Ndugu msomaji
wa blog hii, kati ya makala au masomo ambayo nimeyaandika humu, hili ni somo na
ushuhuda mmojawapo wenye nguvu sana ambao, kila mwana wa Mungu atakayeusoma,
atapata msukumo wa rohoni usio wa kawaida. Haya ni mafunuo yenye nguvu mno
ambayo, hakika yatakuinua kwa kiwango cha juu sana nawe utamshukuru Mungu.
Nilipouona ushuhuda huu kwenye mtandao, moyo wangu ulianza kuwaka niweze
kuutafsiri harakaharaka na kuuweka kwenye blog hii ili yamkini uweze kuwafikia
wapendwa wengi iwezekanavyo.
Huu ni
ushuhuda ulioandikwa na Mchungaji John Mulinde wa Uganda kutokana na kile
alichosikia kutoka kwa mhusika mwenyewe. Mhusika huyo, mchungaji hajamtaja,
lakini alikuwa ni kijana ambaye alimtumikia shetani tangu angali tumboni mwa
mama yake. Baadaye, kwa neema ya Bwana kijana huyo aliokolewa, ndipo akaanza
kueleza siri hizi za ufalme wa giza na ufalme wa nuru.
Mamilioni ya
Wakristo duaniani tunamwomba Mungu wetu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali
tuliyonayo. Lakini liko swali moja kubwa linalojirudiarudia ndani ya mioyo yetu
karibu kila siku. Tunajiuliza, “Nimeomba sana na kwa muda mrefu. Mbona Mungu
hajibu...?” Tunabaki bila majibu, tunavunjika moyo, na tunaanza kudhani labda
sisi ni wenye dhambi sana ndio maana hatujibiwi.
Ukiifahamu
siri iliyomo kwenye ushuhuda huu, utatiwa nguvu sana za rohoni; maana maarifa
ndiyo yanayotufanya tuwe na nguvu za Mungu. Tunaenenda kiimani kwa kadiri ya
kiwango cha maarifa au ufahamu uliomo ndani yetu. Tukijua sana, tunaweza sana;
tukijua kidogo, tunaweza kidogo.
Karibu
ujipatie maarifa ambayo Bwana wetu ameruhusu yatufikie. Nami na hakika
utamfurahia Bwana kwa kukupigisha hatua nyingine ya imani. Utafanya vema kama
ukiweza kuwapatia na wengine somo hili la muhimu sana kwa ajili ya mwili wa
Kristo.
******************
Yafuatayo ni maelezo ya Mchungaji John Mulinde:
Napenda nikushirikishe ushuhuda wa
kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana ambaye alikuwa akimtumikia ibilisi. Na mtu
yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia changamoto kubwa sana. Sikutaka kuamini.
Ilinibidi nifunge kwa muda wa siku kumi mbele za Bwana, huku nikimuuliza,
"Bwana, hivi mambo haya ni kweli?" Na ilikuwa ni katika wakati
huo ndipo Bwana alipoanza kunifundisha kile kinachotokea kwenye ulimwengu wa
roho pale tunapoomba.
Kijana huyu alizaliwa baada ya wazazi
wake kuwa wamejiweka wakfu wao wenyewe kwa lusifa. Wakati bado akiwa tumboni,
walifanya matambiko mengi na kumweka wakfu awe mtumishi wa lusifa. Alipozaliwa
na kufikisha miaka minne, tayari alianza kutumia nguvu zake za kiroho. Hata
wazazi wake walianza kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba yake alimkabidhi kwa
wachawi ili akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka kumi, alikuwa akifanya mambo
makubwa katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa akiogopwa hata na wachawi wa kawaida.
Alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini
mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni mabaya mno. Alikua hadi kufikia miaka ya
ishirini akiwa na damu nyingi ya watu mikononi mwake. Aliua watu kila
alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka nje ya mwili wake kupitia taamuli ya
kinjozi (transcendental meditation), yaani kitendo cha kutuliza mawazo na mwili
kama wafanyayo Wahindukatika yoga. Tazama mfano HAPA. Katika huko kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka kimwili
kutoka ardhini pale alipokaa na kuelea hewani (levitate). Tazama mfano HAPA. Wakati mwingine aliweza kutoka nje ya mwili; akauacha
mwili wake na kwenda nje huko na kule kufanya mambo mbalimbali
(astro-travelling). Na kijana huyu alitumiwa na shetani kuharibu makanisa
mengi; na kuwaharibu wachungaji wengi.
Siku moja, alipangiwa kwenda kuharibu
kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi ya kutosha. Kulitokea na migawanyiko
mingi kanisani na kuchanganyikiwa kwingi. Alianza kufanya kazi kwenye kanisa
hili; lakini mchungaji wa kanisa lile aliitisha mfungo wa kanisa zima. Kanisa
lilipoanza kufunga, watu walitubu sana na kufanya mapatano mengi. Na watu
wakawa kitu kimoja, na wakaanza kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana katikati yao.
Na wakaendelea kufanya maombezi na kumlilia Mungu ili awarehemu na kuingilia
kati maishani mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea, bwana huyu alikuwa akija
tena na tena akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili. Lakini lilitoka neno la
kinabii likiwaambia Wakristo wasimame pamoja na kufanya vita dhidi ya nguvu za
giza ambazo zilikuwa zinashambulia kanisa lile.
Siku moja, kijana huyu aliuacha tena
mwili wake chumbani kwake na akatoka nje. Aliongoza jeshi kubwa la mapepo moja
kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili kwenda kufanya vita vya kiroho.
Sasa, ufuatao ni ushuhuda wake.
Roho yake ilikuwa inapaa hewani juu ya
kanisa lile na kujaribu kulishambulia, lakini kulikuwa na kifuniko cha nuru juu
ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na mapambano, ghafla, kulikuja jeshi la
malaika ambalo liliwashambulia na kukawa na mapambano makali pale hewani.
Hatimaye, mapepo yalikimbia, lakini yeye alikamatwa na wale malaika.
Ndiyo, alikamatwa na malaika! Alijiona
akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na wakamleta kwa kumpitisha kwenye paa hadi
kwenye madhabahu ya kanisa. Akawa yuko pale huku watu wanaendelea kuomba.
Walikuwa wamezama kwenye maombi, wakifanya vita vya kiroho; wakifunga na kuvunja,
na kutupa nje. Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu akiongoza maombi hayo na
vita. Roho wa Bwana akaongea na mchungaji, akisema, "Nira imevunjika,
na mhusika yuko hapa mbele yako. Msaidie kwa kumfungua."
Mchungaji alipofungua macho yake,
alimwona yule kijana akiwa ameanguka pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa pamoja
naye! Kijana yule anasema kuwa haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana naye;
maana alikuwa ameuacha nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui ni kwa vipi
aliingia, isipokuwa tu malaika walimpitishia kwenye paa.
Sasa, mambo haya ni magumu kuamini,
lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na kuwaambia kile ambacho Bwana
alimwambia. Kisha akamwuliza yule kijana, "Wewe ni nani?"
Kijana yule alikuwa anatetemeka wakati mapepo yalipoanza kumtoka.
Kwa hiyo, waliomba kwa ajili ya
kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye alianza kusema ushuhuda wake. Hivi sasa
kijana huyu ameshaingia kwa Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri Injili.
Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka huru watu wengine.
Usiku mmoja, mimi (John Mulinde)
nilienda kwenye chakula cha usiku mahali fulani. Sababu hasa ya kwenda pale ni
kwa vile kuna mtu alinieleza habari za huyo kijana; na nilikuwa na shauku kubwa
sana ya kumwona, na kuona kama kweli hadithi yake ina ukweli wowote. Kwa hiyo, nilipofika,
nilikaa mezani. Na jioni ile, kijana huyu alipewa nafasi ya kutoa ushuhuda
wake. Alizungumza juu ya mambo mengi sana. Mara nyingine alilia kutokana na
mambo aliyoyafanya. Alipomaliza kusema, alitoa ombi.
Kulikuwako na wachungaji wengi pale
kwenye ukumbi. Alisema, "Ninawaomba ninyi,
wachungaji. Tafadhalini, wafundisheni watu namna ya kuomba.” Watu ambao hawaombi, wanaweza kuchukuliwa
na chochote, katika chochote na ibilisi; na ziko hata njia za adui za kutumia
maisha yao na maombi yao. Adui anajua hata namna ya kutumia kwa faida yake
maombi ya watu wasiojua kuomba. "Wafundisheni watu namna ya kutumia
silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa."
Kisha alieleza jinsi ambavyo alikuwa
akiongoza mapambano kwenye anga. Alikuwa akienda pamoja na maajenti wengine wa
shetani na mapepo mengi hadi angani. Ilikuwa kama zamu. Inabidi kwenda
kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo, ni mara nyingi tu alikuwa na muda wa kwenda
kwenye anga ili kufanya vita. Na akasema kuwa kule angani, kwenye ulimwengu wa
roho, kama anga limefunikwa na blangeti la giza, blangeti hilo linakuwa ni nene
sana; na ni kama jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote. Na mapepo haya
yanaweza kwenda juu yake na chini yake. Na yakiwa huko, yanaweza kuathiri
matukio yanayoendelea duniani.
Pale mapepo wachafu pamoja na maajenti
wa shetani wa kibinadamu wanapomaliza zamu yao, wanashuka duniani kwenye maeneo
ya kimaagano, iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza kurejesha upya nguvu
zao, maana zinakuwa zimepungua kutokana na kufanya kazi angani wakati wa zamu
yao. Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia kafara ambazo watu wanatoa kwenye
madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa ni uchawi wa wazi, damu za aina zote,
ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na utoaji wa kafara za wanadamu na
wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara za uzinzi, pale ambapo watu wanafanya
uzinzi na uashetati wa kila aina. Na matendo haya maovu yanaleta nguvu kwenye
ulimwengu wa giza. Na ziko aina nyingi za kafara.
Kijana huyo alisema kuwa, maajenti wa
shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na Wakristo wakaanza kuomba hapa duniani,
maombi ya Wakristo huonekana kwa namna tatu. Maombi yote huonekana kama moshi
ambao unapaa kuelekea mbinguni.
Baadhi ya maombi huonekana kama moshi,
na yanaenda juu kiasi na kupotelea hewani. Maombi ya aina hii hutoka kwa watu
ambao wana dhambi maishani mwao na hawako tayari kushughulika nazo. Maombi yao
ni dhaifu sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na kupotelea angani.
nyingine ya maombi nayo ni kama moshi
ambao unainuka juu hadi unapofikia kwenye ule mwamba, lakini hayana nguvu ya
kupenya mwamba huo. Kwa kawaida, hawa ni watu ambao hujaribu kujitakasa, lakini
hawana imani juu ya kile ambacho wanakifanya pale wanapoomba, yaani wanaomba
lakini moyoni hawana ujasiri kwamba kile wanachokiomba watakipokea. Mara nyingi
huwa wanapuuzia mambo mengine ya muhimu yanayotakiwa wakati mtu anapoomba.
Aina ya tatu ya maombi ni kama moshi
ambao umejaa moto. Yanapokuwa yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana kiasi kwamba
yanapoufikia ule mwamba, unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya mwamba huo na
kuendelea hadi juu.
Mara nyingi watu wanapoanza kuomba,
maombi yao huonekana kama aina ya kwanza ya maombi. Lakini kadiri
wanavyoendelea kuzama, yanageuka na kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea zaidi,
ghafla yanalipuka moto. Na maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana kiasi kwamba
yanapenya kabisa ule mwamba.
Mara nyingi maajenti wa uovu hubaini
kwamba kuna maombi yanabadilika na kuelekea kwenye kuwa moto. Kisha huwasiliana
na viumbe vingine vilivyoko duniani na kuwaambia, "Mvurugieni mtu huyo maombi! Mfanyeni aache
kuomba! Mwondoeni kwenye maombi!"
Mara nyingi Wakristo hushindwa na mbinu
hizi. Wanakuwa wanaomba kwa nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno kukagua nafsi zao;
imani inaanza kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa na shabaha zaidi. Kisha
ibilisi anaona kuwa maombi yao yanaanza kukusanya nguvu. Ndipo vurugu zinaanza
ili kuharibu maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati mwingine, katikati ya maombi
ambapo mtu alikuwa amezama kabisa, , simu inaweza kulia na unawaza kuwa, ngoja
niende nikaipokee kisha nitarudi kuendelea na maombi.
Mbinu zingine za kuvuruga maombi nazo
zinaweza kutumika; hata kama ni kukugusa mwili wako na kuleta maumivu mahali
fulani. Hata pia kukufanya ujisikie njaa ambapo utajisikia kwenda jikoni
kutengeneza japo chakula kidogo. Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke mahali
pale, wanakuwa wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima muwafundishe watu jinsi
ya kuomba. Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi ya juujuu. Mara moja kwa
siku, Wakristo wanatakiwa kuwa na muda wa kujielekeza kwa moyo wote kwa Mungu,
bila kuwapo kwa kitu chochote cha kuwaharibia umakini wao.
Na kama watu waking’ang’ana kabisa kwa
njia hii ya maombi na kuruhusu kupata mwongozo wa kiroho, kisha wakawa
wanaendelea na kuendelea, lazima kitu kitatokea rohoni. Moto utalipuka na
kugusa ule mwamba na kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni moto sana kiasi kwamba
hakuna pepo ambaye anaweza kustahimili. Wala hakuna roho ya mwanadamu inayoweza
kustahimili pia. Wote wanakimbia.
Kama mtu atajitoa kuomba kwa bidii na
kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye kutafuata kufunguka kwa ulimwengu wa roho.
Na mara hili linapotokea, matatizo yote haya katika maombi yanafikia mwisho!
[Yaani ule ugumu na ule uzito unakwishilia mbali!] Yule ambaye anakuwa anaomba
duniani anakuwa sasa anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini kabisa, cha
kuburudisha, na chenye nguvu.
Na nimegundua kuwa wakati huo, huwa
tunapoteza kabisa hisia za muda na mambo mengine. Si kwamba tunakosa mpangilio;
la hasha! Mungu anakuwa anashughulika na muda wetu. Lakini inakuwa ni kama
unaachilia kila kitu, na unaunganishwa moja kwa moja na Mungu. Maombi yako
yanapopenya, kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia hapo; na mtu anayeomba
anaweza kuendelea kwa muda mrefu kama apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi.
Na mara anapomaliza kuomba, lile tundu
linabakia wazi.
Kijana huyu pia alisema kuwa, watu wa
namna hii wanapomaliza kuomba na kuondoka mahali hapo, lile tundu linakuwa
linaondoka pamoja nao. Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile blangeti la jiwe.
Wanakuwa wanaenenda chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema kwamba, katika hali
hiyo, ibilisi hawezi kufanya kile anachokitaka kwao. Na uwepo wa Mungu unakuwa
kama nguzo kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha yao. Wanalindwa; na kunakuwa
na nguvu kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi kwamba kadiri wanavyotembea huku
na kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata watu wengine. Nguzo hiyo inakuwa
inatambua kile ambacho adui amefanya kwa watu wengine. Na pale watakatifu hao
wanapozungumza na watu wengine, na wale watu wakawa wamesimama nao, wanaingia
ndani ya nguzo hiyo. Na mradi tu wakiwa ndani ya ile nguzo, vifungo vyote vya
adui vinadhoofika.
Kwa hiyo, watu hawa wenye mpenyo huu wa
kiroho wanapowashuhudia wenye dhambi habari za Yesu Kristo, upinzani wa wenye
dhambi unakuwa wa chini. Ni rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa Kristo. Wanapoomba
kwa ajili ya wagonjwa, au kwa ajili ya mambo mengine, maombi yao yanakuwa na
nguvu sana.
Na kama kuna sehemu ambako maombi ya
namna hii huombwa mara kwa mara, uwepo wa Mungu unakuja mahali pale na
hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama hizo,
ghafla vifungo vyao vinakatika.
Na kama atatokea mtu wa kusema nao kwa
uvumilivu na kwa upendo, wanaweza kugeuka haraka sana; si kwa nguvu au kwa
uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu, ambaye anakuwa yuko pale. Na kama hakuna mtu
atakayewajali watu hawa, wanakuja kwenye uwepo wake na kujisikia hatia,
wanaanza kujadili kama wakubali au la. Pale watakapoondoka, vifungo vinakuwa na
nguvu zaidi kwao. Na ibilisi anajihadi kwa kila njia kutowaruhusu kurudi tena
kwenye sehemu kama hizo.
Je, shetani anakaa kimya tu baada ya mtu kupata mpenyo?
Kijana huyu alisema kuwa, ibilisi
anawachukia sana watu wa namna hiyo, yaani wale waliopata mpenyo wa maombi.
Sasa unaweza kupiga picha, sote
tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia kijana huyu akieleza ushuhuda wake.
Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiyafanya na
aliyoyashuhudia kwa macho yake. Alitueleza kile ambacho walifanya kwa watu
ambao walipata mpenyo katika maombi. Alisema kuwa waliwaweka akilini sana watu
kama hao. Kisha waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu wao ili kuwajua vizuri.
Walitafuta kila kitu kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu wao wote, na ikitokea
mtu akawashinda kwenye maombi na kupenya, wanawasiliana na wengine kwenye
ulimwengu wa giza na kusema, "Mumlenge
mtu huyu kwenye eneo hili na hili. Udhaifu wake uko hapa na hapa."
Kwa kuwa mtu wa aina hii anapotoka nje
ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi inakuwa juu yake, uwepo wa Mungu upo juu
yake, roho yake inakuwa iko juu, na furaha ya Bwana ndiyo nguvu zake; anapokuwa
anaenda, adui anajaribu kila njia kuleta yale mambo ambayo yatamvuruga ili
asielekeze macho yake kwa Bwana.
Kama, kwa mfano, imeshajulikana kuwa
udhaifu wake uko kwenye eneo la hasira, basi adui atasababisha watu watende
mambo ambayo yatamfanya akasirike. Na kama hayuko makini kumsikiliza Roho
Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi ataondoa macho yake kwa Bwana. Na
anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu zinamjaa. Baadaye anapokuja kujirudi,
anakuwa anataka kutupilia mbali hali hiyo na kuendelea na furaha ya Bwana,
lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha kama mwanzo. Anajitahidi kujisikia
vizuri tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini? Alipojiachilia kwenye
kishawishi cha hasira, mapepo walifanya bidii zote katika muda huo kufunga lile
tundu kule juu. Na mara waliporudishia lile jiwe, uwepo wa Bwana unakuwa umekatika,
yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea mbinguni na kumfunika inakuwa haimfikii
tena!
Mtu huyo hataacha kuwa mwana wa Mungu.
Lakini ule upako wa ziada uliokuwa unaandamana naye maishani; ule uwepo
uliokuwa ukitenda mambo bila yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa umekatika!
Maana pepo wachafu wanatafuta uliko udhaifu wako.
Kama udhaifu wa mtu ni kwenye masuala
ya mapenzi, adui ataandaa watu, matukio, na mambo ambayo yatainua hisia za mtu
huyo za tamaa ya kimapenzi. Na kama mtu huyo atazikubalia hizo tamaa na
kufungua akili yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea nafsini mwake, pale
anapomaliza kila kitu na kutaka kurejea tena kwenye hali ya upako ili asonge
mbele, anakuta kwamba ule uwepo haupo tena. Labda unasema, “Hii si vizuri
kabisa.” Kumbuka tu Biblia inasemaje, " Tena ipokeeni chapeo ya wokovu. Vaeni dirii ya haki." Mara nyingi hatuoni haja ya silaha hizi za kivita. Lakini kumbuka
Yesu alivyotuambia juu ya namna ya kuomba "Usitutie majaribuni, lakini
utuokoe na yule mwovu."
Kila mara unapopata mpenyo katika
maombi, unapofika mwisho, kumbuka kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu aliye
dhaifu. Kumbuka kuwa haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana, useme, "Bwana,
nimefurahia wasaa huu wa maombi, lakini nitakapotoka nje kwenye dunia,
usiniongoze kwenye majaribu. Usiruhusu niangukie kwenye mtego wa ibilisi. Najua
kuwa adui anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego ya namna gani. Na ninajua
kuwa bado mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo. Kama nikiingia kwenye hali
fulani fulani, nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona ninaelekea kule ambako
kuna mitego niliyotegewa, nifanye nielekee upande mwingine. Uingilie kati, Ee,
Bwana. Usiche niende tu kwa nguvu zangu na uwezo wangu. Niokoe na yule mwovu.”
Mungu anaweza kufanya hivyo. Lakini,
kama kuna kitu kibaya kitatokea, ambacho kitakufanya uondoe macho yako kwa
Kristo, wewe sema tu, “Asante Yesu.” Ndiyo sababu Mtume Paulo aliandika,
“Mshukuruni Mungu kwa kila jambo.” Baadhi ya mambo si mazuri. Yanaumiza, na
tunashangaa kwa nini Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini kama tu tungejua kwa
njia hiyo anatuokoa na mambo yapi,
tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini Bwana, tutamshukuru kwa kila jambo.
Yule kijana aliendelea kusema kuwa,
unapopata mpenyo katika maombi, majibu yako ni lazima yatakuja. Alisema kuwa jibu mara zote huja, lakini mara
nyingi, huwa halifiki kwa mtu aliyeliomba. Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano
yaliyoko kwenye anga. Pia, majibu yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu wa
rohoni watafanikiwa kurejesha ule mwamba na kuziba tundu ambalo mwombaji
alifanikiwa kulitoboa kwa njia ya maombi yake.
Kisha aliongea jambo ambalo kwa kweli
lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi niingie kwenye mfungo wa siku kumi,
ili kumwuliza Bwana kama hilo alilosema lilikuwa na ukweli wowote. Basi
sikiliza haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila Mkristo anaye malaika ambaye
anamtumikia Mkristo huyo. Nasi tunafahamu kuwa Biblia inasema kuwa malaika ni
roho wanaotutumikia. (Waebrania 1:14). Alisema kuwa watu wanapoomba,
majibu huletwa kwa mikono ya malaika. Malaika huleta majibu, kama ambavyo
tunasoma kwenye kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo ambalo ni gumu sana.
Alisema kwamba, kama yule anayeomba anafahamu silaha za kiroho na amejivika
silaha hizo, majibu nayo huja kwa kupitia malaika ambaye, naye amejivika
kikamilifu kwa silaha hizohizo.
Lakini, kama anayeomba hajali silaha za
kiroho, basi malaika nao wanakuja bila silaha hizo. Wakristo ambao hawajali
kile ambacho kinaingia mawazoni mwao; hawashindani kuangusha mawazo yasiyofaa;
malaika wao huja bila chapeo. Silaha zozote utakazoacha kuzitilia maanani
duniani, malaika anayekutumikia naye anakuwa hanazo. Kwa maneno mengine, silaha
zetu za kiroho hazitulindi miili yetu, bali zinalinda vitu vile vya kiroho
tunavyofanikiwa kuvipata kutoka kwa Bwana.
Malaika anapokuwa anakuja, mapepo
wanamtazama na kumkagua na kubaini maeneo ambayo hajajifunika; na hayo ndiyo
maeneo ambayo watashambulia. Kama hana chapeo kichwani, basi watashambulia
kichwani. Kama hana dirii, watashambulia kifuani. Kama hana viatu, watajaribu
kutengeneza moto ili kumwunguza miguuni.
Sasa, najua kuwa hili ni gumu kuamini;
mimi narudia tu kile ambacho kijana huyu alisema. Kisha tulimwuliza, “Je,
malaika wanaweza kuungua moto?” Na unajua alisema nini? Kumbuka kuwa huu ni
ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho zinapambana. Mapambano ni makali sana,
na pale wanapomshinda malaika wa Mungu, jambo la kwanza wanalokimbilia ni lile
jibu alilobeba; na wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa ni zawadi ambazo
hutolewa kwa watu kupitia imani za siri, au uchawi.
Kumbuka kile ambacho Biblia inasema
kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote vyema hutoka kwa Mungu (Yakobo 1:17).
Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu vizuri anavyowapatia watu? Baadhi ya watu
ambao hawawezi kupata watoto, huenda kwa wachawi na waabudu shetani, na
wanapata mimba! Mtoto anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni muumbaji? HAPANA!
Anaiba kutoka kwa watu ambao hawaombi maombi yao hadi mwisho.
Katika Biblia, Yesu alisema,
"Ombeni bila kukoma." Pia alisema, "atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? " Je, Yesu atakukuta bado unangojea? Au utakata tamaa na kumwacha
adui aibe kile ambacho umekuwa ukikiombea?
Na hawaridhiki tu na kuiba jibu la
maombi. Wanataka pia kumweka malaika kifungoni. Na wanaanza kupambana naye.
Wakati mwingine wanafanikiwa kumkamata na kumfunga malaika. Inapotokea hivyo,
Mkristo anakuwa kama chakula chao duniani. Wanaweza kumfanyia chochote maana
hana ulinzi tena kwenye ulimwengu wa roho.
Nilimwuliza kijana huyo, “Una maana
kuwa malaika anaweza kushikiliwa katika ulimwengu wa giza?” Sasa alikuwa
anaeleza uzoefu wake, na akasema, hawatamshikilia malaika kwa muda mrefu kwa
sababu ya Wakristo wengine ambao wanaomba mahali pengine. Jeshi la ziada
litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na kama yule Mkristo anayehusika hajaomba
hadi kwenye mpenyo, basi atabakia mateka. Ndipo shetani atatuma malaika wake na
malaika wa nuru kwa mtu huyu, na hapo
ndipo uongo na udanganyifu unapotokea; maono ya uongo na unabii wa uongo.
Uongozi wa uongo, na kufanya kila aina ya maamuzi mabaya. Na mara nyingi, mtu
wa namna hii anaweza kupata mashambulizi na vifungo vya kila aina.
Niliondoka kwenye kile chakula cha
jioni huku na mawazo mengi sana. Nikasema, “Bwana, sitaki hata kujaribu kuamini
jambo hili.” Linaondoa ujasiri na usalama wangu wote! Nilipoenda kumlingana
Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na Bwana alifanya mambo mawili. Kwanza, si tu
kwamba alithibitisha mambo hayo niliyoyasikia kutoka kwa yule kijana, bali pia
alifungua akili zangu zaidi ili kuona mambo mengine mengi zaidi ya yale ambayo
niliyasikia. Pili, aliniongoza kuona kile ambacho tunatakiwa kukifanya wakati
mambo haya yanapotokea ili tuweze kuwa washindi.
Alinipa mambo matatu:
Moja: namna ya kutumia silaha za vita vyetu vya kiroho. Biblia
inaziita silaha za Mungu. Si silaha zetu. Tunapozitumia, tunamruhusu Mungu
kupigana kwa niaba yetu.
Mbili: tambua uhusiano wa roho zinazotutumikia, yaani malaika,
na maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima kuwa makini sana na kile kinachotokea
mioyoni mwetu; kama mwongozo wa kile ambacho kinatakiwa kutokea rohoni kutuhusu
sisi.
Tatu: ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatakiwi kuja kama
mtumishi wetu, kututumikia na kutuletea vitu mbalimbali. Hakimbiikimbii kwa
Baba kumweleza kile ambacho tunataka. Hiyo ni kazi ya malaika. Lakini Yeye
husimama pamoja nasi. Anafanya nini? Anatuongoza, anatufundisha, anatutangulia,
anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na mambo haya yanapotokea kwenye ulimwengu wa
roho, anatuambia. Wakati mwingine anakuamsha usiku na kukwambia, “Omba.” Wewe
unasema, “Hapana! Muda wangu haujafika.” Na anasema, “Omba sasa!” Kwa nini
inakuwa hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila kinachoendelea kwenye ulimwengu
wa roho. Wakati mwingine anasema, “Kesho ni kufunga.” Wewe unasema, “Hapana,
nitaanza Jumatatu!”
Lakini kumbuka kuwa Yeye anaelewa kile
kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Ni lazima tujifunze kuwa makini na
Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye njia za haki. Wapendwa, tuishie hapa. Labda
wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo tunaweza kuomba hadi kupata mpenyo,
maana sasa tunajua mapambano yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na namna
tunavyoweza kudumu tukiwa na mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza hili,
linakuwa ni jambo la furaha sana. Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu, bali
ni vya Bwana! Haleluya!
Hebu tusimame. Mwangalie mwenzio
machoni na utafakari ni mara ngapi amekosa kile ambacho Mungu alikiandaa kwa
ajili yake. Lakini shikaneni mikono kama inawezekana; watu wawili au watatu,
kisha tu muambiane, “Hakuna haja ya kushindwa tena! Tunaweza kushinda! Iko
nguvu ya kutosha kushinda! Yesu tayari ameshafanya kazi yote.” Muombeane ninyi
kwa ninyi ili Bwana aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi kushindwa. Iko neema
ya kutosha; nguvu ya kutosha kuleta ushindi!
Asante Yesu.
**********************
Ndugu msomaji
wa blog hii, somo hili ambalo ni muhimu sana kwa kila mwanadamu na mwili wa
Kristo, nimeliweka pia kama E-Book, hivyo unaweza kulipakua na kulisoma tena na
tena; na pia kuwagawia wengine. Bofya HAPA.
Usikate
tamaa. Simama imara katika imani. Unaweza kushinda. Bwana si dhalimu;
anakupenda na amekuwa akijibu maombi yako siku zote. Je, Biblia si inasema kuwa
KILA aombaye hupokea? (Mathayo 7:8). Na kwamba Mungu si mwanadamu hata aseme
uongo (Hesabu 23:19).
Tumia mafunzo
haya kusonga mbele katika wokovu na imani yako. Bwana Yesu akubariki sana.
Post A Comment:
0 comments: