwa ajili ya matendo hayo utakufa, lakini nimetumwa nikujulishe kuwa kama utampokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wako utaokoka nawe hutakufa" Ndipo nikamwambia ninakubali kumpokea Yesu, naye akanimbia nipige magoti ili aniongoze sala ya toba. Nikapiga magoti akaniongoza salam ya toba, na ya kumkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yangu. Pale pale litatokea ziwa la maji na akaniambia njoo nikubatize, akanichukua na kunizamisha ndany ya maji, Akanibatiza kwa jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu. Mimi kabla ya hapo sikuwa nimeona au kusikia kuwa kuna ubatizo wa kuzamishwa ndan ya maji mengi.
Asubuhi baba yangu aliniuliza "Ulikuwa unaongea nini usiku mwenyewe?" Ndipo nilipomweleza yote yalionitokea na jinsi nilivyobatizwa ndani ya ziwa la maji. Kumbe nilipokuwa nasema na yule mtu nilikuwa nikisikika hata kwenye chumba ndani ya ziwa la maji alinionya na kuniambia nipunguze ulevi. Hata baada ya kutubu kwenye yale maono sikupona ule ugonjwa nilokuwa nao mara baada ya yale maono niliondoka kwenda mjini arusha. Wakati nikiwa Arusha nilielezwa juu ya kikundi kidogo kilichouwa kinaimba na kuhubiri Injili . Mimi na wenzangu tuliamua kwenda hapo ili tukaangalie. Jambo lililotufanya twende ni kule kusikia kuwa kuna mama wa Kizungu ambaye alikuwa akiimba nyimbo za Mungu kwa kutumia gitaa . Siku zile gitaa ilitambulikana kama chombo cha shetani kabisa. kwa hiyo tulienda ili kuona dini ya kishetani inavyoimba. Tukaingia ndani mara yule mama akaanza kuimba na wimbo aliouimba maneno yake ni kama ifuatavyo. "Usisumbuke kwa safari, Mungu akulinda utegemee pendo lake , Mungu akulinda..."
Kabla mama yule hajamaliza kuimba, Nilishukiwa na nguvu zilizoingia moyoni na kuondoa ile hali ya siku zote ya kufa nikawa mzima kabisa. Kwa sababu zile nguvu zilisisimua mwili wangu wote, nilijikuta natokwa jasho jingi sana. Wenzangu niliofuatana nao walipigwa na mshangao wakajaribu kunituliza lakini sikuweza kusema nao , baada ya zile nguvu kutulia nikaamua kumwona huyo Mmisionari na mke wake ili niwaulize ni kitu gani kilichonitokea na imekuwaje mtu aimbe kisha nipone. Ndipo waliponihubiria habari za Yesu na uweza wake wa kuokoka na kuponya , Na kwa kuwa alikuwa akinisomea Biblia nikadhani Biblia ile siyo kama ya kanisa letu huenda ni nyingine .
Ndipo nilipoamua kurudi nyumbani nikachukua biblia ya baba yangu kwa kuwa mimi sikuwa na biblia yangu. Nilipoona Biblia ya yule mmisionari na ileile ya baba yangu ni sawa neno kwa neno, na mstari kwa mstari nilishangaa na kujiuliza, "Mbona maneno ya wokovu na uponyaji hayahubiriwi kanisani kwetu?" Nilirudi tena Arusha kukutana na Yule Mmishionary, Ndipo nilipokubali kumpokea Yesu. Naye akaniongoza sala ya kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wangu. Nilibatizwa ndani ya ziwa la aina ile ile niliyoona kwenye yale maono. Niliamua kufata kila neno la Biblia lilivyokuwa linaeleza kuhusu wokovu. Kisha wakanifundisha juu ya ubatizo wa Roho Mtakaifu : Nikawa na hamu kubwa ya kupokea Roho Mtakatifu . Nilikesha kwa muda mrefu nikimsihi Mungu anibatize kwa Roho Mtakatifu. 
SHETANI ATAFUTA KUNIANGAMIZA TENA
Nikiwa natafuta ubatizo wa Roho Mtakatifu alinitokea mwanamke ambaye alikuwa amepanga chumba kilichokuwa karibu na chumba changu. Alinipenda sana akataka nizini naye, lakini upendo wa Kristo ulikuwa mkuu ndani yangu kiasi ambacho kishawishi chake hakikunitia shida yeyote bali niliendelea kumshuhudia neno la Mungu. Bila mimi kujua makusudi yake, alinitengenezea dawa, akaweka kwenye kahawa akanipa . Nilikunywa ile kahawa na baada ya kunywa nilianza kusikia kifua changu kikiwa kizito.
Baadaye kikatokea kitu kifuani kama ndege na mtu akitoa sauti mbele yangu au akinisalimu kile kitu kilizunguka kifuani na kutoa miiba ambayo iliniumiza kwa maumivu makali sana. Wakati huo nilikuwa sijajazwa Roho Mtakatifu. Nilienda hosipitalini na daktari aliponipima alinambia kuwa sina ugonjwa kifuani bali ni mawazo tu. Niliendelea kuumwa na nikazidiwa sana. Yule mwanamke alipoona nakaribia kufa alinijia akiwa amejaa chuki na akaniambia kuwa haya yote yamenipata kwa sababu nilikataa kuzini naye. Wale wenzangu waliokuwa wameokoka walinieleza juu ya uponyaji wa Yesu na kunisomea maandiko ya
"Marko 16:17-18 ''Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;" 
Wakaniuliza "je unaamini jina la Yesu?" nikawaambia ndio. Ndipo walipoweka mikoni juu yangu na kwa jina la Yesu wakamwamuru pepo ndani yangu anitoke, saa hiyo hiyo , kile kitu kikapiga kelele ndani yangu kikatoka nikawa mzima pale pale. Nikapigwa na mshangao mkubwa nikabakia nikiangalia kulikuwa na nini kwenye mikono yao na nilipoona hakukuwa na kitu chochote isipokuwa jina la YESU tu ndipo nilipoamua mimi na maisha yangu yote nitamtumikia Bwana Yesu. Yule mwanamke alipoona nimepona alikasirika sana na kuniambia ni lazima ataniua . Nilikuwa tayar nina ujasiri mkubwa wa jina la Yesu hivyo nikampuuzia na kumwambia "Hutaniweza kwani mimi nina jina la Yesu" kuanzia wakati ule yule mama aliogopa sana, mwishowe alihama Arusha na hatimaye aliugua ugonjwa wa kuvimba mwili na akafa
Shetani aliazimia kuniua tena wakati huu waziwazi, lakini Mungu aliniandaa kwa wakati wangu ili adhihirishe Uweza wake kwa watu wa kizazi chetu, naye shetani hali akijua hayo alijitahidi kutaka kuniangamiza mara nyingi ili kusudi la Mungu lisitimie lakini kama vile Neno lake lisemavyo katika Isaya 55:11 "Ndivyo litakavyokuwa neno langu litokalo katika kinywa changu halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu nalo litafaikiwa katika mambo yale niliyolituma" katika Yeremia 1:12 amesema "Ninaliangalia neno langu ili nilitimize" kwa maana halisi ni kwamba Mungu hulilinda Neno lake, na kuhakikisha kuwa limefanikiwa na kutekeleza yale aliyolituma. Mimi nilishangazwa sana na matokeo ya mambo ambayo yalikuwa yakinipata kwani nilipokuwa nikiangalia wenzangu hawakuwa wakipatwa na jambo lolote mfano wa hayo.


 NAJAZWA NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU.

Nilianza kuutafuta uso wa Bwana, ili nipate ahadi ya Roho wake; nakumbuka nilikesha mbele zake kwa maombi kwa muda kama wa miezi mitatu. Siku moja tulikuwa kwenye Conference huko puge Tabora, na nguvu za Mungu zilikuwepo kwa wingi sana. Yule mtu aliyekuwa akihubiri alipomaliza alisema "wote tuseme moto" na watu wote tukasema moto. Mara zikanishukia nguvu nyingi nikajikuta nanena maneno nisiyoyafahamu. Niliendelea kunena kwa lugha kwa masaa mengi , moyo wangu ulifurika nguvu za Mungu na hapo hapo nikaanza kupokea moyo wa kwenda nyumbani kwetu Moshi nikawaeleze mambo ambayo Mungu amenitendea.
Tuliporudi Arusha kutoka Puge Tabora niliendelea kukesha na kuomba. Siku moja Mmisionari  tuliyekuwa naye ambaye aliitwa Claeson aliniita akaniambia "Mungu amesema nenda nyumbani kwenu" Mimi sikujua maana yake ni nini ila moyoni  mwangu nilishataka sana kwenda nyumbani niwaeleze yale yaliyonitokea. Mara nilipofika, nilienda kanisani kwetu nikamwomba Mchungaji aniruhusu niwaambie mambo ambayo Mungu amenitendea . Akaniuliza ni mambo gani nikamweleza jinsi nilivyookoka na jinsi Mungu alivyoniponya kwa jina la Yesu na jinsi nilivyojazwa Roho Mtakatifu kama mitume.
Mchungaji akaniambia "Siwezi kukuruhusu kwa kuwa wewe unataka kuleta dini mpya hapa" Nikamwambia sio kweli ila tu nataka kushuhudia Bwana alivyonitendea . Kwakwel mimi sikuwa na haja ya kuhubiri ila tu  hamu yangu kuwaeleza yale Bwana aliyonitendea. Nilipoona Mchungaji amekataa niliwafuata vijana nikawaeleza jinsi nilivyookoka, nilivyoponywa na kujazwa Roho. 
Vijana wakashangaa sana wakaniuliza "je hata sisi tunaweza kujazwa Roho vile vile kama wewe? " Nikawaambia "ndio" wakaniuliza "tufanyeje ili tupate huo ujazo?" Nikawaambia ni kwa njia ya kuomba tu. Wakaniambia "Tuko tayari tuongoze jinsi ya kuomba" Mimi nikaanza kuogopa nikifikiri kama tukiombea kanisani na Roho Mtakatifu akashuka itatokea hali ambayo viongozi wa kanisa hawataipenda, na mimi nitasumbuliwa na sikutaka niwakosee viongozi wa kanisa langu.
Kwa hiyo nikawaambia kama mnataka kujazwa Roho, twendeni porini tukaombee huko. Huku nikijua kama Roho akishuka huko hakuna mtu atakayetusikia. Vijana kwa kuwa walitamani sana kujazwa Roho walikubali kwenda porini bila kujali, kwa kuwa hamu yao ilikuwa ni kujazwa Roho tu.
Source:maishaushindi.blogspot.com


Ndugu msomaji wa blog hii, kati ya makala au masomo ambayo nimeyaandika humu, hili ni somo na ushuhuda mmojawapo wenye nguvu sana ambao, kila mwana wa Mungu atakayeusoma, atapata msukumo wa rohoni usio wa kawaida. Haya ni mafunuo yenye nguvu mno ambayo, hakika yatakuinua kwa kiwango cha juu sana nawe utamshukuru Mungu. Nilipouona ushuhuda huu kwenye mtandao, moyo wangu ulianza kuwaka niweze kuutafsiri harakaharaka na kuuweka kwenye blog hii ili yamkini uweze kuwafikia wapendwa wengi iwezekanavyo.



Huu ni ushuhuda ulioandikwa na Mchungaji John Mulinde wa Uganda kutokana na kile alichosikia kutoka kwa mhusika mwenyewe. Mhusika huyo, mchungaji hajamtaja, lakini alikuwa ni kijana ambaye alimtumikia shetani tangu angali tumboni mwa mama yake. Baadaye, kwa neema ya Bwana kijana huyo aliokolewa, ndipo akaanza kueleza siri hizi za ufalme wa giza na ufalme wa nuru.


Mamilioni ya Wakristo duaniani tunamwomba Mungu wetu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali tuliyonayo. Lakini liko swali moja kubwa linalojirudiarudia ndani ya mioyo yetu karibu kila siku. Tunajiuliza, “Nimeomba sana na kwa muda mrefu. Mbona Mungu hajibu...?” Tunabaki bila majibu, tunavunjika moyo, na tunaanza kudhani labda sisi ni wenye dhambi sana ndio maana hatujibiwi.


Ukiifahamu siri iliyomo kwenye ushuhuda huu, utatiwa nguvu sana za rohoni; maana maarifa ndiyo yanayotufanya tuwe na nguvu za Mungu. Tunaenenda kiimani kwa kadiri ya kiwango cha maarifa au ufahamu uliomo ndani yetu. Tukijua sana, tunaweza sana; tukijua kidogo, tunaweza kidogo.


Karibu ujipatie maarifa ambayo Bwana wetu ameruhusu yatufikie. Nami na hakika utamfurahia Bwana kwa kukupigisha hatua nyingine ya imani. Utafanya vema kama ukiweza kuwapatia na wengine somo hili la muhimu sana kwa ajili ya mwili wa Kristo.


******************

Yafuatayo ni maelezo ya Mchungaji John Mulinde:
Napenda nikushirikishe ushuhuda wa kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana ambaye alikuwa akimtumikia ibilisi. Na mtu yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia changamoto kubwa sana. Sikutaka kuamini. Ilinibidi nifunge kwa muda wa siku kumi mbele za Bwana, huku nikimuuliza, "Bwana, hivi mambo haya ni kweli?" Na ilikuwa ni katika wakati huo ndipo Bwana alipoanza kunifundisha kile kinachotokea kwenye ulimwengu wa roho pale tunapoomba.

Kijana huyu alizaliwa baada ya wazazi wake kuwa wamejiweka wakfu wao wenyewe kwa lusifa. Wakati bado akiwa tumboni, walifanya matambiko mengi na kumweka wakfu awe mtumishi wa lusifa. Alipozaliwa na kufikisha miaka minne, tayari alianza kutumia nguvu zake za kiroho. Hata wazazi wake walianza kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba yake alimkabidhi kwa wachawi ili akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka kumi, alikuwa akifanya mambo makubwa katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa akiogopwa hata na wachawi wa kawaida.

Alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni mabaya mno. Alikua hadi kufikia miaka ya ishirini akiwa na damu nyingi ya watu mikononi mwake. Aliua watu kila alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka nje ya mwili wake kupitia taamuli ya kinjozi (transcendental meditation), yaani kitendo cha kutuliza mawazo na mwili kama wafanyayo Wahindukatika yoga. Tazama mfano HAPA. Katika huko kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka kimwili kutoka ardhini pale alipokaa na kuelea hewani (levitate). Tazama mfano HAPA. Wakati mwingine aliweza kutoka nje ya mwili; akauacha mwili wake na kwenda nje huko na kule kufanya mambo mbalimbali (astro-travelling).  Na kijana huyu alitumiwa na shetani kuharibu makanisa mengi; na kuwaharibu wachungaji wengi.

Siku moja, alipangiwa kwenda kuharibu kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi ya kutosha. Kulitokea na migawanyiko mingi kanisani na kuchanganyikiwa kwingi. Alianza kufanya kazi kwenye kanisa hili; lakini mchungaji wa kanisa lile aliitisha mfungo wa kanisa zima. Kanisa lilipoanza kufunga, watu walitubu sana na kufanya mapatano mengi. Na watu wakawa kitu kimoja, na wakaanza kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana katikati yao. Na wakaendelea kufanya maombezi na kumlilia Mungu ili awarehemu na kuingilia kati maishani mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea, bwana huyu alikuwa akija tena na tena akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili. Lakini lilitoka neno la kinabii likiwaambia Wakristo wasimame pamoja na kufanya vita dhidi ya nguvu za giza ambazo zilikuwa zinashambulia kanisa lile.

Siku moja, kijana huyu aliuacha tena mwili wake chumbani kwake na akatoka nje. Aliongoza jeshi kubwa la mapepo moja kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili kwenda kufanya vita vya kiroho.

Sasa, ufuatao ni ushuhuda wake.

Roho yake ilikuwa inapaa hewani juu ya kanisa lile na kujaribu kulishambulia, lakini kulikuwa na kifuniko cha nuru juu ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na mapambano, ghafla, kulikuja jeshi la malaika ambalo liliwashambulia na kukawa na mapambano makali pale hewani. Hatimaye, mapepo yalikimbia, lakini yeye alikamatwa na wale malaika.  

Ndiyo, alikamatwa na malaika! Alijiona akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na wakamleta kwa kumpitisha kwenye paa hadi kwenye madhabahu ya kanisa. Akawa yuko pale huku watu wanaendelea kuomba. Walikuwa wamezama kwenye maombi, wakifanya vita vya kiroho; wakifunga na kuvunja, na kutupa nje. Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu akiongoza maombi hayo na vita. Roho wa Bwana akaongea na mchungaji, akisema, "Nira imevunjika, na mhusika yuko hapa mbele yako. Msaidie kwa kumfungua."

Mchungaji alipofungua macho yake, alimwona yule kijana akiwa ameanguka pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa pamoja naye! Kijana yule anasema kuwa haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana naye; maana alikuwa ameuacha nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui ni kwa vipi aliingia, isipokuwa tu malaika walimpitishia kwenye paa.



Sasa, mambo haya ni magumu kuamini, lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na kuwaambia kile ambacho Bwana alimwambia. Kisha akamwuliza yule kijana, "Wewe ni nani?" Kijana yule alikuwa anatetemeka wakati mapepo yalipoanza kumtoka.

Kwa hiyo, waliomba kwa ajili ya kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye alianza kusema ushuhuda wake. Hivi sasa kijana huyu ameshaingia kwa Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri Injili. Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka huru watu wengine.    

Usiku mmoja, mimi (John Mulinde) nilienda kwenye chakula cha usiku mahali fulani. Sababu hasa ya kwenda pale ni kwa vile kuna mtu alinieleza habari za huyo kijana; na nilikuwa na shauku kubwa sana ya kumwona, na kuona kama kweli hadithi yake ina ukweli wowote. Kwa hiyo, nilipofika, nilikaa mezani. Na jioni ile, kijana huyu alipewa nafasi ya kutoa ushuhuda wake. Alizungumza juu ya mambo mengi sana. Mara nyingine alilia kutokana na mambo aliyoyafanya. Alipomaliza kusema, alitoa ombi.

Kulikuwako na wachungaji wengi pale kwenye ukumbi. Alisema, "Ninawaomba ninyi, wachungaji. Tafadhalini, wafundisheni watu namna ya kuomba.”  Watu ambao hawaombi, wanaweza kuchukuliwa na chochote, katika chochote na ibilisi; na ziko hata njia za adui za kutumia maisha yao na maombi yao. Adui anajua hata namna ya kutumia kwa faida yake maombi ya watu wasiojua kuomba. "Wafundisheni watu namna ya kutumia silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa."

Kisha alieleza jinsi ambavyo alikuwa akiongoza mapambano kwenye anga. Alikuwa akienda pamoja na maajenti wengine wa shetani na mapepo mengi hadi angani. Ilikuwa kama zamu. Inabidi kwenda kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo, ni mara nyingi tu alikuwa na muda wa kwenda kwenye anga ili kufanya vita. Na akasema kuwa kule angani, kwenye ulimwengu wa roho, kama anga limefunikwa na blangeti la giza, blangeti hilo linakuwa ni nene sana; na ni kama jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote. Na mapepo haya yanaweza kwenda juu yake na chini yake. Na yakiwa huko, yanaweza kuathiri matukio yanayoendelea duniani. 

Pale mapepo wachafu pamoja na maajenti wa shetani wa kibinadamu wanapomaliza zamu yao, wanashuka duniani kwenye maeneo ya kimaagano, iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza kurejesha upya nguvu zao, maana zinakuwa zimepungua kutokana na kufanya kazi angani wakati wa zamu yao. Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia kafara ambazo watu wanatoa kwenye madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa ni uchawi wa wazi, damu za aina zote, ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na utoaji wa kafara za wanadamu na wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara za uzinzi, pale ambapo watu wanafanya uzinzi na uashetati wa kila aina. Na matendo haya maovu yanaleta nguvu kwenye ulimwengu wa giza. Na ziko aina nyingi za kafara. 

Kijana huyo alisema kuwa, maajenti wa shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na Wakristo wakaanza kuomba hapa duniani, maombi ya Wakristo huonekana kwa namna tatu. Maombi yote huonekana kama moshi ambao unapaa kuelekea mbinguni.

Baadhi ya maombi huonekana kama moshi, na yanaenda juu kiasi na kupotelea hewani. Maombi ya aina hii hutoka kwa watu ambao wana dhambi maishani mwao na hawako tayari kushughulika nazo. Maombi yao ni dhaifu sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na kupotelea angani.

nyingine ya maombi nayo ni kama moshi ambao unainuka juu hadi unapofikia kwenye ule mwamba, lakini hayana nguvu ya kupenya mwamba huo. Kwa kawaida, hawa ni watu ambao hujaribu kujitakasa, lakini hawana imani juu ya kile ambacho wanakifanya pale wanapoomba, yaani wanaomba lakini moyoni hawana ujasiri kwamba kile wanachokiomba watakipokea. Mara nyingi huwa wanapuuzia mambo mengine ya muhimu yanayotakiwa wakati mtu anapoomba. 

Aina ya tatu ya maombi ni kama moshi ambao umejaa moto. Yanapokuwa yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana kiasi kwamba yanapoufikia ule mwamba, unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya mwamba huo na kuendelea hadi juu.

Mara nyingi watu wanapoanza kuomba, maombi yao huonekana kama aina ya kwanza ya maombi. Lakini kadiri wanavyoendelea kuzama, yanageuka na kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea zaidi, ghafla yanalipuka moto. Na maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana kiasi kwamba yanapenya kabisa ule mwamba.

Mara nyingi maajenti wa uovu hubaini kwamba kuna maombi yanabadilika na kuelekea kwenye kuwa moto. Kisha huwasiliana na viumbe vingine vilivyoko duniani na kuwaambia, "Mvurugieni mtu huyo maombi! Mfanyeni aache kuomba! Mwondoeni kwenye maombi!"

Mara nyingi Wakristo hushindwa na mbinu hizi. Wanakuwa wanaomba kwa nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno kukagua nafsi zao; imani inaanza kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa na shabaha zaidi. Kisha ibilisi anaona kuwa maombi yao yanaanza kukusanya nguvu. Ndipo vurugu zinaanza ili kuharibu maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati mwingine, katikati ya maombi ambapo mtu alikuwa amezama kabisa, , simu inaweza kulia na unawaza kuwa, ngoja niende nikaipokee kisha nitarudi kuendelea na maombi.  

Mbinu zingine za kuvuruga maombi nazo zinaweza kutumika; hata kama ni kukugusa mwili wako na kuleta maumivu mahali fulani. Hata pia kukufanya ujisikie njaa ambapo utajisikia kwenda jikoni kutengeneza japo chakula kidogo. Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke mahali pale, wanakuwa wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima muwafundishe watu jinsi ya kuomba. Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi ya juujuu. Mara moja kwa siku, Wakristo wanatakiwa kuwa na muda wa kujielekeza kwa moyo wote kwa Mungu, bila kuwapo kwa kitu chochote cha kuwaharibia umakini wao. 

Na kama watu waking’ang’ana kabisa kwa njia hii ya maombi na kuruhusu kupata mwongozo wa kiroho, kisha wakawa wanaendelea na kuendelea, lazima kitu kitatokea rohoni. Moto utalipuka na kugusa ule mwamba na kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni moto sana kiasi kwamba hakuna pepo ambaye anaweza kustahimili. Wala hakuna roho ya mwanadamu inayoweza kustahimili pia. Wote wanakimbia.

Kama mtu atajitoa kuomba kwa bidii na kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye kutafuata kufunguka kwa ulimwengu wa roho. Na mara hili linapotokea, matatizo yote haya katika maombi yanafikia mwisho! [Yaani ule ugumu na ule uzito unakwishilia mbali!] Yule ambaye anakuwa anaomba duniani anakuwa sasa anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini kabisa, cha kuburudisha, na chenye nguvu.

Na nimegundua kuwa wakati huo, huwa tunapoteza kabisa hisia za muda na mambo mengine. Si kwamba tunakosa mpangilio; la hasha! Mungu anakuwa anashughulika na muda wetu. Lakini inakuwa ni kama unaachilia kila kitu, na unaunganishwa moja kwa moja na Mungu. Maombi yako yanapopenya, kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia hapo; na mtu anayeomba anaweza kuendelea kwa muda mrefu kama apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi. 

Na mara anapomaliza kuomba, lile tundu linabakia wazi.

Kijana huyu pia alisema kuwa, watu wa namna hii wanapomaliza kuomba na kuondoka mahali hapo, lile tundu linakuwa linaondoka pamoja nao. Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile blangeti la jiwe. Wanakuwa wanaenenda chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema kwamba, katika hali hiyo, ibilisi hawezi kufanya kile anachokitaka kwao. Na uwepo wa Mungu unakuwa kama nguzo kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha yao. Wanalindwa; na kunakuwa na nguvu kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi kwamba kadiri wanavyotembea huku na kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata watu wengine. Nguzo hiyo inakuwa inatambua kile ambacho adui amefanya kwa watu wengine. Na pale watakatifu hao wanapozungumza na watu wengine, na wale watu wakawa wamesimama nao, wanaingia ndani ya nguzo hiyo. Na mradi tu wakiwa ndani ya ile nguzo, vifungo vyote vya adui vinadhoofika.  

Kwa hiyo, watu hawa wenye mpenyo huu wa kiroho wanapowashuhudia wenye dhambi habari za Yesu Kristo, upinzani wa wenye dhambi unakuwa wa chini. Ni rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa Kristo. Wanapoomba kwa ajili ya wagonjwa, au kwa ajili ya mambo mengine, maombi yao yanakuwa na nguvu sana.

Na kama kuna sehemu ambako maombi ya namna hii huombwa mara kwa mara, uwepo wa Mungu unakuja mahali pale na hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama hizo, ghafla vifungo vyao vinakatika.

Na kama atatokea mtu wa kusema nao kwa uvumilivu na kwa upendo, wanaweza kugeuka haraka sana; si kwa nguvu au kwa uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu, ambaye anakuwa yuko pale. Na kama hakuna mtu atakayewajali watu hawa, wanakuja kwenye uwepo wake na kujisikia hatia, wanaanza kujadili kama wakubali au la. Pale watakapoondoka, vifungo vinakuwa na nguvu zaidi kwao. Na ibilisi anajihadi kwa kila njia kutowaruhusu kurudi tena kwenye sehemu kama hizo.

Je, shetani anakaa kimya tu baada ya mtu kupata mpenyo?

Kijana huyu alisema kuwa, ibilisi anawachukia sana watu wa namna hiyo, yaani wale waliopata mpenyo wa maombi.

Sasa unaweza kupiga picha, sote tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia kijana huyu akieleza ushuhuda wake. Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiyafanya na aliyoyashuhudia kwa macho yake. Alitueleza kile ambacho walifanya kwa watu ambao walipata mpenyo katika maombi. Alisema kuwa waliwaweka akilini sana watu kama hao. Kisha waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu wao ili kuwajua vizuri. Walitafuta kila kitu kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu wao wote, na ikitokea mtu akawashinda kwenye maombi na kupenya, wanawasiliana na wengine kwenye ulimwengu wa giza na kusema, "Mumlenge mtu huyu kwenye eneo hili na hili. Udhaifu wake uko hapa na hapa."

Kwa kuwa mtu wa aina hii anapotoka nje ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi inakuwa juu yake, uwepo wa Mungu upo juu yake, roho yake inakuwa iko juu, na furaha ya Bwana ndiyo nguvu zake; anapokuwa anaenda, adui anajaribu kila njia kuleta yale mambo ambayo yatamvuruga ili asielekeze macho yake kwa Bwana.

Kama, kwa mfano, imeshajulikana kuwa udhaifu wake uko kwenye eneo la hasira, basi adui atasababisha watu watende mambo ambayo yatamfanya akasirike. Na kama hayuko makini kumsikiliza Roho Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi ataondoa macho yake kwa Bwana. Na anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu zinamjaa. Baadaye anapokuja kujirudi, anakuwa anataka kutupilia mbali hali hiyo na kuendelea na furaha ya Bwana, lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha kama mwanzo. Anajitahidi kujisikia vizuri tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini? Alipojiachilia kwenye kishawishi cha hasira, mapepo walifanya bidii zote katika muda huo kufunga lile tundu kule juu. Na mara waliporudishia lile jiwe, uwepo wa Bwana unakuwa umekatika, yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea mbinguni na kumfunika inakuwa haimfikii tena!

Mtu huyo hataacha kuwa mwana wa Mungu. Lakini ule upako wa ziada uliokuwa unaandamana naye maishani; ule uwepo uliokuwa ukitenda mambo bila yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa umekatika! Maana pepo wachafu wanatafuta uliko udhaifu wako. 

Kama udhaifu wa mtu ni kwenye masuala ya mapenzi, adui ataandaa watu, matukio, na mambo ambayo yatainua hisia za mtu huyo za tamaa ya kimapenzi. Na kama mtu huyo atazikubalia hizo tamaa na kufungua akili yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea nafsini mwake, pale anapomaliza kila kitu na kutaka kurejea tena kwenye hali ya upako ili asonge mbele, anakuta kwamba ule uwepo haupo tena. Labda unasema, “Hii si vizuri kabisa.” Kumbuka tu Biblia inasemaje, " Tena ipokeeni chapeo ya wokovu. Vaeni dirii ya haki." Mara nyingi hatuoni haja ya silaha hizi za kivita. Lakini kumbuka Yesu alivyotuambia juu ya namna ya kuomba "Usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu."

Kila mara unapopata mpenyo katika maombi, unapofika mwisho, kumbuka kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu aliye dhaifu. Kumbuka kuwa haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana, useme, "Bwana, nimefurahia wasaa huu wa maombi, lakini nitakapotoka nje kwenye dunia, usiniongoze kwenye majaribu. Usiruhusu niangukie kwenye mtego wa ibilisi. Najua kuwa adui anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego ya namna gani. Na ninajua kuwa bado mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo. Kama nikiingia kwenye hali fulani fulani, nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona ninaelekea kule ambako kuna mitego niliyotegewa, nifanye nielekee upande mwingine. Uingilie kati, Ee, Bwana. Usiche niende tu kwa nguvu zangu na uwezo wangu. Niokoe na yule mwovu.”

Mungu anaweza kufanya hivyo. Lakini, kama kuna kitu kibaya kitatokea, ambacho kitakufanya uondoe macho yako kwa Kristo, wewe sema tu, “Asante Yesu.” Ndiyo sababu Mtume Paulo aliandika, “Mshukuruni Mungu kwa kila jambo.” Baadhi ya mambo si mazuri. Yanaumiza, na tunashangaa kwa nini Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini kama tu tungejua kwa njia hiyo anatuokoa na mambo yapi,  tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini Bwana, tutamshukuru kwa kila jambo.

Yule kijana aliendelea kusema kuwa, unapopata mpenyo katika maombi, majibu yako ni lazima yatakuja. Alisema kuwa jibu mara zote huja, lakini mara nyingi, huwa halifiki kwa mtu aliyeliomba. Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano yaliyoko kwenye anga. Pia, majibu yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu wa rohoni watafanikiwa kurejesha ule mwamba na kuziba tundu ambalo mwombaji alifanikiwa kulitoboa kwa njia ya maombi yake. 

Kisha aliongea jambo ambalo kwa kweli lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi niingie kwenye mfungo wa siku kumi, ili kumwuliza Bwana kama hilo alilosema lilikuwa na ukweli wowote. Basi sikiliza haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila Mkristo anaye malaika ambaye anamtumikia Mkristo huyo. Nasi tunafahamu kuwa Biblia inasema kuwa malaika ni roho wanaotutumikia. (Waebrania 1:14).  Alisema kuwa watu wanapoomba, majibu huletwa kwa mikono ya malaika. Malaika huleta majibu, kama ambavyo tunasoma kwenye kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo ambalo ni gumu sana. Alisema kwamba, kama yule anayeomba anafahamu silaha za kiroho na amejivika silaha hizo, majibu nayo huja kwa kupitia malaika ambaye, naye amejivika kikamilifu kwa silaha hizohizo.

Lakini, kama anayeomba hajali silaha za kiroho, basi malaika nao wanakuja bila silaha hizo. Wakristo ambao hawajali kile ambacho kinaingia mawazoni mwao; hawashindani kuangusha mawazo yasiyofaa; malaika wao huja bila chapeo. Silaha zozote utakazoacha kuzitilia maanani duniani, malaika anayekutumikia naye anakuwa hanazo. Kwa maneno mengine, silaha zetu za kiroho hazitulindi miili yetu, bali zinalinda vitu vile vya kiroho tunavyofanikiwa kuvipata kutoka kwa Bwana.

Malaika anapokuwa anakuja, mapepo wanamtazama na kumkagua na kubaini maeneo ambayo hajajifunika; na hayo ndiyo maeneo ambayo watashambulia. Kama hana chapeo kichwani, basi watashambulia kichwani. Kama hana dirii, watashambulia kifuani. Kama hana viatu, watajaribu kutengeneza moto ili kumwunguza miguuni.

Sasa, najua kuwa hili ni gumu kuamini; mimi narudia tu kile ambacho kijana huyu alisema. Kisha tulimwuliza, “Je, malaika wanaweza kuungua moto?” Na unajua alisema nini? Kumbuka kuwa huu ni ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho zinapambana. Mapambano ni makali sana, na pale wanapomshinda malaika wa Mungu, jambo la kwanza wanalokimbilia ni lile jibu alilobeba; na wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa ni zawadi ambazo hutolewa kwa watu kupitia imani za siri, au uchawi.

Kumbuka kile ambacho Biblia inasema kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote vyema hutoka kwa Mungu (Yakobo 1:17). Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu vizuri anavyowapatia watu? Baadhi ya watu ambao hawawezi kupata watoto, huenda kwa wachawi na waabudu shetani, na wanapata mimba! Mtoto anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni muumbaji? HAPANA! Anaiba kutoka kwa watu ambao hawaombi maombi yao hadi mwisho.

Katika Biblia, Yesu alisema, "Ombeni bila kukoma." Pia alisema, "atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? " Je, Yesu atakukuta bado unangojea? Au utakata tamaa na kumwacha adui aibe kile ambacho umekuwa ukikiombea?

Na hawaridhiki tu na kuiba jibu la maombi. Wanataka pia kumweka malaika kifungoni. Na wanaanza kupambana naye. Wakati mwingine wanafanikiwa kumkamata na kumfunga malaika. Inapotokea hivyo, Mkristo anakuwa kama chakula chao duniani. Wanaweza kumfanyia chochote maana hana ulinzi tena kwenye ulimwengu wa roho.

Nilimwuliza kijana huyo, “Una maana kuwa malaika anaweza kushikiliwa katika ulimwengu wa giza?” Sasa alikuwa anaeleza uzoefu wake, na akasema, hawatamshikilia malaika kwa muda mrefu kwa sababu ya Wakristo wengine ambao wanaomba mahali pengine. Jeshi la ziada litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na kama yule Mkristo anayehusika hajaomba hadi kwenye mpenyo, basi atabakia mateka. Ndipo shetani atatuma malaika wake na malaika wa nuru  kwa mtu huyu, na hapo ndipo uongo na udanganyifu unapotokea; maono ya uongo na unabii wa uongo. Uongozi wa uongo, na kufanya kila aina ya maamuzi mabaya. Na mara nyingi, mtu wa namna hii anaweza kupata mashambulizi na vifungo vya kila aina.

Niliondoka kwenye kile chakula cha jioni huku na mawazo mengi sana. Nikasema, “Bwana, sitaki hata kujaribu kuamini jambo hili.” Linaondoa ujasiri na usalama wangu wote! Nilipoenda kumlingana Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na Bwana alifanya mambo mawili. Kwanza, si tu kwamba alithibitisha mambo hayo niliyoyasikia kutoka kwa yule kijana, bali pia alifungua akili zangu zaidi ili kuona mambo mengine mengi zaidi ya yale ambayo niliyasikia. Pili, aliniongoza kuona kile ambacho tunatakiwa kukifanya wakati mambo haya yanapotokea ili tuweze kuwa washindi.

Alinipa mambo matatu:

Moja: namna ya kutumia silaha za vita vyetu vya kiroho. Biblia inaziita silaha za Mungu. Si silaha zetu. Tunapozitumia, tunamruhusu Mungu kupigana kwa niaba yetu.

Mbili: tambua uhusiano wa roho zinazotutumikia, yaani malaika, na maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima kuwa makini sana na kile kinachotokea mioyoni mwetu; kama mwongozo wa kile ambacho kinatakiwa kutokea rohoni kutuhusu sisi.

Tatu: ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatakiwi kuja kama mtumishi wetu, kututumikia na kutuletea vitu mbalimbali. Hakimbiikimbii kwa Baba kumweleza kile ambacho tunataka. Hiyo ni kazi ya malaika. Lakini Yeye husimama pamoja nasi. Anafanya nini? Anatuongoza, anatufundisha, anatutangulia, anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na mambo haya yanapotokea kwenye ulimwengu wa roho, anatuambia. Wakati mwingine anakuamsha usiku na kukwambia, “Omba.” Wewe unasema, “Hapana! Muda wangu haujafika.” Na anasema, “Omba sasa!” Kwa nini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Wakati mwingine anasema, “Kesho ni kufunga.” Wewe unasema, “Hapana, nitaanza Jumatatu!” 

Lakini kumbuka kuwa Yeye anaelewa kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Ni lazima tujifunze kuwa makini na Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye njia za haki. Wapendwa, tuishie hapa. Labda wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo tunaweza kuomba hadi kupata mpenyo, maana sasa tunajua mapambano yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na namna tunavyoweza kudumu tukiwa na mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza hili, linakuwa ni jambo la furaha sana. Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu, bali ni vya Bwana! Haleluya! 

Hebu tusimame. Mwangalie mwenzio machoni na utafakari ni mara ngapi amekosa kile ambacho Mungu alikiandaa kwa ajili yake. Lakini shikaneni mikono kama inawezekana; watu wawili au watatu, kisha tu muambiane, “Hakuna haja ya kushindwa tena! Tunaweza kushinda! Iko nguvu ya kutosha kushinda! Yesu tayari ameshafanya kazi yote.” Muombeane ninyi kwa ninyi ili Bwana aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi kushindwa. Iko neema ya kutosha; nguvu ya kutosha kuleta ushindi!

Asante Yesu.


**********************


Ndugu msomaji wa blog hii, somo hili ambalo ni muhimu sana kwa kila mwanadamu na mwili wa Kristo, nimeliweka pia kama E-Book, hivyo unaweza kulipakua na kulisoma tena na tena; na pia kuwagawia wengine. Bofya HAPA.


Unaweza pia kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza (pamoja na shuhuda zingine) kwa kubofya HAPA.


Usikate tamaa. Simama imara katika imani. Unaweza kushinda. Bwana si dhalimu; anakupenda na amekuwa akijibu maombi yako siku zote. Je, Biblia si inasema kuwa KILA aombaye hupokea? (Mathayo 7:8). Na kwamba Mungu si mwanadamu hata aseme uongo (Hesabu 23:19).


Tumia mafunzo haya kusonga mbele katika wokovu na imani yako. Bwana Yesu akubariki sana.
 By James John