Na Peter Mabula.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibuni wote tujifunze Neno la MUNGU.
Siku moja nilikuwa ibadani Kanisa fulani na ibada ilipoisha tu Mchungaji alilitangazia Kanisa kwamba kutakuwa na semina ya wamama pekee yao na mabinti peke yao siku hiyo hiyo na Mchungaji akatangaza kwamba Mwalimu wa semina hiyo ni Mimi Peter Mabula.
Nilishtuka sana maana sikujiandaa kufundisha semina. Mchungaji akatangaza kwamba anatoa dakika 10 wamama na mabinti kupumzika nje ya Kanisa kisha watarudi ndani na semina itaanza. Niliwaza sana kwamba natakiwa kuandaa masomo mawili ndani ya dakika kumi ili somo moja kufundisha wamama peke yao, yaani wanawake walio katika ndoa, kisha niandae somo lingine la kufundisha mabinti yaani wanawake ambao hawajaolewa. Kipindi cha wamama nilitakiwa nifundishe dakika 25 kisha dakika 5 maswali na baada ya hapo nilitakiwa kufundisha mabinti dakika 25 kisha dakika 5. maswali.
Niliingia ofisini kwa Mchungaji kisha nikaomba kwa MUNGU juu ya nini cha kufundisha kwenye semina hiyo.
Kwangu Mimi andiko lisemalo "Uwe tayari wakati unaofaa na usiofaa" huwa nalizingatia sana. Niliogopa kutoa maoni yeyote wakati Mchungaji ameshatangaza tayari bila kunishirikisha.
Nilipokuwa Naomba juu ya nini cha kuwafundisha wamama nilisikia sauti rohoni ikisema "WAFUNDISHE WANAWAKE WALIOOLEWA KUWASTAHI WAUME ZAO"
Nilianza kuandika haraka haraka nikianza na maana ya KUSTAHI.
Sikuambii nilipewa ujumbe gani kwa ajili ya mabinti hadi nitakapofundisha juu ta ujumbe huo.
Sasa baada ya utangulizi huo naomba sasa ndugu uzingatie neno hili wewe unayejifunza ujumbe huu, kwa ajili tu ya afya safi ya ndoa yako.
Waefeso 5:33 "Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose KUMSTAHI mumewe."


Wala Mke asikose kumstahi mumewe, yaani wewe mwanamke uliye katika ndoa hakikisha siku zote unamstahi mume mwema wako.

Nini maana ya kustahi?
Neno kustahi lina maana mbili.
1. Maana ya kwanza ya kustahi ni kuwa na heshima.
Hivyo usimkosee heshima mumeo.
Mke inampasa sana kumheshimu mumewe.
Mume ndio kichwa cha familia yaani Mume ndio kiongozi mkuu wa familia, hivyo apewe heshima yake.
Waefeso 5:23 "Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama KRISTO naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili." 
Mume ni kichwa cha mkewe, ni kichwa cha familia hivyo asipopewa heshima yake inaweza kuwa ndoa yenye tatizo.
Mume asipoheshimiwa na Mke hiyo ndoa haiwezi kuwa na afya njema Kamwe.
Kumheshimu Mume wako ni sehemu ya kumstahi.


2. Maana ya pili ya kumstahi mtu ni kuwa na adabu mbele zake.
Kumstahi Mume wako ni kuwa na adabu mbele zake.
Adabu yako kwa Mume wako itaifanya ndoa kuwa ndoa na sio ndoana.
Maana ya adabu ni tabia njema.

Mithali 11:16a"Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; "
Hakikisha sasa unamheshimu Mume wako huku ukiwa na staha mbele zake.

Staha ni nini?
Neno staha lina maana ya heshima inayoambatana na aibu au haya ya kutenda jambo baya mbele za watu.
Ukiona mwanamke hawezi kumstahi Mume wake ujue anakaribisha migogoro isiyoisha kwenye ndoa yake.
Ukiona mwanamke hana staha ujue huyo yuko kundi la wanawake wanaovunja ndoa zao kwa mikono yao wenyewe.
Mithali 14:1-2 " Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe. Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha BWANA; Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau."


Yeye aendaye kwa unyoofu ni yule tu anayemcha MUNGU.
Kwa kuzifuata Kanuni za MUNGU ambazo ni takatifu hakika utakuwa pia unajua kumstahi Mume wako.

Mambo Yale tu yaliyo machukizo ambayo ndiyo mambo yote ya kishetani, hayo ndio yakatae na yakemee.
Biblia inasema tusishirikiane na mambo ya Giza Bali tuyakemee.


Waefeso 5:11 "Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;"


Kataa mambo mabaya tu ambayo Mume wako anakushirikisha, hapo hutakuwa na hatia mbele za MUNGU.
Kataa dhambi tu, hapo kustahi kwako kutakuwa hakujaondoka.

Lakini kumstahi Mume wako ni agiza la Biblia kabisa hivyo mstahi mumeo huku ukikataa dhambi tu kutoka kwake.
Mke hakikisha unamstahi mume wako hata mbele za wazazi wako na mbele za ndugu zako wote.
Ukimdhalilisha Mume wako mbele ya ndugu zako ujue unaidhalilisha ndoa yako.
Mstahi Mume wako mbele za watu wote.
Sio unamkuta Mume wako anaongea na wanaume wenzake na wewe unaanza kumkaripia au kumuomba vitu ambavyo vitamfanya adhalilike, hapo utakuwa unaua ndoa na sio kuijenga.
Huwezi kumkuta Mume wako mbele za watu na wewe ukatoa shida yako huku watu wale wanasikia.
Inakupasa sana kumstahi Mume wako.
Ukiona mwanamke anaisaliti ndoa yake ujue huyo hana staha.
Ukiona mwanamke anamtangaza vibaya Mume wake kwa wanawake wenzake ujue huyo hana staha.
Wajulishe watumishi wa MUNGU tu au wazazi au watu sahihi katika ukoo ili kusaidia kuondoa tatizo la ndoa kiroho au kimwili kama lipo.
Biblia inamwagiza kila mwanamke aliye katika ndoa ahakikishe anamstahi Mume wake.
Hata wewe ambaye hujaolewa najua umejifunza ujumbe huu ili siku ukifunga ndoa ujue na hilo kwamba itakupasa sana kumstahi mumeo.
Hata wewe Mwanaume uliyejifunza somo hili unaweza kuwafundisha wengine ili wazingatie Neno la MUNGU linalowataka wanawake kuwastahi waume zao.
Leo nimezungumzia hilo tu hivyo wale ambao hulalamika kwamba "Mbona Mtumishi Mabula umezungumzia hicho tu" naomba watambue kwamba Leo ni zamu ya hicho, siku ikifika zamu ya kitu kingine hakika na hicho nitakufundisha.
Leo nasema hivi MWANAMKE MSTAHI MUME WAKO.
Kwa maana nyingine kinyume cha kustahi mumeo ni kumwaibisha, hivyo usimwaibishe. Maana nyingine ya kutokumstahi ni kumfanya awe hana thamani, hana msaada, ni mzigo tu, hajielewi, hana chochote, kumchafua mbele za watu n.k, ukifanya hayo ujue hujafuata agizo la Neno la MUNGU linalokutaka kumstahi mumeo.


Waefeso 5:22 " Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii BWANA wetu."

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Axact

Axact

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

Post A Comment:

1 comments: