Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na kisha tuombe maombi ya ushindi.
Nakumbuka kuna siku nilikufundisha somo lisemalo MAOMBI YA KUMUOMBEA MTU ALIYEBEBA KUSUDI LA MUNGU KWA AJILI YAKO na kuna watu  walinipa shuhuda juu ya somo hilo la maombi, Lakini namshukuru ROHO MTAKATIFU maana amenipa somo lingine la maombi kwa ajili yako ndugu, somo hili ni tofauti na somo la kwanza, hili linasema MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUINULIE WATU ILI KUFANIKISHA KUSUDI LA MAFANIKIO. Kuna tofauti kati ya kuomba MUNGU akuinulie watu na kumuomba MUNGU awafanye kutimiza lengo wale walioinuliwa tayari kwa ajili yako. Nimeaanza hivyo ili usidhani ni somo moja, Sasa tunaendelea.
Jambo la kwanza kabisa nataka ujue katika somo hili ni kwamba usimtegemee mwanadamu wa aina yeyote kukuinua bali mtegemee MUNGU anayeweza kukuinulia watu ili ufanikiwe.
Kumbuka kuwatumainia wanadamu ni kosa mbele za MUNGU maana tendo la kuwategemea wanadamu huleta laana.
Yeremia 17:5 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.''

 Baada ya kukujenga katika hilo sasa naomba ujue kwamba MUNGU anao uwezo wa kukuinulia watu ili tu wewe ushinde au ufanikiwe.
Iko mifano mingi kwenye Biblia ya jinsi ambavyo MUNGU aliwainuliwa watu kundi lake ili washinde au wafanikiwe.
Acha tuone mifano hii.
1. MUNGU aliwainuliwa waisraeli Musa ili MUNGU awatoe Misri hao waisraeli kupitia huyo Musa.
Waisraeli kama ilivyo kwako leo walikuwa katika wakati mgumu sana lakini Baada ya maombi Biblia inasema hivi. 
Kutoka 2:23''Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa MUNGU kwa sababu ya ule utumwa.'
 Baada ya maombi yao kufika kwa MUNGU Biblia inaendelea kusema '' Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. - Kutoka 3:9-10 ''
 MUNGU aliwainulia Waisraeli Musa ili kuwatoa Misri.
Hata wewe kwa maombi yako ya kumwambia MUNGU akuinulie watu anaweza kukuinulia watu wa kukutetea katika ukoo wako unaokukataa, anaweza kukuinulia watu ili uajiriwe serikalini,hakikisha Ttu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai, anaweza kukuinuliwa watu ili kukuombea, anaweza kukuinuliwa watu ili wawapige maadui zako na wewe ushinde vita ya kiroho.
Inawezekana kuna jambo gumu sana kila ukijaribu unashindwa, leo mwambie MUNGU akuinulie watu wa kufanikisha jambo hilo.

2. Yoshua alipewa na MUNGU jukumu la kuwarithisha waisraeli maeneo.
Yoshua 1:16 '' Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. '
 Inawezekana kuna haki yako fulani unatakiwa uipate, umezungushwa sana na kuonewa kwa sababu walio katika maamuzi ya kukupatia haki yako sio watu wazuri, leo omba MUNGU akuinulie watu katika nafasi hiyo ili wewe ufanikiwe.
Inawezekana unashindana mahakamani  au kwenye mabalaza na mtu mwenye nguvu au tajiri, inawezekana ana ushawishi mkubwa kiasi kwamba hakuna anayekujali wewe wala kukusikiliza, leo muombe Bwana YESU akuinulie watu katika nafasi ya maamuzi ili ufanikiwe, hakikisha tu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Unaweza ukashangaa meneja au mkurugenzi au mkuu wako aliyekuwa anakuonea sana, baada ya maombi akapata uhamisho wa ghafla kumbe analipisha kusudi la MUNGU la kufanikiwa kwako, maana atakayechukua nafasi yake atakuthamini wewe na atakuwa mtu wa haki hivyo haki yako utaipata kirahisi sana.

3. Othnieli aliinuliwa na MUNGU kwa ajili ya kuwasaidia waisraeli dhidi ya maadui zao wenye nguvu.
Waamuzi 3:9-10 '' Kisha wana wa Israeli walipomlingana BWANA, BWANA akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. ROHO  ya BWANA ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye BWANA akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.''
 Biblia inasema walipomlingana MUNGU yaani walipotoa haja za mioyo yao kwa MUNGU yeye MUNGU aliwainulia Mtu na mtu huyo akawa chanzo cha ushindi wao dhidi ya maadui kwa miaka 40.
Unaweza ukamuomba MUNGU akuinulie watumishi wake ambao watakapokuombea majini waliokutesa watakuachia tangu dakika hiyo hadi uzeeni mwako, hakikisha tu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Inawezekana mtaani kwenu kumejaa ushirikina na uko hatarini kwa sababu wachawi wanakuwinda ili wakumalize, unaweza ukaomba MUNGU akuinuliwe watu na ukashangaa MUNGU akainua waombaji au MUNGU akamtuma mtumishi wake kufungua kanisa mtaani hapo na utashangaa wachawi wote wanatoroka mji maana nguvu ya MUNGU itawapiga na hawatakaa tena eneo hilo, kuna jinsi nyingi sana MUNGU anaweza akakuinulia watu ili wewe uwashinde madui zako. Unaweza ukashangaa sana yule aliyekuwa anakutisha na kukukosesha amani mara unamuona Polisi wamemkamata kwa makosa yake lakini hali hiyo ikawa na manufaa kwako maana hatakutisha tena, yaani hapo MUNGU anakuwa amekuinuliwa vyombo vya sheria ili tu wewe usiteseke tena, kuna njia nyingi mno.

MUNGU aliwainulia Daudi ili awe mfalme badala ya Sauli aliyewataabisha. Unajifunza nini?
Kuna watu wakikaaa tu kwenye ofisi fulani utasikia ajira zinatangazwa na wewe unapata kazi, hakikisha tu unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kuna watu MUNGU anaweza kuwainua na wamebeba kusudi lake kabisa la kufanikiwa kwako.

Kwanini MUNGU akuinulie watu?

1. Ili watimize kusudi la MUNGU la wakati huo kwako.
Wafilipi 2:13 '' Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.''
Inawezekana kabisa umekosa mchumba lakini MUNGU anaweza kukuinulia mtu atakayeitimiza ahadi ya MUNGU kwako kwamba utafunga ndoa, mtu huyo atakupenda na kukuthamini hata kama wewe ngine wanakuona mbaya au wanakuona takataka, lakini aliyelibeba kusudi la MUNGU kwako atakuona unavaa sana  hata mpaka anaanza kujiuliza kwanini hakukufahamu mapema.
Inawezekana kusudi la MUNGU ni wewe ukue kiroho hivyo MUNGU anaweza kukuinulia mtumishi ili kukusaidia katika jambo hilo na hapo atakuwa analitimiza kusudi la MUNGU.
Mimi Mabula sitasahau mwaka 2012 ambapo MUNGU aliwainua watu wawili wakafunga siku 5 kila mmoja  ili kuniombea, mmoja alikuwa Mwanza na mwingine Dar es salaam, watu hawa wala hawakujuana na hata hawakujua niko katika hali gani lakini ROHO wa MUNGU aliwaonyesha hatari iliyokuwa inaniandama hivyo wakajikuta wanafunga na kuomba kwa siku 5 kuniombea mimi, hao walikuwa wanalitimiza kusudi la MUNGU. MUNGU ana njia nyingi sana za kuwafanya watu walitimize kusudi lake kwako. Sitasahau siku moja Mwanamke mmoja ambaye hatujawahi kuonana ila huwa ananifuatilia tu mtandaoni akijifunza masomo yangu, siku moja alinitumia Tsh 50,000 na nilisita kuitumia maana maana niliogopa lakini nilipokuja kumuuliza aliniambia jambo la ajabu sana, alisema kwamba aliambiwa rohoni na akakoseshwa amani hadi aliponitumia ndipo akawa na amani na MUNGU akasema na yeye kitu. Nilishangaa sana hata nikakosa majibu  ya kumweleza, ila wakati pesa hiyo inatumwa nilikuwa katika wakati mgumu sana sana lakini MUNGU akamwinua ili kunisaidia, hivyo ndivyo MUNGU anaweza kuinua watu kwa ajili yako. Hata siku nyingine tena kuna mtu alinitumia kiasi fulani cha pesa na nilipoongea naye kwenye simu niliishia tu kumwambia kwamba '' Hakika Wewe una ROHO wa MUNGU'' Maana ni kama MUNGU aliona nini kinaendelea kwangu hivyo akaniinuliwa watu kunisaidia.

2. Ili wakuletee jibu la MUNGU la maombi yako.
Isaya 38:14-15 '' Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.''
Tunafahamu habari hii vyema sana kwamba Hezekia alikuwa anaumwa sana na aliambiwa atakufa muda mfupi baadae. Yeye baada ya kuambiwa hivyo aliamua kugeukia ukutani na kuomba mbele za MUNGU na MUNGU akamuinulia Isaya Nabii kumletea majibu ya maombi yake kwamba atapona na kuongezewa miaka ya kuishi.
MUNGU anaweza akamwinua mtu kukuletea majibu ya maombi yako ambayo umeomba muda mrefu.
Sitasahau siku za karibuni nilikuwa nawaombea watu kwa simu, siku hiyo nilikuwa naombea watu zaidi ya 20. Wakati namuombea mtu wa kwanza nilisikia sauti ikisema ''Waambie wote utakaowaombea leo kwamba MUNGU anaenda kutenda jambo jipya la muujiza'' Kisha nikapewa andiko la Zaburi 35:8 ili kuwaombea dhidi ya maadui zao. Niliwaombea nikiwambia kwamba MUNGU anaenda kutenda jambo jipya baada ya maombi  nikalala na nilipoamka asubuhi nilikuta meseji za watu watatu katika lile kundi ambalo niliwaombea wakisema kwamba hakika MUNGU amefanya jambo jipya, kila mtu akanipa ushuhuda wake. Hapo ndipo nikaelewa kwanini MUNGU alisema atatenda jambo jipya. Ndugu unaweza kumuomba MUNGU akuinulie watu na akawainua wa kukuletea majibu yako kutoka kwa MUNGU na ukashinda vita ya kiroho uliyokuwa unapitia.

 3. Ili wewe umtukuze MUNGU kwa  kukujibu mahitaji yako kwa njia hiyo.
2 Wafalme 5:14-15  ''Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa MUNGU; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa MUNGU, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna MUNGU duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.''
 Inawezekana walikuwepo watumishi wa MUNGU wengi tu waliomuombea Naamani ili apone ukoma lakini hakupona, lakini siku moja MUNGU akamuinulia Elisha na Elisha akampa Naamani Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU uliopelekea Naamani kupona ukoma uliomtesa miaka mingi.
Naamani baada ya kumponywa alisema Neno hili  ''Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna MUNGU duniani mwote, ila katika Israeli ''
Naamani alimtukuza MUNGU aliye hai kwa sababu alitendewa ,uujiza wake baada ya kukutana na watu walioinuliwa na MUNGU kwa ajili yake.
Hata wewe inawezekana una mateso sugu sana, inawezekana unanyanyaswa sana, inawezekana unataka kufukuzwa hata katika nyumba uliyoijenga mwenyewe. Ndugu Unaweza kuomba maombi ya kumuomba MUNGU akuinuliwe watu wa kukusaidia na ukashangaa MUNGU anakuletea watu ambao wataguswa na matatizo yako na kukusaidia kiajabu sana.

4. Ili MUNGU aweke nguvu zake ndani yao kwa lengo la kukusaidia wewe.
Waamuzi 2:18 '' Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.'
MUNGU anaweza akaweka nguvu zake ndani ya watu fulani ili kuwasaidia watu wengine.
Inawezekana una maadui wengi mno kazini kwako, lakini MUNGU anaweza kukuinulia marafiki wenye nguvu sana kiasi kwamba maadui zako watajikuta wanakukimbia na kukuogopa.
MUNGU anaweza kukuinulia mtumishi Mwaminifu wa KRISTO ambaye atakuombea na utashinda kila kikwazo cha kipepo. 
MUNGU anaweza akakuinulia mtu wa kukusaidia na ndani ya Mtu huyo MUNGU akaweka nguvu za kumfanya mtu huyo kukusaidia na kukuletea ushindi.
Ndugu muombe MUNGU akuinuliwe watu.

 MUNGU Baba anaweza kukuinuliwa watu wa kukusaidia katika kila eneo la maisha yako au kila eneo la hatua zako za ushindi, ili wewe umtukuze MUNGU.
Mama mmoja mjane alikuwa anateswa na madeni ya mume wake marehemu na hadi watoto wake wanataka kuchukuliwa ili kufidia Madeni hayo. Siku moja mama yule akamwendea Elisha aliyekuwa ameinuliwa na MUNGU kwa ajili ya mama yule. Elisha alimuomba MUNGU na MUNGU akatenda muujiza na madeni yakaisha tangu siku hiyo kwa yule mama, Hiyo iko 2 Wafalme 4:1-7.
Hata wewe inawezekana uko katika tatizo la muda mrefu na gumu sana kwako lakini MUNGU anaweza akakuinulia mtu wa kuliondoa tatizo hilo kwa dakika 5 tu, ndugu leo omba MUNGU akuinulie watu ili kufanikisha kusudi la maendeleo.

 MUNGU aliwainulia Ayubu akina Elifazim Mtemani na marafiki zake wawili ili huyo Ayubu aliyeinuliwa kwa ajili yao awaombee msamaha kwa MUNGU ndipo watasamehewa. Hiyo iko Ayubu 42:7-8 '' ''
Hata wewe unaweza ukainuliwa watu wa kukuombea, kukupatia kazi, kuombea huduma yako au biashara yako n.k
 Samweli aliwaombea Israeli, Musa aliwaombea Israeli  ili wasiteketezwe, hata wewe wanaweza wakainuliwa watu kukuombea ili ufanikiwe.
 MUNGU alimwinulia Eliya mama mjane ili amlishe chakula.
1 Wafalme 17:8-9 ''Neno la BWANA likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.'
 Hata wewe MUNGU anaweza kukuinulia watu kukuhudumia katika wakati mgumu.
 MUNGU alimuinulia mama Mshunemu nabii Elisha ili Mtumishi huyo wa MUNGU aombe na mama yule apate uzao na akapata, hiyo iko 2 Wafalme   4:16-17.

 Hata wewe katika vifungo , katika jaribu, katika uonevu wa nguvu za giza, katika kuteswa na madhabahu za giza n.k MUNGU anaweza kukuinuliwa watu na kupelekea ushindi kwako, mtukuze tu MUNGU baada ya muujiza wako na hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.

Maombi ya leo.
1. Omba MUNGU akuinulie watu katika kila eneo la maisha yako.
2. Omba MUNGU watu hao wakae katika nafasi zao sawasawa na kusudi la MUNGU.
3. omba kwa MUNGU kwamba upate neema na kibali mbele ya watu hao.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni 
MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUINULIE WATU ILI KUFANIKISHA KUSUDI LA MAFANIKIO.   Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 


MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUINULIE WATU ILI KUFANIKISHA KUSUDI LA MAFANIKIO.



 Ninakushuru MUNGU Baba kwa kuwa wewe u mwema, na kwa maana fadhili zako ni za milele.
Niko hapa BWANA naomba usisamehe dhambi zangu zote na uovu wangu wote. Neno lako linasema Katika 1 Yohana 1:8-9kwamba ''Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.'' Eee MUNGU wangu katika jina la YESU KRISTO  naomba unisamehe tu BWANA, nisamehe kwa makosa yangu yaliyosababisha nikawa kinyume na kusudi lako, nisamehe BWANA kwa makosa ya wazazi wangu na mababu zangu yaliyosababisha mimi niwe katika agano la urithi la uovu, naomba unitakase na damu ya YESU KRISTO initenge mbali na hilo agano la urithi la kipepo. Nakuomba nipe nguvu za kushinda dhambi, makosa na uovu na kuanzia leo nitakuwa Mteule wako ninayeishi maisha safi ya Wokovu wako Bwana YESU mwokozi wangu.
Niko BWANA mahali hapa nikiomba juu ya watu utakaowatumia ili kufanikisha kusudi la maendeleo na mafanikio kwangu.
Eee MUNGU Baba nakuomba niinulie watu ambao watafanikisha kufanikiwav kwangu kiroho na kimwli.
Katika kutaka kazi nahitaji BWANA uniinulie watu wa kuniajiri na kunilipa mshahara mzuri.
Katika kupona kwangu nahitaji watu BWANA wa kutimiza kusudi lako la uponyaji kwangu.
Eee MUNGU Baba ahadi yako katika Neno lako Yeremia 33:6inasema kwamba utaniponya na kunipa afya njema, Eee Bwana YESU nakuomba uniponya na mahali ambapo panahitaji kuniinulia watu Eee BWANA nakuomba uniinulie watu ili nitoke katika vifungo vyote vya giza.
Eee MUNGU Baba ahadi yako katika Mwanzo 2:24 ni kwamba mimi nifunge ndoa takatifu mbele zako, Eee MUNGU wangu nakuomba niinulie uliyemkusudia ili awe mwenzi wangu wa ndoa, mwinue wakati huu ili kunitimiza kusudi lako la mimi kuwa katika ndoa takatifu niliyofunga Kanisani mbele za watumishi wako.
 Eee MUNGU Baba ahadi yako katika Neno lako Waebrania 1:14 ni kwamba Malaika zako watanihudumia kwa sababu mimi ni mteule wa KRISTO, Eee BWANA nakuomba niinulie malaika ambao watanihudumia na Malaika ambao watalinda na kuniokoa kama ahadi yako inavyosema katika Zaburi 91:11
Katika kazi Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu.
Katika safari na katika Biashara  Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu, niinulie wateja na watetezi wa ajira yangu.
Katika kesi mahakamani inayonikabili na katika wadeni wangu, Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu.
 Katika kila baraka yangu ambayo inazuiliwa kipepo, Eee JEHOVAH MUNGU wangu niinulie watu uliowakusudia wa kufanikisha kusudi la maendeleo yangu.
Sasa katika jina la YESU KRISTO ninaomba kila aliyeinuliwa na MUNGU ili kunisaidia namuombea kwa MUNGU kwamba akae katika nafasi yake itakayoleta ushindi wangu.
Nawafukuza wote waliokalia nafasi kiuongozi za kunididimiza mimi na kunifanya nisifanikiwe katika kazi yangu.
Naamuru kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO Mwokozi kwamba viongozi wakuu wawatoe au kuwahamisha wale wote walioshikilia nafasi na kunionea au kunididimiza, na sasa namuru yule ambaye ni kusudi la MUNGU ili mimi nifanikiwe huyo ndiye akae katika nafasi yake iliyo na kusudi la MUNGU ili kunisaidia mimi.
Eee MUNGU Baba ninaomba kwa rehema zako na neema mimi nipate kibali na neema mbele ya wote uliowainua ili wanisaidie.
Neno lako linasema kwamba '' Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.-Mwanzo 39:21'' Eee MUNGU uliyekuwa pamoja na Yusufu, Ukampa Yusufu kibali mbele za wanadamu na pia ukamfadhili, nami naomba Eee YAHWEH MUNGU wa uzima uwe nami, unipe kibali na Neema mbele ya kila uliyemwinua kwa ajili yangu ili kufanikiwa, Eee MUNGU wangu, na iwe hivyo kwangu katika jina la YESU KRISTO.
Eee MUNGU Neno lako katika Esta 2:17 Linasema kwamba ulimpa Esta Neema mbele ya Mfalme na tena ukampa Esta kibali cha kipekee mbele ya macho ya mfalme, Eee MUNGU ninaomba unipe neema na kibali mbele za mwenzi wangu, mchumba wangu aliye kusudi lako, nipe neema na kibali mbele ya wazazi wangu na wafanya kazi wenzangu wote, nipe neema na kibali mbele ya ndugu zangu na wakuu wangu wa kazi na kila aliyeinuliwa na wewe kwa ajili ya kunifanikisha, nakuomba Eee BWANA nipe neema na kibali mbele zake na sasa kusudi lako litimie. Mimi naamini hakika imekuwa katika jina la YESU KRISTO.
Mimi naamini kabisa kwamba imekuwa sawasawa na nilivyoomba.
Katika jina la YESU KRISTO mwokozi aliye hai nimeomba na sasa ninashukuru.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
+255714252292.
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Axact

Axact

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

Post A Comment:

4 comments:

  1. Mimi ni muumini wa kanisa katoliki tangu kuzaliwa mpaka sasa na miaka 47 kiufupi kwetukra kikazi nina miaka 16 nikiwa kama mtumishi wa serikali nilianza kazi mwaka 2003 ambapo mwaka 2005 nilipata mwenza wa maisha na mungu akatubariki mwaka 2006 tuka mtoto wa kike lakini yule mwenza hatukuweza kudumu kufunga pingu za maisha akaondoka niliendelea kuishi mwenyewe ktk nyumba yangu niliyojenga kwa miaka 3 mwaka 2009 mungu akanipa mwenza mwingine na akatubariki mwaka 2010 tukapata mtoto wa kiume na mwaka 2011Tukafunga ndoa takatifu kanisani mwaka 2012 mungu akatujalia tena mtoto wa kike mwaka huo huo nikapata uhamisho kwenda mkoa mwingine tena kagera kwa mke wangi mpenzi alikuwa na mtoto mchanga tena alijifungua kwa operation nilimuomba niende nikaripoti ofisi mpya na baadae nikipata nyumba nirudi kuchukua familia sikuwa na wasiwasi kwa vile niliwaacha ktk nyumba yangu na pesa nikamuchia nakumuahidi kuwaendelea kuwatumia matumizi kwa mpesa niliondoka nikafika ils nikakuta ni mbali unasifiri siku 3 na maisha kile yakawa ni magumu sana ila nikipata pesa natuma baadae akapata washauri wabaya wakamuambia mumeo kaenda kagera lazima huko kaoa mhaya au mnyarwanda ibilisi akamuingia akarubuniwa na mume wa mtu akampa ujauzito akaogopa akafunga nyumba self akapeleka wale wanangu kwa wazazi wake akaenda kijificha mji mwingine ambapo yule hawara alimpangia chumba kimoja yy akavinja ndoa yake mwenyewe mpaka sasa ni miaka saba yupo na mtoto wake japo wanangu ni wakubwa na watunza jambo lilinifanya nikapata ugonjwa wa presha na stress nikawa mlevi wa kupindukia jambo hili linanitatiza mno nafanya kazi nyeti ola siishi na familia na siwezi oa mke mwingine nokavunja kile kiapo cha ndoa cha katika shida na raha hadi kifo japo na mimi ibilisi aliniingilia nakazaa mtoto bahati mbaya baada ya mke kuvinja kiapo cha natunza mke ila mwanamke siishi sasa mkuu wangu wa kazi ananinyanyapaa kuwa nina afya mgogoro kunishitakia kwa wakubwa pengine nifukuzwe kazi japo akijua hakuna mkamilifu duniani na hkuna anayeomba kuumwa au kifo baada ya kusoma ile makala yako mtumishi mabula roho wa mungi akaniongoza kwa vile maombi sijui kuomba vizuri naweza pata muombezi kupitia makals hii nikanusuru kazi na ndoa na pepo la ulevi ns kutumia pesa bols mpangilio na pepo la uzinzi linitoke nakushukuru sana pia nitaendelea kufuatilia blog yako namba yangu ya simu ni 0755042669 email yangu ni kama onavyo ktk google mara coments itakapo deliver kwako nakuombea roho mtakatifu azidi kukufunulia siri za ufalme wa mbonguni ili maana Bwana Yesu karibu anarudi kuchikua kanisa lake nami na familia yangu tunyakuliwe tusijebaki wana wa ibilisi amen

    JibuFuta
  2. Mtu wa Mungu, kwa hakika nikupe pole sana ila naamini umefika sehemu sahihi sana utapata huduma ya Maombi, ushauri na naamini Mungu aliye ziumba mbinu na Nchi atakubadilisha utakuwa kama ulivyo. Nitakupigia Simu na Kukupa maelekezo zaidi

    JibuFuta
  3. Asante mtumishi wa Mungu kila ninaposali kupitia maombi yako nafarijika Sana na muda mwingine najikuta ktk maombi naomba utafikiria ulijua ndio nayahitaji Asante barikiwa sana🙏

    JibuFuta
  4. Ubarikiwe mtumishi wa mungu

    JibuFuta