Na Askofu Mkuu Zakaria Kakobe. |
Biblia
inasema kwamba, siku hizi za mwisho, kutakuwako nyakati za hatari.
Wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo na
mafundisho yaliyo kinyume na kweli [2 TIMOTHEO 3:1; 1 TIMOTHEO 4:1].
Siku hizi tulizo nazo tunazungukwa na “WANAFUNZI WA MUSA” [YOHANA
8:28-29],
ambao kwa kutaka kuwawekea watu msisitizo mkubwa wa kuabudu Jumamosi na
kushika Sabato; wanafundisha kwamba watu wote wanaoabudu Jumapili
wamepotea, na tena wana alama ya mnyama “666”. Wanafundisha kwamba
kuiacha Sabato na kuabudu Jumapili kulianzishwa na Costantine pamoja na
Kanisa Katoliki. Ni muhimu basi kama wanafunzi wa Yesu, kujifunza yote
kuhusu jambo hili, ili tuweze kuishindania imani tuliyokabidhiwa
watakatifu MARA MOJA TU [YUDA 1:3]. Tutaligawa somo hili katika
vipengele vitano:-
( 1 ). UTANGULIZI KUHUSU SABATO.
( 2 ). KUKOMESHWA KWA SABATO.
( 3 ). SABATO, KIVULI CHA YESU KRISTO
( 4 ). SABABU ZA WAKRISTO KUABUDU JUMAPILI
( 5 ). KUSHIKA SIKU, SIYO NJIA YA KUOKOKA.
1) UTANGULIZI KUHUSU SABATO
1. MAANA YA NENO SABATO.
Neno
“Sabato”, linatokana na neno la Kiebrania, “SHABBATH” ambalo maana yake
ni PUMZIKO au KUSTAREHE NA KUACHA KAZI.
Pumziko hili siyo lazima liwe siku ya saba. Katika mazingira fulani
watu waliagizwa kuwa na Sabato siku ya Kwanza na siku ya nane [MAMBO YA
WALAWI 23:39], na pia walikuwa na Sabato siku ya saba kila wiki [KUTOKA
20:8-11].
Kulikuwa pia na Sabato ya mwaka mzima wa saba kwa ajili ya nchi.
Haikuruhusiwa kulima nchi mwaka huo, ilitakiwa nchi istarehe au ipumzike
[MAMBO YA WALAWI 25:2-5].Awaye yote ambaye anadai leo kwamba
anazingatia sheria kwa kushika sabato, imempasa kutokulima au kuvuna
kila mwaka wa saba , au sivyo amekosa juu ya yote[YAKOBO 2:10]
2. MWANZO MWA AGIZO LA KUSHIKA SABATO NA MAKUSUDI YAKE.
Agizo la kwanza kwa watu kuishika Sabato, lilitolewa na Mungu kwa Wanaisraeli,kwa mkono wa Musa,katika AGANO LA KALE.Agizo
hili halikutolewa kwa Adam, Nuhu, Ibrahim,Isaka,Yakobo na Wengine kabla
ya Musa[KUMBUKUMBU 5:1-3,12-14].Agizo hili pia, lilikuwa kwa TAIFA la
Wanaisraeli tu! Siyo mataifa mengine ambayo hayakupewa sheria [WARUMI
2:14;KUMBUKUMBU 4:7-10].WANAISRAELI waliagizwa kushika sabato kwa
makusudi yafuatayo:- ( a ). Ili
wapate kukumbuka jinsi walivyokuwa watumwa katika nchi ya Misri na ya
kuwa BWANA Mungu aliwatoa utumwani na kuwapa PUMZIKO kutoka katika kazi
hizo za utumwa [KUMBUKUMBU 5:15].
( b ).
Ili ipate kuwa ISHARA ya Agano lao na Mungu, Agano la kale
[KUTOKA31:12-13,16-17;EZEKIELI20:20].Agano hili linatajwa kuwa ni la
“MILELE” siyo kwa maana kwamba lisilo na mwisho.Siyo
kila mahali katika Biblia “MILELE” ilipotumika, ina maana isiyo na
mwisho. AGANO LA MILELE hapa lina maana Agano la muda mrefu sana
ujao.[mifano:Nyumba ys kukaa itakayothibitishwa “milele”[WALAWI
25:29-30];Mtu, kuwa mtumishi wa mtu “milele”[KUMBUKUMBU 15:12-17];Ukoma
wa “milele”[2WAFALME5:25-27].
3. HUDUMA YA MAUTI ILIYOAMATANANA KUTOKUISHIKA SABATO.
Agizo la
kushika sabato,lilikuwa ni KONGWA zito.Mtu ambaye hakuishika sabato,
alipewa huduma ya mauti, ALIUAWA{KUTOKA31:14-15,35:2-3}.Hata mama
aliyejaribu kukusanya kuni ili kuwapikia chakula wanawe siku ya sabato
,alipigwa kwa mawe hata akafa [HESABU 15:32-36].Mtu
hakuruhusiwa kutembea kwa mwendo wa maili moja siku ya sabato. “Mwendo
wa sabato” ulioruhusiwa ili mtu asihesabike amefanya kazi, ilikuwa chini
kidogo ya maili MOJA kama mwendo wa kutoka Yerusaremu kwenda Mlima
Mizeituni [MATENDO1:12].Hata kujitwika godoro ilikuwa ni kuvunja sheria
ya kushika Sabato [YOHANA 5:8-10].Hata kuponya siku ya sabato ilikuwa ni
kuivunja sheria ya kushika Sabato[LUKA 13:14].Ilikuwa ni huduma ya
adhabu, huduma ya mauti! [2WAKORINTHO 3:7-9].Wanafunzi
wa Musa leo, wanaojidai kwamba wanashika sabato ,haiwapasi kwenda
hospitali siku ya sabato, wala kutafuta kuponywa kwa njia yoyote siku ya
sabato, tena miongoni mwao, asiyeishika sabato ,wanatakiwa wamwue!Mbona
hawayafanyi haya?
( 2 ). KUKOMESHWA KWA SABATO.
Mwanadamu hakuumbwa kwa ajili ya sabato, bali kwa ajili ya Mungu aliye BWANA wa Sabato au mwanzilishi wa Sabato.Mungu
ambaye ndiye aliyeleta agizo la kuishika Sabato, ana haki pia ya
kuikomesha au kuiondoa agizo hilo na hakuna mwenye haki ya kumlaumu
[MARKO 2:27-28].Mapema katika unabii, kabla ya kuja Yesu Kristo,
ilitabiriwa kwamba Mungu ataikomesha Sabato [HOSEA 2:11].Yesu
Kristo , alikuja kuitimiliza torati kwa kuikomesha Sabato. Kiongozi
wetu mkuu wa wokovu Yesu kristo ,kwa wazi kabisa, alishindana na kila
wazo la Wayahudi la kushika sabato. Alikuja kuikomesha Sabato kwa kuivunja.Ikiwa
Yesu ni Bwana wetu ,sisi nasi tutakuwa mstari wa mbele kwa kumfuata
yeye kama kielelezo na kuivunja Sabato [MARKO 2:23-28;LUKA
6:6-11;13:10-16;14:1-6;YOHANA 5:8,18; 9:13-16].Yesu Kristo
,aliigongomelea msalabani hati yakutushtaki kwa kutokuishika sabato,
akaiondoa ,isiwepo tena! [WAKOLOSAI 2:13-14].Kushika siku na miezi na
nyakati na miaka, ni kuyarejea MAFUNDISHO YALIYO MANYONGE YENYE UPUNGUFU
[WAGALATIA 4:9-11].Hatupaswi tena kuhukumiwa na mtu YEYOTE kwa sababu
ya SABATO![WAKOLOSAI 2:13-16]. Ili kupata tafsiri nzuri ya neno “Sabato”
katika andiko hilo, soma Biblia ya Kiingereza, ya tafsiri ya
King James Version inataja neon “SIKU ZA SABATO” au “SABBATH DAYS”.
Nanukuu ( COLOSIANS 2:16 ) “Let no man therefore judge you in meat, or
in drink, or in respect of an holyday, or of the new moon, or of the Sabbath days”.
Kwa hiyo, mtu awayeyote asituhukumu sisi kwa habari ya sabato za siku
au siku ya sabato. Amri ya nne ya sabato katika zile Amri kumi, haipo
katika Agano Jipya, Yesu wala mitume hawakutuagiza kushika
sabato[MATHAYO19:16-19;MATENDO 15:1-29].Kama
wakati uliokuwapo kabla ya Musa, sisi nasi kama uzao wa Ibrahimu kwa
imani, hatukuagizwa kushika sabato kama jinsi ambavyo hakuagizwa
Ibrahimu!Agizo Jipya, limekuwa badala ya Agano la Kale lenye upungufu
,lililokuwa na huduma ya adhabu au ya mauti.Huduma hiyo IMEBATILIWA
[2WAKORINTHO 3:6-11;WAEBRANIA8:6-9,13].
(3) SABATO , KIVULI CHA YESU KRISTO.
Sabato,
ilikuwa ni kivuli cha mambo yajayo [WAKOLOSAI 2:16-17].
Sabato, ilikuwa ni kivuli tu cha PUMZIKO ambalo wanadamu was umbukao na
kulemewa na mizigo wangelilipata kwa kumwendea, Yesu kristo [MATHAYO
11:28].
Baada ya kuja mwenyewe aliye PUMZIKO, Yesu kristo; hatuna haja tena ya
kushika kivuli. Tukimshika Yesu kristo , YEYE Pia, atatupa SABATO ya
milele huko mbinguni [WAEBRANIA 4:8-11].Sabato hii siyo ya Jumamosi
maana ni wale watakaofanya bidii kuingia raha hiyo na kuwa mbali na
kumwasi Yesu watakaoingia [WAEBRANIA 4:1-11;UFUNUO 14:13]
( 4 ). SABABU ZA WAKRISTO KUABUDU JUMAPILI
Hakuna andiko lolote katika agano jipya linalotupa kumbukumbu ya
kusanyiko la Wakristo siku ya Sabato kwa ajili ya kumuabudu Mungu.Neno “Sabato” linaonekana mara 60 katika Agano Jipya.Mara
50 katika hizo ,linatumika KABLA ya Agano Jipya lenyewe kufanywa kwa
damu ya Yesu.Katika mara kumi zilizosalia, mara sita(6) linazungumzia
Paulo akiwawahubiri WAYAHUDI kwenye makusanyiko YASIYO YA KIKRISTO
kwenye sabato zao za kiyahudi [MATENDO 13:14,42,44;17:1,2;18:4].Mara
mbili, neno hilo linaelezea juu ya sheria ya Musa isomwapo na Wayahudi
katika masinagogi[MATENDO 13:27;15:21];Mara moja inaeleza jinsi
tusivyopaswa kuhukumiwa katika Sabato [WAKOLOSAI 2:16];Mara moja
iliyosalia inataja juu ya mwendo wa sabato [MATENDO 1:12].Siku ya
JUMAPILI , ambayo ndiyo siku ya kwanza ya juma ,SIKU YA BWANA
aliyoshinda mauti na kufufuka [UFUNUO 1:10],Tunaitenga maalum kumwabudu
Bwana kwa sababu:-
( a ).
Ni sikukuu ya malimbuko ya mavuno ambayo ilifanywa katika Agano la
Kale,SIKU YA PILI baada ya Sabato;Ikiwa ni utabiri wa Kristo ambao ni
LIMBUKO lao waliolala [WALAWI23:9-14;1WAKORINTHO15:20].
( b ).
Ni siku ya ushindi ya Bwana wetu Yesu aliyofufuka, na kujidhihirisha
kwa wanafunzi wake baada ya kufufuka kwa Yesu [YOHANA 20:1,19,26 WARUMI
10:9].
( c ).
Siku ya kuja Roho mtakatifu ,Mwangalizi mkuu wa kazi yote ya Mungu
katika kanisa , ilikuwa siku ya pentekoste ambayo ni Jumapili, siku ya
pili baada ya sabato [MATENDO 2:1]
( d )
Siku ya pentekoste ,Jumapili ndiyo siku ya kwanza ambayo kanisa la
kwanza lilianza mahubiri na watu 3,000 wakaokoka na kuanza kusanyiko la
kwanza la Ibada kanisani [MATENDO 2].
( e ). Wakristo wa kanisa la kwanza walikusanyika Jumapili [MATENDO 20:6-12;1WAKORINTHO 16:1-2].
Sababu
hizi ,zinadhihirisha pia wazi wazi kwamba kuabudu Jumapili
hakukuanzishwa na mfalme CONSTANTINE wala kanisa Katoliki.Hakuna andiko
lolote linalosema mtu yeyote anayeabudu Jumapili ana alama ya 666 ya mnyama.Huo
ni uzushi.Biblia inatupa uhuru wote katika kuchagua siku ya
kumwadhimisha Bwana [WARUMI14:5-6].Vilevile ni muhimu kufahamu kuwa siku
zote ni siku za kujifunza Neno [MATENDO 17:11;2:46].
( 5 ).KUSHIKA SIKU, SIYO NJIA YA KUOKOKAKushika
siku yoyote hata iwe Jumapili, sio njia ya kuokoka.Tunaokolewa kwa
kumuamini Yesu kuwa ni BWANA na MWOKOZI na sio kwa kushika siku yoyote [WARUMI 10:9-10,13].
JE, UNAHITAJI MSAMAHA WA DHAMBI ZAKO ZOTE?
Tunasoma haya katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”. Hii
ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa hakika,
na hivyo kupata wokovu mara moja. Je, kweli utasamehewa? Jibu ni
Ndiyo! Yesu mwenyewe anasema katika YOHANA 6:37,
“……….Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”. Hivyo
kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii, utasamehewa na kupata wokovu.
Je, uko tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia
mbinguni na kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi? (
TITO 3:3-4 ).
Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya toba, mara tu baada ya sala
hii kwa ghafla utawezeshwa kushinda dhambi. Je, uko tayari kuifuatisha
sala hii sasa? Najua uko tayari. Basi sema maneno haya, “Mungu
Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Naomba
unisamehe na kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika
msalabani. Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa. Liandike sasa jina
langu katika kitabu cha uzima mbinguni. Asante kwa kuniokoa, katika
Jina la Yesu, Amen.Tayari umeokoka. Ili uzidi kuukulia wokovu,
hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri
wokovu. ( LUKA 19:9-10)………………………………………………………………………………………………………………………..
Zipo Baraka nyingi kwa
yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa
ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na
kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa
kubonyeza neno“ facebook na twitter” yaliyopo chini ya maelezo haya,
kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za
Mungu zitakuwa nawe.
kwa Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe Fungua
Tovuti : www.bishopzacharykakobe.orgFacebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe
Post A Comment:
0 comments: