BIBLIA TAKATIFU |
Katika utangulizi
fahamu mambo matatu makubwa yafuatayo:
1.
Wewe ni balozi wa Kristo na kwa ajili ya Kristo hapa ulimwenguni.
“Basi tu wajumbe (mabalozi) kwa ajili ya Kristo….” (2Wakorintho
5:20)
2.
Ikiwa wewe ni balozi, basi wewe si wa ulimwengu huu kama vile Kristo
asivyo wa ulimwengu huu (Yohana 17:16). Uraia wako au wenyeji wako si wa hapa
ulimwenguni, bali ni wa nyumbani mwake Mungu. “ Basi tangu sasa ninyi si
wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa
nyumbani mwake Mungu.” (Waefeso 2:19)
3.
Ikiwa wenyeji wako ni mbinguni katika ufalme wa Mungu, nyumbani mwake
Mungu unafanya nini hapa ulimwenguni? Kuna sababu kubwa za wewe kuwa hapa
ulimwenguni. Ni kwa sababu umetumwa kama Kristo alivyotumwa. “Kama vile
ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.”
(Yohana 17:18)
Tunajua
hukutumwa hapa ulimwenguni ili ufanye kazi peke yako. Tuko hapa ulimwenguni
tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu. “ Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na
Mungu…” (1Wakorintho 3:9)
Huwezi
ukawa mfanyakazi pamoja na Mungu bila ya kuwa mtendaji wa Neno; kwa kuwa Mungu
ni Neno (Yohana 1:1). Kuwa balozi wa Kristo maana yake ni kuwa mwakilishi wa
Neno; kwa kuwa Kristo ni Neno (Yohana 1:14). Uwakilishi huu hauonekani kwa
sabatu watu wa Mungu walio wengi hawaelewi namna ya kuwa watendaji wa Neno ili
Neno lionekane hapa ulimwenguni.
Katika
somo hili tunajifunza juu ya namna ya kuwa mtendaji wa Neno, ili ufanye kazi ya
ubalozi wa Kristo vizuri. Ni maombi yetu kwa Mungu ya kuwa somo hili lizae
matunda katika maisha yako ya kiroho katika Kristo.
UMUHIMU WA KUWA MTENDAJI WA
NENO
Ikiwa
kuna swali kubwa ambalo linawatatanisha wakristo wengi, basi ni swali la kukua
kwa imani yao ya kikristo. Wengine wanaita ni kukua kiroho kwa
wakristo.
Ukiwauliza wakristo wengi ya kuwa ni tatizo gani wanaloliona kubwa,
linalowakwamisha katika maisha yao ya kikristo; walio wengi watasema ni tatizo
la imani.
Tatizo
hili linatokea kati ya watu wa Mungu, kwa kuwa hawajui imani ni nini, na kwamba
inapatikanaje. Na wengine wamekuwa wakijitahidi kuomba kwa Mungu kwa muda mrefu
ili imani zao zikue, lakini bila mafanikio ya kuridhisha.
Kwani
imani maana yake nini?
“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana
ya mambo yasiyoonekana” (Waebrania 11:1)
Katika mstari huu tunaona mambo mawili
makubwa.
- Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo; na 2. Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana.
Imani
inakupa uhakika sasa juu ya mambo ambayo unayoyatarajia. Imani inaweka wazi
(bayana) mambo yasiyoonekana.
Chanzo
cha imani ndicho pia chanzo cha uhakika wako katika maisha ya kikristo; pia ni
chanzo cha uwazi wa mambo ya rohoni yasiyoonekana. Chanzo cha imani ndicho pia
kinakupa uhakika wa maisha yako ya wokovu.
Chanzo cha imani ni nini? Imani huwa mtu anaipataje? Kwa
maneno mengine unaweza ukauliza, chanzo cha uhakika ulio nao wa wokovu na
ukristo ni kitu gani?
Mara
nyingi watu wa mataifa huwa wanauliza maswali yafuatayo: Mtu atawezaje kuwa na
uhakika wa kuokoka akiwa hapa duniani? Mtu atawezaje kuwa na uhakika ya kuwa
amesamehewa dhambi wakati bado yupo duniani?
Maswali
haya huwa yanatokea mara kwa mara kwa sababu hawajui uhakika wa mambo hayo
unatoka wapi. Laiti wangejua, basi wangekuwa na usemi mwingine midomoni mwao juu
ya wokovu.
Biblia
inasema wazi kabisa kwamba yote yawezekana kwake aaminiye (Marko 9:23). Na kama
biblia ambayo ni Neno la Mungu inasema yote yawezekana kwake aaminiye, mwanadamu
ni kitu gani mbele za Mungu hata apinge?
Basi
imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo
yasiyoonekana.
Imani
chanzo chake ni nini?
“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa Neno
la Kristo” (Warumi 10:17)
Mstari
huu wa biblia unatufahamisha kuwa imani chanzo chake ni kusikia Neno la Kristo.
Hii ina maana ya kuwa uhakika wa wokovu, au ukristo na misingi yake unapatikana
kutokana na kusikia Neno la Kristo.
Watu
wengi utawasikia wakiomba na wakati mwingine kwa kufunga na kwa kuomboleza ili
Mungu awape imani. Lakini mabadiliko katika maisha yao hayaonekani.
Biblia
inatufahamisha wazi kabisa kuwa ‘imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja
kwa Neno la Kristo. Imani huja kwa Neno la Kristo. Imani huja kwa kusikia Neno
la Kristo!
Watu
wengi wamekuwa wakiomba imani na wanapoona haionekani katika maisha yao,
wanaanza kumkemea shetani bila mafanikio yoyote. Watu wengi wanajikuta wamo
katika hali ya kukwama kiroho na kudumaa kwa sababu hawajawa wasikiaji wa Neno
la Kristo.
“Lakini iweni watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali
mkijidanganya nafsi zenu” (Yakobo 1:22)
Kwa
mstari huu tunapata upeo mkubwa kidogo juu ya chanzo cha imani. Tunaweza sasa
kusema, imani chanzo chake ni kusikia na kulitenda neno la Kristo.
Imani
huja kwa kulisikia na kulitenda neno la Kristo. Uhakika tulio nao katika Njia
hii ya wokovu katika Kristo unatokana na Neno la Kristo tulilolisikia na
kulitenda.
Kuwa
msikiaji tu wa Neno la Kristo haitoshi bila ya kuwa mtendaji wake. Neno la
Kristo lililosikiwa na mtu, lisipowekwa katika matendo haliwezi kuonekana na
watu wengine.
Watu
wengi sana ni wasikiaji wa Neno la Kristo, utawakuta makanisani, wakiliskiliza
Neno, utawakuta kwenye mikutano ya kiroho pia utawakuta kwenye semina za Neno la
Mungu; lakini watendaji wa Neno hilo la Kristo wanalolisikiliza ni wachache
sana.
Wasomaji wa biblia ni wengi sana, lakini watendaji wa Neno hilo
wanalolisoma ni wachache sana. Na kwa sababu hii siku hizi ni vigumu sana kuweza
kutofautisha kati ya mkristo na mtu wa kawaida, au mtu aliyeokoka na mtu
asiyeokoka, kwa kuwaangalia matendo yao.
Mtu
anajiita mkristo au ameokoka lakini matendo yake yako mbali sana na Neno la
Kristo. Huu ni unafiki mkubwa – unaohitaji kutafutiwa ufumbuzi.
Wakati
umefika, na wakati wenyewe ndiyo huu wa watu kujulikana maisha yao ya kikristo
yamesimama katika msingi upi. Ikiwa msingi huo ni Neno la Kristo, basi neno hilo
ni budi lionekane katika matendo yao ya kila siku.
Imeandikwa; “Lakini iweni watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu,
hali mkijidanganya nafsi zenu”.
Kuwa
mtendaji wa Neno la Kristo maana yake nini?
Kuwa
mtendaji wa Neno la Kristo maana yake ni kuwa mtumiaji wa Neno la Kristo
ulilolisikia. Kuwa mtendaji wa Neno ni kulitumia Neno na Neno nalo likutumie
wewe.
Wewe
unakuwa ndani ya Neno la Kristo na Neno la Kristo linakuwa ndani yako. Neno la
Kristo lililondani yako unalitumia kuwa utukufu wa Mungu. Na wewe ukiwa ndani ya
Neno la Kristo, unatumiwa na Neno hilo kumtwalia Mungu utukufu.
Ndiyo
maana Yesu Kristo alisema;
“Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza
kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani
yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake,
huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu
asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na
kuyatupa motoni, yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa
ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu,
kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu,” (Yohana
15:4-8)
Kwa
mistari hii tunaona kuwa imani ya kikristo ni matokeo ya mtu kuunganishwa na
Kristo mwenyewe. Na matokeo ya matunda mazuri ya kikristo yanategemea jinsi
ambavyo mtu anavyolisikia na kulitenda Neno la Kristo.
Pia,
tunaona kuwa matokeo ya maombi ya mtu aliye mtendaji wa Neno la Kristo ni mazuri
na yenye mafanikio kuliko matokeo ya mtu aliye msikiaji tu wa Neno na wala si
mtendaji.
Watu
wengi ni wasikiaji wa Neno la Kristo, lakini hawalitumii wala Neno haliwatumii
kabisa. Na wengine ni wasikiaji na watumiaji wa Neno la Kristo katika sehemu
chache tu za maisha yao.
Lakini
imeandikwa wazi kabisa kuwa hao wanajidanganya nafsi zao wenyewe, wala
hawamdanganyi Mungu, shetani wala mtu yeyote, bali wao wenyewe; kwa kuwa
wamekuwa wasikiaji wa neno la Kristo lakini si watendaji.
Na
ndiyo maana Roho wa Mungu aliomboleza kwa kupitia kwenye kinywa cha Nabii Hosea
akisema; “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ……” (Hosea
4:6)
Na Yesu
Kristo, pia, alikuwa na haya ya kusema juu ya watu wa namna hiyo:
“Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu”
(Mathayo 22:29)
Ni
kweli kabisa kuwa kanisa ambalo ni mwili wa Kristo, limekuwa katika hali ngumu
kiroho kwa sababu ya kukosa maarifa ya Mungu yanayotokana na kulisikia na
kulitenda Neno la Kristo.
Imeandikwa;
“Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali
mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si
mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana
hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.” (Yakobo
1:22-24)
Tunakumbuka wakati fulani tulikuwa tunaongea na mtu mmoja juu ya
maisha yake ya wokovu. Tulimuuliza swali hili; “Ni kitu gani kinachokutofautisha
wewe na mkristo mwingine wa kawaida?”
Akasema; “Ni kwa sababu nimemwamini Mungu”
Tukasema; “ Hiyo haitoshi kwa sababu hata wao wanamwamini Mungu.
Je! hujasoma ya kuwa mashetani nao wanaamini na kutetemeka?”
Akauliza; “Sasa kitu gani kinacholeta tofauti?”
Tukasema; “ Ni maisha yako mapya yanayopatikana baada ya kumpokea
Kristo moyoni mwako”.
Tukamsomea waraka wa pili kwa Wakorintho Sura ya tano na mstari wa kumi
na saba, unaosomeka hivi; “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani
ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa
mapya”
Unapompokea Kristo (Neno) moyoni mwako unapewa uzima wa Mungu ndani
yako, na tabia mpya inayoongozwa la Neno la Kristo.
Ni
vigumu sana kumtofautisha mtu wa Mungu na mtu wa kawaida kwa kusikia wanachosema
tu peke yake. Ni lazima maisha mapya ndani ya Kristo, maisha ya wokovu
yaandamane na tabia mpya.
Tabia
mpya hiyo haionekani siku hizi kwa sababu, watu hawajawa watendaji wa Neno.
Yakobo anauliza:
“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini
hana matendo? Je! ile imani yaweza kumwokoa?.....
Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini
mwake” (Yakobo 2:14,17)
Hii
maana yake mtu asipokuwa mtumiaji wa Neno la Kristo, anaonekana kama vile si
mkristo. Utafahamu ni mkristo kwa sababu anakwenda kanisani jumapili au
jumamosi, lakini si kwa sababu umeona matendo ya kikristo maishani
mwake.
Na hata
watu wengi waliookoka wanaliabisha Jina la Bwana kwa kujiita wao ni watu wa
Mungu, watoto wa Mungu, wana wa mfalme, watumishi wa Bwana; kwa sababu matendo
yao hayafanani na maneno wanayosema.
Yafaa
nini basi, mtu kusema ameokoka wakati bado anatawaliwa na matendo ya dunia?
Yafaa nini, basi mtu kusema yeye ni mkristo, wakati maisha yake yana matendo
kama ya mtu asiyemjua Kristo?
“Lakini mtu atasema, wewe unayo imani, nami ninayo matendo.
Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu KWA NJIA YA
MATENDO YANGU”. (Yakobo 2:18)
KWA
NJIA YA MATENDO watu watajua kuwa imani yako ni ipi. Kwa njia ya matendo yako
watu watajua ya kuwa wewe in mkristo au La.
Imani
yako na ijulikane mbele za watu kwa njia ya kuwa mtendaji wa Neno.
Umefanyika kuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo, kwa hiyo matendo yako
ni mapya, pia, matendo ya kale yamepita. Kwa matendo yako yaliyosimama ndani ya
Neno la Kristo, ulimwengu utajua ya kuwa umeokoka au La.
“Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao
waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba
imani pasipo matendo haizai?....
Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani
pasipo matendo imekufa” (Yakobo 2:19,20,26)
Mashetani yanamjua Mungu ya kuwa ni mmoja, na yanaamini hivyo na
kutetemeka. Mashetani yana hofu ya Mungu, lakini watu wengi hawana hofu ya Mungu
ndani yao.
Kwa
kutokuwa mtendaji wa Neno, unajikuta kuwa utamu wa maombi, utamu wa kushuhudia,
utamu wa Neno la Mungu unafifia ndani yako.
Imani
haiji kwa kuomba, kukua kwa imani yako hakutakuja kwa kuomba, bali huja kwa
kusikia na kulitenda Neno la Kristo.
Si
kwamba tunadharau sehemu ya maombi katika maisha ya mkristo, la hasha. Maombi ni
muhimu sana kwa mkristo kama vile petroli ilivyo muhimu kwa ajili ya
gari.
Ukijaza
petroli kwenye gari haina faida yoyote hadi hapo utakapoingia ndani ya gari na
kuliendesha toka mahali lilipo na kwenda mahali pengine unapotaka.
Maombi
bila kuwa mtendaji wa Neno, ni bure. Maombi PAMOJA na utendaji wa Neno vinaleta
mafanikio makubwa katika kukua kiroho. Neno ndilo linakuongoza unapotaka kusogea
kiroho.
Maombi
PAMOJA na utendaji wa Neno ni muunganiko wenye maana kubwa katika kuifanikisha
kazi yetu tuliyotumwa kuifanya hapa ulimwenguni; kazi ya kuwa wajumbe (mabalozi)
kwa ajili ya Kristo.
Lakini
tunajua kuwa “sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu” (1Wakoritho 3:9). Kuwa
mfanyakazi pamoja na Mungu maana yake ni kuwa mfanyakazi pamoja na Neno, kwa
sababu Mungu ni Neno (Yohana 1:1)
Kuwa
mfanyakazi pamoja na Neno maana yake ni kuwa mtenda kazi pamoja na Neno; ni kuwa
mtendaji wa Neno; ni kuwa mtumiaji wa Neno.
Si
kwamba watu wanapenda kutokuwa watendaji wa Neno, bali wengi hawafahamu ni namna
gani ambavyo watafanya ili neno la Kristo walilolisikia au kulisoma lionekana
katika maisha yao.
....fuatilia sehemu ya pili baada ya siku chache.
....fuatilia sehemu ya pili baada ya siku chache.
Post A Comment:
0 comments: