Biblia
ni kitabu cha ajabu kuliko vitabu vyote duniani. Kwa nini? Ni kwa sababu jina
lenyewe lina maana ya vitabu au maktaba ya Mungu, yenye jumla ya vitabu sitini
na sita. Tena, Biblia ina waandishi wapatao arobaini, waliotumiwa na Mungu
kuiandika Biblia kwa vipindi tofauti, kati ya muda wa miaka 1500 na 1600,
wakiongozwa na Mungu mwenyewe, hivyo kuifanya Biblia iwe na mwandishi mmoja tu,
yaani Mungu.
Jambo
lingine la ajabu, Mungu aliwatumia waandishi wa fani mbalimbali, mazingira na
nyakati tofauti wakiwemo manabii, wafalme, wakulima, wafugaji, wavuvi, watoza
ushuru, madaktari, wajenzi n. k; hata hivyo Biblia imekuwa na umoja wa ajabu,
bila kuhitilafiana kunakotokana na mazingira wala nyakati. Umoja huu
unatuthibitishia kuwa mwandishi wa Biblia ni mmoja, ambaye amekuwako nyakati
zote za historia ya dunia, yaani Mungu.
“Maana unabii haukuletwa popote kwa
mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa
na Roho Mtakatifu” (2Pet.
2:21).
Mungu
ndiye Alfa na Omega, yaani mwanzo na mwisho, (Uf. 1:17); “Aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja (Uf.4:4), “Niko ambaye Niko” Kut.3:14; Yoh. 8:58. Huyu ndiye
aliyewapa waandishi maneno ya kuandika katika vizazi vyote. Jambo lingine la
ajabu kuhusu kitabu hiki ni kwamba, ni kitabu peke ambacho kimeenea duniani
pote na kusomwa na watu wengi. Pia ni kitabu kilichowatenganisha watu na
kuwafarakanisha kuliko kitabu kingine chochote duniani; lakini wakati uo huo ni
kitabu chenye majibu ya maswali mengi ya wanadamu duniani kuliko kitabu kingine
chochote.
Ili
kuielewa Biblia vema, ni sharti kutumia kanuni ambazo zitalinda umoja wa Biblia
na kuleta maana zisizohitilafiana na kupingana. Masomo muhimu yote duniani kama
vile sayansi au hisabati na mengineyo, yanafundishwa kwa kutumia kanuni maalumu
ili kutunza usahihi wake; vinginevyo kila mmoja angekuwa na majibu yake tofauti
na mwingine. Kwa kuwa tunajua kuwa Biblia ni somo muhimu sana kuliko masomo
yote duniani, sharti isomwe na kufasiriwa kwa kanuni maalumu ili kulinda umoja
wake, na kuepuka athari za kupoteza maana halisi ya Mungu iliyokusudiwa; huku
tukitumia akili zetu za kibinadamu. Kuna mitafaruku mingi sana tunapoingia
katika masuala ya imani, inayosababishwa na mafundisho yasiyozingatia kanuni za
kusoma na kufasiri maandiko ya Biblia. Mungu ni mwaminifu kutoa ufunuo kwa njia
ya Roho kuhusu Neno lake (Yoh.6:63;
1Kor.2:13,16). Lakini kwa kuwa ufunuo ni suala la kiroho na siri kati ya
mwanadamu na Mungu wake, hakuna mtu mwingine wa pembeni awezaye kujua
kinachoendelea. Hii imekuwa sababu ya watu wengi kudai kwamba wamefunuliwa na
Mungu wakati ni mawazo yao wenyewe. Ili kuepuka athari hizi, Mungu ametupa
kanuni zake ambazo zinaweza kumsaidia mtu yeyote hata yule asiyejua mambo ya
ufunuo wa Roho; kwa sababu kanuni ni kanuni, haijalishi umeokoka au la! Kama
ilivyo kwa masuala mengine yoyote yanayohitaji kutekelezwa kwa kutumia kanuni,
haijalishi kuwa unaamini au la, kanuni itafanya kazi yake!
Hebu
nitumie mifano michache ya hesabu za kujumlisha na kuzidisha zenye tarakimu
mbili: 25+25, ukijumlisha kuanzia kushoto kwenda kulia, jawabu lake litakuwa
410; lakini ukijumlisha kuanzia kulia kwenda kushoto, jawabu lake litakuwa 50.
Majawabu yote mawili ni sahihi iwapo hakuna kanuni ya hisabati ya kujumlisha.
Hakuna mmoja kati ya hawa wawili atakayekuwa na ujasiri wa kumkosoa mwenzake
kuwa amekosea iwapo hakuna kanuni inayomhakikishia yeye kuwa yuko sahihi.
Lakini kwa kuwa kanuni ya hesabu hii ni kujumlisha kutoka kulia kwenda kushoto,
basi atakuwa na uhakika kuwa jawabu sahihi ni 50. Uhakika wa jibu hili
unatokana na kanuni ya hesabu za kujumlisha!
Mfano
mwingine: Unapotaka kuhakikisha usahihi wa hesabu ya kuzidisha, ni sharti
kugawa jawabu na tarakimu mojawapo kati ya mbili zilizotumika kuzidisha, kwa
mfano, 6 x 8= 48; na 48 ukigawa kwa 8, jawabu litakuwa 6; hapo unakuwa na
uhakika wa jawabu lako kuwa ni sahihi. Kwa hiyo, bila kuwa na kanuni ya
kuhakikisha usahihi wa jawabu lako, huwezi kujua kama uko sahihi au la. Kutokana
na mifano hii miwili, tunaona jinsi ilivyo muhimu kusoma na kuifasiri Biblia
kwa kutumia kanuni zake, ili kuwa na uhakika wa yale tunayoyasoma na
kuyafundisha, tusifundishe upotofu. “Kila Neno la Mungu limehakikishwa; yeye ni
ngao ya wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; asije akakulaumu,
ukaonekana u mwongo” (Mith.30:5,6).
Je,
tutazipata wapi kanuni za kutuwezesha kusoma na kufasiri Biblia? Jibu la swali
hili ni rahisi kwa sababu, kanuni hizi zinapatikana katika kitabu hiki cha
ajabu, yaani Biblia. Kwa hiyo, haifai mtu fulani kuinuka na kutoa maana ya
maandiko matakatifu kwa kutumia mawazo na akili zake; au kwa kusema, “nadhani,
huenda, bila shaka” au kutumia misimamo ya dini, au mkuu fulani katika dini, au
imani ya madhehebu kwa kusema, “dini yetu inasema hivi” badala ya kutumia
msimamo wa mwandishi mkuu wa Biblia ambaye ni Mungu. “Mkijua neno hili kwanza,
ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu
fulani tu” (2Pet.1:2).
Yesu
alitusaidia sana kutupa mwongozo wa kuielewa Biblia na makusudi yake aliposema,
“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii la, sikuja kutangua,
bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, mpaka mbingu na nchi
zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote
yatimie” (Math.5:17,18).
“…..Hayo
ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni
lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika torati ya Musa, na katika manabii
na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko” (Luka
24:44,45).
“Mwayachunguza
maandiko, kwasababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo
ndiyo yanayonishuhudia. Kwasababu kama mngemwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa
sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake,
mtayaamini wapi maneno yangu?” (Yoh.5:39, 46, 47).
“…..Akiwaonya
mambo yake Yesu, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata
jioni. Wengine waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini” (Mdo 28:23, 24).
Katika maandiko yote haya hapa juu,
tunaupata ukweli ufuatao:
1. Torati, Zaburi na Manabii, ziliandikwa kwa
ajili ya Yesu.
2. Yesu alikuja kuyatimiza yote aliyoandikiwa
katika Torati, Zaburi na Manabii.
3. Yote yaliyoandikwa yataendelea kutimizwa
mpaka hapo mbingu na nchi zitakapoondoka (kuja kwa Yesu mara ya pili)
4. Wanafunzi wake hawakuijua siri hii mpaka
walipofunuliwa akili zao na Yesu, baada ya kufufuka kwake.
Hapa
tunaona kuwa, Agano la kale limekuwa kama ramani ya nyumba iliyochorwa; Agano
jipya linajenga mpango wa Mungu kwa kufuata ramani iliyochorwa na Mungu
mwenyewe katika Agano la kale, kama fundi stadi. Fundi washi anahitaji kujua
jinsi ya kuisoma ramani vema, ili kujenga nyumba kama ilivyokusudiwa na
mchoraji bila kupoteza vipimo au sura ya nyumba. Mitume, manabii, wainjilisti,
wachungaji na waalimu, hao wote ni wajenzi wa kanisa la Mungu. “Maana msingi
mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani
Yesu Kristo” (1Kor.3:11). Hatuwezi
kujenga kwa kutumia mafundisho ambayo Yesu hakutuachia sisi, tukiwa ndio kanisa
lake; naye ndiye mtimizaji wa Torati, Zaburi na Manabii; tutakuwa sawa na fundi
washi anayeacha kuisoma ramani aliyopewa na kuanza kuchora ramani yake. Pia
ikumbukwe kwamba, hata katika mazingira yetu, kuna wajenzi wengi wa nyumba za
kawaida, wasio na uwezo wa kusoma ramani iliyochorwa, ingawa wanaweza kujenga
bila kutumia ramani.
Yesu
alisema, “Torati na manabii vilikuwepo
mpaka Yohana; tangu wakati huo, habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na
kila mtu hujiingiza kwa nguvu” (Luka
16:16).
Alisema
tena, “Kwa maana Manabii wote na Torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana” (Math. 11:13). Katika maandiko haya
mawili tunaona kuwa Torati yote na Manabii wote, ujumbe wao ulilenga kufikia
wakati wa Yohana mbatizaji, ambao pia ulikuwa ni wakati wa Yesu mwenyewe
duniani; lakini baada ya muda huo kupita, unaobaki ni muda wa utekelezaji wa
yale yote yaliyoandikwa katka Agano la kale. Yesu alitekeleza yale yaliyomhusu
kwa wakati wake; yaliyosalia yalitekelezwa na mitume; baada ya hapo, kanisa
limeendelea kutekeleza yote yaliyobaki na kulihusu, litaendelea na kazi hiyo
mpaka wakati wa kuja Yesu mara ya pili, yaani mwisho wa dunia. Yohana alikuwa
ndio mwisho wa unabii; hakuna unabii mwingine uliotolewa baada ya Yohana
mbatizaji, isipokuwa Injili za Yesu, nyaraka za mitume na ufunuo, ambamo ndani
yake tunapata ufafanuzi au kuisoma ramani ya Agano la kale, iliyochorwa kuishia
mwisho wa dahari, yaani kuja kwa Yesu mara ya pili, au mwisho wa dunia. Kwa
maneno mengine ni kusema kwamba, hakuna ramani nyingine iliyochorwa au
itakayochorwa baada ya Yohana mbatizaji, bali ni ujenzi utakaoendelea. Zaidi ya
hayo ni kusema kuwa, hata kitabu cha ufunuo wa Yohana hakileti jambo lolote
lililo jipya, ambalo halikunenwa na Torati, Zaburi, Manabii, Yesu na mitume.
“…..Na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu
haitalishinda” (Math.16:18).
Agano
la kale lina sehemu kuu tatu ambazo ni Torati, Zaburi na Manabii; pia Agano
jipya lina sehemu kuu tatu zinazofafanua Agano la kale, nazo ni Injili, Nyaraka
na Ufunuo. Ni lazima sehemu hizi zikubaliane katika maana ya kile
tunachokitafuta. Kwa sababu ya umoja wa Biblia ulivyo, haifai kuitenganisha
vipande vipande, hata kupoteza maana yake. Kwa kufanya kosa hilo, tutasababisha
andiko moja kufasiriwa kwa maana nyingi zilizo tofauti, na kujenga mafundisho
dhaifu ndani ya kanisa la Yesu Kristo, na kulifanya lishindwe kwa kushambuliwa
na milango ya kuzimu. Yesu alirehemu kanisa lake!
Msomaji
anapoijua siri ya umoja wa Biblia, na jinsi ambavyo haiwezi kutofautiana kutoka
andiko hata andiko; au mwandishi na mwandishi; au karne na karne; maana
mwandishi mkuu ni mmoja yule yule. Kujua huku kutamsaidia msomaji kutokuielewa
vibaya Biblia, au kupata maana ambayo itapingana na maandiko mengine. Ukichukua
kizibo cha chupa halafu ukakosea kukikalisha katika chupa, utashindwa kufunga
hata ukadhani sio kizibo chake. Kama utalazimisha kufunga bila kujua kwamba
umekosea kukikalisha inavyotakiwa, hatimaye hata wakati wa kufungua unaweza
kushindwa, na ukalazimika kukivunja. Tatizo si la kizibo, tatizo ni la mfungaji
ambaye hakujua jinsi ya kukikalisha inanyotakiwa. Vivyo hivyo, ndivyo ilivyo
katika Neno la Mungu! Wasomaji wengi wanadhani kuwa Biblia ni ngumu sana
kuielewa; ingawa kuna ukweli katika jambo hili, kwa sababu yatambulikana kwa
jinsi ya roho; lakini tatizo kubwa ni kwamba mtu anaisoma Biblia huku akiwa
ametanguliza mawazo binafsi na mapokeo ya kidini, hivyo kushindwa kuiunganisha
ili kuipata maana iliyo sahihi.
Wayahudi
waliyajua sana maandiko ya torati na kujisifu katika jambo hilo; lakini Yesu
alipokuja walishindwa kuyaunganisha maneno ya torati na ya Yesu, wakiyafanya
kuwa ni vitu viwili tofauti, na kushindwa kabisa kumwelewa Yesu ni nani.
Walidai kumjua Yesu, lakini walimkataa Yesu alipojiita kuwa ni Mungu. Mifano: Kumb.8:3 na Math.4:4; Isa.6:9,10 na Math.13:14,15; Kumb.18:15 na Yoh.5:47;
Zab.82:6 na Yoh.10:34; Yoeli 2:28,29 na Mdo 2:16-21; Zab.16:8-11 na Mdo 2:25-28; Zab.110:1 na Luka 20;41-44;
Luka 24:44-46. Haya ni baadhi ya maandiko machache ambayo Yesu
aliwakumbusha Wayahudi kwamba, yale waliyokuwa wakiyasoma katika Torati, Zaburi
na Manabii, yalimhusu yeye na wasingeweza kumtenganisha na maandiko hayo. Kwa
hiyo, waliosoma agano la kale bila kumwona Yesu, na wale waliomwona na kumsikia,
na sisi tunaosoma sasa, hakuna tofauti yoyote. Paulo katika waraka wake
anasema, “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya
mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini hatumtambui
hivi tena” (2Kor.5:16).
Mtume
Yohana naye katika waraka wake anasema, “Lile lililokuwako tangu mwanzo,
tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu
ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima; na uzima huo ulidhihirika, nasi
tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa
kwa Baba, ukadhihirika kwetu. Hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na
ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi; na ushirika wetu ni pamoja na
Baba , na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo” (1Yoh.1:1-3).
Mtume
Petro naye anasema, “Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa
hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye
utukufu….Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu
walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale
waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo
hayo malaika wanatamani kuyachungulia.” (1Pet.1:8,12).
Mwandishi
wa kitabu cha Waebrania anaandika kwa kusema, “Mungu ambaye alisema zamani na
baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku
hizi amesema na sisi katika mwana , aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa
yeye aliufanya ulimwengu” (Ebr.1:1).
“Na
watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;
kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao
wasikamilishwe pasipo sisi” (Ebr.11:39,40).
Waandishi
hawa wote wanakiri jambo moja lile lile kwamba, hakuna tofauti kati ya watu
walioisikia torati ya Musa, zaburi, manabii na wale waliomsikia Yesu ana kwa
ana na kumwona; pia na sisi tuliomwamini bila kumwona kwa jinsi ya mwili. Sisi
sote tumelipokea neno lile lile lililo sawa kwa njia ya imani iliyo katika
Kristo Yesu. Mungu wetu hawezi kubadilika-badilika katika maneno yake; ni yeye
yule, jana na leo na hata milele. Huu ndio umoja wa Biblia ulio imara na
hauwezi kuyumbishwa na mwanadamu yeyote. Mtume Paulo aliwaonya wakristo wa
Kolosai kuhusu mchanganyo huu wa mafundisho yanayoingizwa kwa ujanja wa watu
kwa kusema, “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na
madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya
awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo” (Kol.2:8).
Mungu
amekuwa akijifunua kwa watu wake kwa njia tofauti-tofauti kulingana na majira
na wakati; lakini akiwa ni yeye yule. Alijidhihirisha kwa watu wa kale kama
Mungu Baba, Mwenyezi, Yehova, Niko ambaye niko, Muumba wa mbingu na nchi, Mungu
wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, Baba wa milele, na mengine mengi; lakini zamani
hizi amejidhihirisha kama Mwana, na majina hayo yote pia ni yake, kuonyesha
kwamba ni Mungu yeye yule. Alifanya agano la kale, zamani hizi amefanya agano
jipya, lakini Mungu ni yeye yule. Kwa hiyo maagano haya mawili hayapingani,
bali kila moja linaleta tafsiri nzuri kwa lingine. Ili kulielewa vema agano la
kale, unahitaji kulielewa agano jipya; kadhalika, ili kulielewa vema agano
jipya, unahitajika kulielewa vema agano la kale, kwa kuwa mwandishi wa maagano
haya ni yule yule mmoja.
Somo
letu litaendelea wakati mwingine……………………
Usisahahu kufollower, comment, like na kushare kwa wapendwa wengine.
Source: Mwalusambo International Ministry
Ni Mimi ndugu yako Counselor Nicholaus Simon.
Kiungo katika mwili wa kristo.
Kwa msaada ushauri au maswali
Whatsap: +255 766 635 382/+255 659 990 111
Email: pataufahamu@gmail.com/
info@mwalusambo.or.tz
Post A Comment:
0 comments: